Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru. Ni Condester Sichalwe. Ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nianze kwa kuipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi na kuishukuru. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Momba, nashukuru sana kwa miradi yote ambayo tulipewa pesa ndani ya Jimbo la Momba. Yawezekana hatujafika pale mahali tunapotaka, lakini tunasema asiyeweza kushukuru kwa kidogo, hawezi kushukuru hata akipewa kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie fursa hii kuwashukuru Watanzania; pamoja na changamoto yote ya mfumuko wa bei tunayoipitia, wanaendelea kupambana kuhakikisha wanaijenga nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka leo hoja yangu niielekeze katika kuishauri Serikali na kuiomba. Nimesoma vizuri sana Taarifa ya Kamati ya Viwanda na Biashara, lakini kuna kipengele ambacho natamani kuona Serikali inawasaidia wananchi wa chini kabisa; mwanachi yule aliyeko kijijini ambaye hajui hata kusoma na kuandika, anaweza akatumia uwezo wake na maarifa yake ambayo Mwenyezi Mungu amemsadia katika kuzalisha viwanda vidogo vidogo na kufanya biashara ndogo ndogo ambazo zinawasadia kulea watoto wao na kuwasomesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapotupelekea Vituo vya Afya na Zahanati, wanafanya hizo biashara ndogo ili waweze kupata fedha ya kununua dawa kwenye vituo vyetu. Pamoja na kwamba Serikali imetoa elimu bila malipo, kuna kununua daftari, uniform za watoto na michango mingine elekezi ambayo imewekwa kwenye shule zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapotoa mchango huu, nataka nijielekeze kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano ambao unaanzia mwaka 2021/ 2022 mpaka 2025/2026 wenye dhima ya kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu. Tafsiri yake ni kwamba tunapotaka kujenga viwanda, vifanane na maendeleo ya watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuongelea Local Industry na Consumers Industry; na hapa nataka kuongelea pombe za kienyeji. Pombe za kienyeji kwenye makabila mbalimbali na mikoa mbalimbali; kila makabila wana pombe zao za kienyeji. Kuna pombe ya ulanzi inatengenezwa kule Iringa, kuna mbege kule Kilimanjaro, dengelua, ntulu kule Singida kwa kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, pombe ya mnazi kwenye mikoa huko ya Pwani; pia kuna kindi, kimpumu na pombe nyingine ambazo Serikali imezizuia, mfano gongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishauri Wizara ya Viwanda na Biashara, kwanza kabisa iiunde bodi kama ambavyo Wizara ya Kilimo imefanya, imeunda Bodi ya CPB ambayo inasimamia mazao ya nafaka na mazao yote mchanganyiko. Mfano sijui mpunga, mahindi, dengu na mazao yote. Wizara ya Kilimo imeunda bodi maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumwambia Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, pombe hizi ambazo naweza nikasema Serikali haijazipa kipaumbele na imezidharau, wakati mwingine wanasema mataputapu. Ukionekana wewe unakunywa kindi, kimpumu au gongo, hujielewi, huna akili kabisa. Ila ukionekana unakunywa bia ambazo watu wa TBL wanatengeneza, unaonekana ni wa kisasa. Hata ukienda kwenye Balozi zetu huko kuna ile inaitwa Cartas, wanawatengea kabisa fungu kununua zile pombe za bei ghali ya shilingi 300,000 , ya shilingi 400,000 , lakini zote ukizionja ladha yake haina tofauti na gongo. Tunajiuliza, swali ni kwamba, ni sababu hizi zina jina la Kizungu na gongo ina jina la Kibantu?
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, bodi hii itakapoundwa, inatasaidia kwenda kupima kiwango ambacho gongo inapotengenezwa. Je, mlishawahi kupima mkaona ni nini watu wa TBS wanaweza wakatusaidia kutoa makali ambayo yapo kwenye gongo yafanane na konyagi na pombe nyingine hizo ambazo mnaziona ni za kifahari ambazo matajiri wanakunywa, lakini wote wakinywa wanalewa?
Mheshimiwa Spika, nataka kusema kupitia Bunge hili Tukufu, pombe hizi za kienyeji ambazo tumezidharau, wapo wafanyabiashara wakubwa na mashuhuri ambao bibi zao, mama zao, shangazi zao, wamewasomesha kupitia hizi pombe za kienyeji. Wapo Wabunge humu ndani ya Bunge lako hili Tukufu ambao ni wasomi na ni maarufu na tunawajua na nianaamini hata kaka yangu Mwigulu huko kwao atakuwa amesomeshwa na pombe hizi za kienyeji.
Mheshimiwa Spika, pia huko nyuma mimi nilishawahi kusoma profile moja ya Kiongozi mkubwa sana hapa nchini ambaye alihojiwa na vyombo vya Kimataifa Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na yupo hapa kwenye Bunge hili Tukufu akasema kwamba amesomeshwa na bibi yake kwa kutumia pombe za kienyeji. Yupo mahali hapa, nione kama hawezi kuthibitisha.
Mheshimiwa Spika, swali langu kwa Watanzania na Wabunge mliyopo humu ndani, ni nani hapa aniambie hawezi kutamani mtoto wake asome awe Profesa kama Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo? Ni nani aniambie? (Makofi/Kicheko)
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Condester, taarifa.
