Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwa uchache kwa habari ya hoja iliyopo mbele yetu inayohusu uwekezaji viwanda na biashara, mimi ningependa kuchangia eneo moja tu pengine mawili hasa upande wa stakabadhi za ghala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulipata fursa ya kutembelea Mikoa ya Kusini kwa maana ya Mtwara, Ruvuma pamoja na Lindi kujionea ni namna gani mfumo wa stakabadhi za ghala unafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tulijiridhisha vya kutosha pasipo shaka kwamba mfumo huu ni mzuri na unaweza kuisaidia nchi kuweza kufanya shughuli za uratibu unaotokana na shughuli hasa za mazao. Tulivyoangalia ule mfumo ule kwanza unawasaidia sana wananchi kuweza kupata soko la Pamoja, wanavyojiunga kwenye vikundi inasaidia kutafuta soko kwa haraka lakini kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulichoona kwamba unasaidia utunzaji wa mazao katika maeneo yenye viwango vizuri kwenye maghara na hivyo inasaidia mazao kutokuharibika, kwa sababu ukiangalia katika maeneo mbalimbali namna ambavyo tunatunza mazao yetu imekuwa ikisababisha mazao yetu kupata sumu kuvu. Kwa hiyo, kwa mfumo huo wa kutumia stakabadhi za ghala inasaidia sana mazao yetu kutunzwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho tuliona kwamba huu mfumo unalinda wazalishaji wadogowadogo, kinachofanyika ni kwamba wenye fedha wafanyabiashara wa mazao ni rahisi kwenda kuokotaokota mazao kwa wakulima wadogowadogo mwenye magunia mawili, matatu, kwa hiyo unakuta kwamba inawanyonya kwenye bei, lakini kama wakiweza kuuza kwa pamoja inawasaidia kupata bei nzuri. Kwa hiyo ni mfumo mzuri ambao mimi nimeona unafaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninachokiona kwamba kwenye huu mfumo kumekuwa kuna malalamiko mengi kwamba wananchi mazao yao wakati mwingine hayapimwi katika vipimo rasmi lakini kwa kupitia mfumo huu inasaidia sana wananchi waweze kupima mazao yao katika vipimo ambavyo ni rasmi na vinaweza kuwasaidia wao kuweza kupata bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani tulishaweza kusikia Mzee Mangula alikuwa analima viazi akawa analalamika kwamba wananunua kwa lumbesa lakini kwenye mfumo huu sasa inasaidia kwa sababu tunakuwa na mizani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilichokiona kingine ni kwamba wananchi wanaweza kupata elimu ya pamoja, kama watu wamekaa katika vikundi ni rahisi Maafisa Ugani, Maafisa Kilimo kuja kuweza kuwaelimisha kwa hiyo ni jamba zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niliona jambo lingine zuri katika mfumo huu kwamba pembejeo zinaweza kununuliwa katika maeneo ya uhakika kuliko tunavyoona sasa mtaani kuna viuatilifu na pembejeo feki, lakini kwa kupitia mfumo huu wa stakabadhi za ghala ni rahisi sana kuweza kusaidia watu kupata pembejeo katika maduka ambayo ni rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nililiona, kwa sababu katika safari ile pia tulikuwa na taasisi za fedha, kwa hiyo watu wakikaa katika mfumo huu wa stakabadhi za ghala inasaidia sana kuwa accessible kirahisi na hizi benki zinaweza kuwakopesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni changamoto zipi ambazo tuliziona, tulivyotembelea pale wananchi wengi walitoa shuhuda wao kwamba maisha yao yameboreka, wamejenga nyumba wanasomesha Watoto, lakini changamoto kubwa ambayo tuliiona ni kwamba kumekuwa na ucheleweshaji wa malipo ya fedha, kwa hiyo unakuta kwamba wanapeleka bidhaa leo lakini anaweza akalipwa baada ya miezi mitatu, hiyo inawachelewesha wakati mwingine kufanya mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tuliliona uaminifu kwa wale watunza maghala, unakuta kwamba umeleta mzigo wako labda wa korosho, wale wasimamizi wanasema pengine korosho zako zilikuwa na unyaufu wa asilimia fulani, kwa hiyo ni changamoto nyingine. Lingine ambalo nililiona ni kwamba kuna changamoto ya maghala ambayo hayana viwango, hizo ni changamoto tatu ambazo tuliziona. Sasa ni nini mapendekezo yangu:

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho niliona ni kwamba mapendekezo ambayo mimi ninayatoa hivi Vyama Vikuu viwe na mtaji angalau wa kulipa asilimia fulani wakati mkulima anavyoleta mazao yake ili kuweza kumudu yale mahitaji madogomadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninashauri kwamba hivi vyama viwe na uwezo wa kununua angalau pembejeo za kuanzia ili wanachama wao waweze kupata pembejeo kwa wakati angalau zile za kuanzia. Pia benki ziangalie kutoa mikopo kwa wakati, maana hili pia lilikuwa ni lalamiko ambalo nililiona wananchi wanasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tutengeneze maghala yenye viwango, kwa sababu unaweza ukaona kwenye kutunza kwa mfano mbaazi haziwezi kutunzwa katika mazingira fulani kwa muda mrefu yanaweza kuharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine vyama viwe na vipimo vya kuangalia unyevu kwenye mazao hiyo ni mapendekezo ambayo naona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wakala wa vipimo wahakikishe mara kwa mara wanapita kukagua ile mizani kuona kwamba inapima vizuri kwa sababu ile mizani imekuwa na tabia ya kuchezewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu pia iendelee kutolewa hasa kwa viongozi na sisi wanasiasa, maana inaonekana kwamba huu mfumo bado hatujauelewa, wakati mwingine pengine interest zetu, wakati mwingine pengine atuelewi tu mfumo, mimi nilivyouona kwanza utawasaidia wananchi pamoja na Serikali kupata zile tozo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuwa na uhakika kwamba kama nchi fulani inataka mazao ya kiasi fulani ni rahisi kuweza kujua kwamba Songea tuna dengu kiasi fulani tuna mbaazi kiasi fulani ni rahisi kufanya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuwe na vyama vichache vyenye nguvu badala ya kuwa na vyama utitiri ambao wakati mwingine ni utapeli. Tukiwa na vyama vichache vyenye nguvu vinaweza kufanya mambo yake vizuri. Tumeona vyama kule Mbinga tumekwenda, kule Namtumbo wanajenga sasa hivi kiwanda chao cha kutengeneza vifungashio ni kwa sababu ni viwanda ambavyo vimeimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, riba kwenye Benki angalau ziendelee kuwa chini kwa sababu hii pia ni changamoto kubwa ambayo tuliiona. Mfumo wa stakabadhi za ghala pia napendekeza uende nchi nzima nina fahamu kupokea au adoption mara nyingi ni shida sana hapa nchini, hata wakati tunaanza LUKU walikuwa wanakataa lakini sasa ndio imekuwa kitu kizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naona katika mapendekezo minada iwe ya wazi, yaani minada siyo tu mtu anakuja na karatasi kwenye boksi mnada ufanyike kwa uwazi kama inavyofanyika ukienda wakati mwingine sokoni watu wanauza mia tano, mia sita, mnada ukifanyika wazi ni rahisi watu kupandisha bei. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia. (Makofi)