Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nianze kwanza kuipongeza Wizara, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na timu kwa ujumla kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakifanya, pia niipongeze Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa taarifa yao nzuri ambayo wamefanya uchambuzi wa kina nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru katika taarifa zote zinaonyesha kwamba mchango wa ukuaji wa sekta ya viwanda Tanzania umefika asilimia 8.9 sasa katika mazingira tuliyonayo asilimia 8.9 ni ukuaji bado huko chini hauendani na hali halisi ya changamoto tulizonazo na mahitaji tuliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma nchi yetu ilibahatika, tuliweza kujenga viwanda vya aina zote, toka tumepata uhuru tulijenga karibu viwanda vya aina zote. Tulikuwa na viwanda kwanza ni sera ya Chama cha Mapinduzi sasa hivi, Chama cha Mapinduzi kimetoa sera ni moja ya malengo kwamba lazima tujenge viwanda na viwanda ukiviangalia ndio vitatoa suluhu ya matatizo yote tuliyonayo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huko nyuma tulikuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao. Baba wa Taifa alijenga viwanda karibu vyote vilikuwepo! Tulikuwa na viwanda vya kuchakata nyama, viwanda vya kuongeza thamani ya nyama, viwanda vya ngozi vilikuwepo na mazao mbalimbali ya Ngozi, viwanda vya misitu na mbao vilikuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mashine viwanda vya tools za uzalishaji vilikuwepo vililjengwa, mpaka tulipofika mwaka 1974, 1975 karibu viwanda vyote vilikuwepo, viwanda vya nguo vilikuwepo, viwanda vya korosho vilikuwepo, viwanda vya mafuta vilikuwepo, viwanda vya kila kitu vilikuwepo vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabati yalikuwepo, misumari yaani hatukukosa kiwanda cha aina yoyote. Swali ambalo tunatakiwa tujiulize ni nini kilitokea viwanda hivyo vyote vikafa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijua pale tulifeli nini ndipo tutakuwa na mkakati ambao unafaa katika kujenga viwanda kwa sasa, bila kuelewa tulikotoka hatuwezi kujenga viwanda! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara, nimesoma taarifa nafurahi wana mikakati mizuri lakini nataka hasa wanisaidie ni upi mkakati wa Wizara wa kuongeza viwanda na ajira hapa nchini ambao kweli huo mkakati tukiuangalia kama Bunge tutaridhika kwamba nchi hii itatoka hapa tulipo tutafika mahali ambapo tunataka kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la Pili ni upi mkakati wa Wizara wa kuongeza tija na thamani ya bidhaa zetu! Bidhaa zetu ni duni haziwezi kuimiri ushindani katika soko la dunia. Sasa mkakati wetu tunaouweka ni upi ili tupate bidhaa zitakazoweza kushindana katika soko la dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la Tatu ni upi mkakati wa Wizara wa kuongeza biashara ili tupate fedha nyingi za kigeni kwa sababu biashara ndio zinazoleta fedha nyingi za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la Nne, ni upi mkakati wa Wizara wa kuja na Mfuko wa Kujenga Viwanda? Hapa tutaimba! Tutaimba! hivi mfuko wa kujenga viwanda hivyo huko wapi? Je tutajenga viwanda hivyo kwa kuzungumza kwa kuhamasisha tu, au lazima tutengeneze mazingira ambapo watu wanaweza wakapata mtaji, wanaweza wakapata fedha na tunaweza tukajenga viwanda eneo tukatengeneza kabisa tukajenga baadhi ya viwanda, tukawavutia wawekezaji, wao waje na mitaji, waje na mashine lakini tuwe tumeshajenga miundombinu yote pale! Upi hasa mkakati ambao tumeuweka, hapo unafikiri ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni upi mkakati ambao tumejipanga kama wizara kuhakikisha kwamba tunatumia fursa zilizopo. sasa hivi, DRC wanajiunga Afrika Mashariki. DRC ni soko kubwa, tumejipangaje sasa kuhakikisha hii DRC inapokuja tunaenda kufanya biashara tunatumia fursa tuliyonayo tuweze kuchukua lile soko la DRC. Hili ni suala nafikiri ni la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni upi mkakati wa Wizara wa kuongeza ubunifu. Tunayo SIDO, naelewa nimesoma yote lakini inatosheleza kuja na ubunifu tukawa wabunifu wa kutosha? Kwa hiyo nilikuwa nadhani tufike mahali sasa kama nchi tuangalie sekta ya viwanda na biashara ndiyo sekta mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuchumi tunasema uzalishaji una maeneo matatu, kuna viwanda, biashara, huduma, hizo zote ni biashara. Sasa basi kwenye viwanda tuna viwanda mama, lakini tuna viwanda kwanza vile vya kuchakata vya kutafuta malighafi yaani tunaita extractives industries ambayo tuna kilimo, mifugo, uvuvi, madini na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo vyote ni kwa ajili ya kutafuta malighafi, halafu tunakuja na viwanda sasa vya kuongeza thamani hizo malighafi ambayo tunayo, sasa hivi unajenga kiwanda cha nguo Tanzania unataka upate pamba, pamba haijazalisha kwa hiyo ina maana kama hatuta-link viwanda na biashara na kilimo hatutaweza kufanikiwa, hatuwezi kufika. Kama hatuta-link viwanda na biashara na madini hatuwezi kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatuta-link viwanda na ufugaji na uvuvi hatutaweza kufanikiwa, kwa hiyo utakuta kwamba Wizara ya Viwanda ni mama lakini lazima ishirikiane na hizi Wizara, mkakati uwe mmoja, hapo tutaweza kufikia ile ajenda tunayoitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakwenda pale kwenye biashara, biashara inaweza ikawa ndani inaweza ikawa biashara ya nje, inaweza ikawa ni wholesale inaweza ikawa retail, zile biashara zote ni sehemu za ajira tukipanua biashara vijana wetu wote watafanya kazi, watakuwa na ajira hatutakuwa na tatizo la ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni huduma, kuna huduma za elimu, kuna huduma za afya.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Hasunga, malizia sentensi yako.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninachotaka kusema ni kwamba kwenye huduma huku ndiyo tunatakiwa tutumia hiyo nafasi. Kwa mfano, sasa hivi tumejenga vyuo vya elimu vingi sana hapa nchini viko zaidi ya 30, vile vyuo tunatakiwa tuweke mazingira vidahili wanafunzi kutoka nchi za nje ili watuletee fedha za kigeni na nchi itapata hela nyingi sana. Ninaamini kwa kufanya hivyo tutaweza kupata mchango mkubwa na uchumi wetu utakua kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba kuunga mkono hoja, nawapongeza lakini nataka waje na mikakati madhubuti ambayo Bunge hili litaamini na litaweza kuyapitisha kwamba sasa tunaenda kujenga uchumi wa viwanda, tunaenda kufanya biashara, tunaenda kuongeza uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)