T A A R I F A
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekaa na Askofu hapa; kwa hiyo, kidogo ni changamoto. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimpe taarifa mchangiaji kwamba kule kwetu Kijiji ninachotoka kinaitwa Mgela, pale tumejenga mpaka Kilabu cha Pombe na tumekijenga vizuri na ni source kubwa ya mapato. Kwa hiyo, ni mchango wake mzuri sana. Ni kweli mimi nimesoma kwa pombe, kwa hiyo, mchango wake ni mzuri sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Condester.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake. Yupo Mbunge mwingine hapa, mama yangu anaitwa Mheshimiwa Tendega, naye amesoma mpaka Chuo Kikuu kupata digrii yake kwa wazazi wake kupika pombe za kienyeji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa msingi kwa Serikali, miradi mikubwa yote kama SGR, sijui Bwawa la Mwalim Nyerere, tunaipenda sana. Ndani ya Jimbo langu tuna miradi mikubwa mitatu ambayo ina-worth mabilioni ya pesa, lakini miradi hii mpaka sasa hivi tunavyoongea ina zaidi ya miaka mitano haijatekelezeka. Swali la kujiuliza: Je, wananchi hawa tunapoendelea kusubiri hii miradi mikubwa itekelezeke hawaumwi? Hawasomeshi Watoto? Hawaishi? Wakiumwa wanatibiwa na nini? Wanafanya shughuli hizi hizi, pombe za kienyeji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipofanya ziara na Naibu Waziri wa Utawala ambao wanasimamia TASAF, iko chini yao, alipojaribu kuwatembelea wamama ndani ya Jimbo la Momba; wamama ambao wanafanya vizuri kwenye TASAF wakipewa pesa, ni wale ambao wanatengeneza pombe za kienyeji.
Sasa mimi najiuliza, sisi kila siku hatuwezi kuthamini vilivyo vyetu. Kama ambavyo wamechangia Wabunge wengine hapa, sisi kila kitu ni ku-import, kila kitu ni ku-import; jamani hata pombe tu, hatuwezi kuwasaidia hawa watu ambao wanatengeneza ulanzi kule Iringa wapate ithibati?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuipa ithibati kimpumu, kinde ambazo zinatengenezwa kule Momba? Hatuwezi kuwasaidia wamama na wabibi wa Kitanzania tupate wasomi wengi kama akina Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo? Mpaka sasa hizi tunaendelea kuongea suala la Liganga na Mchuchuma, tutasubiri miaka 50…
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: …lakini pombe hizi wananchi wanakula, wanaishi, wanavaa, wanasomesha watoto wao. Mimi nawajua vijana wengi wa Kitanzania wanaendesha V8 huko, mama zao wamewasomesha kwa kupitia pombe za kienyeji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema Waziri wa Viwanda na Biashara atakaposimama hapa, aseme kuhusiana na pombe za kienyeji siyo kushika tu shilingi yako, nitaikwapua shilingi yako. Nitataka aseme neno kuhusiana na pombe za kienyeji wanakujaje? (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Sichalwe, nilikuongezea dakika mbili.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia hizo dakika mbili. Nimefanya utafiti wangu kuonyesha kwamba kuna soko.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Muda wake umeisha Mheshimiwa Matiko.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Sichalwe, mwache akupe taarifa kwa ufupi.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitamalizia hoja yangu. Okay.
T A A R I F A
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Condester; mchango anaoutoa ni mzuri na valid kwa Watanzania wote. Kwa hiyo, napenda kumpa taarifa kwamba kuna kipindi Watanzania ambao wanazalisha mafuta kwa njia ambazo zilikuwa hazijarasimishwa, walikamatwa na Jeshi la Polisi na Waziri wa Kilimo akatoa tamko akasema Watanzania hao wasikamatwe, badala yake wasaidiwe ili waweze kujikwamua zaidi na kuweza kupimwa na kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mchango wake huu, ni kweli na dhahiri unasaidia Watanzania wengi. Hata wakitaka kuchukua takwimu hapa, ni zaidi ya asilimia
70. Basi Serikali ichukue hawa Watanzania wanaofanya biashara ya pombe zilizotajwa hapa, wasikamatwe na kupelekwa Magerezani, na badala yake wawezeshwe kuhakikisha kwamba inakuwa ni pombe ya kiwango na inangia kwenye market. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Condester.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa taarifa, nimepokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutaka kuonesha kuthibitisha, wenzetu nchi za jirani wana-support watu ambao wanatengeneza pombe za kawaida. Nimekuja na sample za pombe za bei rahisi kabisa hapa.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Waheshimiwa muda wake umemalizika, namwachia amalizie.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pombe kama hii inauzwa sijui shilingi 1,000 inatoka Malawi; pombe kama hii inauzwa sijui shilingi 8,000 inatoka Zambia…
(Hapa Mhe. Condester M. Sichalwe Alionesha chupa za pombe mbalimbali)
MBUNGE FULANI: Ni gongo hiyo!
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Zote hizi ni gongo, Shilingi 1,500 na zimeingia nchini kinyume na utaratibu. Hizi ni gongo zimepewa majina ya kizungu, owners kutoka Zambia; sijui lulars whisky kutoka Zambia; sijui Jambo gin, sijui K-Vant, sijui icelandan… (Makofi)