Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze nichangie kwenye Wizara ya Elimu. La kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri na inayoonesha mwelekeo mpya kwenye Wizara ya Elimu. Nina mambo matatu nataka kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza nataka kuchangia kuhusu Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978. Mheshimiwa Waziri katika mambo yako saba ambayo unataka kuyafanyia kazi kwenye Wizara ya Elimu, umeyaorodhesha kwamba mojawapo ni Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978. Ninakupongeza na ninaomba tu nikukumbushe jambo moja kwamba, mmesema mmekusanya karibu maoni 100,000 kama siyo 1,000,000; mfumo wetu wa elimu umekuwa ukichezewa sana. Katika mabadiliko ya sheria ambayo mnaenda kuyafanya, mojawapo ni kuhakikisha jinsi gani tunakwenda kuilinda elimu yetu isipate mawazo ya mtu binafsi yakaingizwa kwenye mfumo wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye nchi hii kuna mambo ambayo yametokea takribani matano kama siyo sita ambayo naweza kusema ni ya ovyo au siyo ya ovyo, lakini ni mambo ambayo yanaonesha ni jinsi gani elimu yetu inachezewa. Ukimsikiliza Nelson Mandela kwenye kitabu chake cha Long Way to Freedom anasema: “Education is a most powerful weapon which you can use to change the world.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye nchi yetu Mawaziri kadhaa wamepita na wamekuwa wakifanya maamuzi ya ajabu ajabu sana. Kuna Waziri siku moja aliamka akafuta UMISETA kwenye nchi hii, kwenye michezo; kuna Waziri siku nyingine akaamua kuchanganya Chemistry na Physics kuwa somo moja; kuna Waziri akaja akaondoa Division kwenye nchi hii akaweka GPA. Namshukuru Mheshimiwa Mama Ndalichako alikataa. Aliporudi kuwa Waziri, akairudisha Division. Siyo hayo tu, kuna mambo mengi sana ambayo Mawaziri mnaamua tu, leo hii elimu ya nchi ielekee huku, leo elimu ielekee huku mnavyotaka nyie.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba mlete sheria hapa Bungeni tuifanyie marekebisho, tuweke sheria jinsi ya kuilinda elimu yetu isichezewe. Kusiwe tu na kikundi cha mtu mmoja anaamua kubadilisha elimu yetu ifanye inavyotaka. Lazima ipate public opinion kuanzia Wabunge na hata wananchi ili tunapofanya mabadiliko yoyote, yawe ni mabadiliko yenye tija kwa Taifa letu. Siyo Waziri tu anaamka leo kutokana na utashi wa Profesa Mkenda, leo akiamua kufuta Form Three, anafuta. Hapana, lazima tuwe na namna ya kuilinda elimu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuchangia ni kwenye utitiri wa kozi kwenye vyuo vyetu. Mheshimiwa Waziri, ubora wa elimu yetu umeendelea kupungua kila siku. Ubora wa elimu yetu unapungua kutokana na kuondoka kwenye mlengo wa vyuo kadha wa kadha ambavyo Mwalimu Nyerere alivianzisha kwa makusudi. Kwa mfano, kuna chuo kama cha SUA (Sokoine University) kilianzishwa kwa ajili ya mambo ya Kilimo, lakini leo wanatoa education, tofauti kabisa na malengo ya chuo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Chuo cha Ardhi ambacho kilianzishwa kwa malengo ya vijana wetu kusoma kuhusu Ardhi, leo wanaotoa Accountants na Finance. Ukienda kwenye Chuo cha UDOM, wakati tuna MUHAS ambayo inahangaika na masuala ya udaktari wa mifupa na binadamu, leo UDOM wanatoa hiyo kozi pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo vipo tofauti tofauti ambavyo vimekuja kutuvuruga. Mzumbe kilianzishwa kwa ajili ya Sheria na Utawala, lakini leo nenda kuna kozi za Education na Tourism. Kwa nini wanafanya hivi? Wanafanya hivi ili wafanye enrollment ya wanafunzi wengi wapate fedha, kwa ajili ya kuendeshea vyuo vyao. Hili Taifa haijafikia uwezo huo wa kushindwa kupeleka fedha kwenye vyuo, hadi vyuo vinaenda kuingiza kozi ambazo ni nje ya mlengo wa chuo husika ili wapate fedha kwa sababu ya enrollment ya wanafunzi na pressure ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, hakuna relationship au mahusiano ya karibu kati ya Wizara ya Elimu, Wizara ya Utumishi na TCU. Nataka nikupe mfano Mheshimiwa Waziri; kwenye meza yako leo watu wa ADEM pale Bagamoyo, kile Chuo cha Bagamoyo ni kwa ajli ya Short Courses, leo hii TCU imewapitishia waanze kufundisha ADEM kwenye suala la Uongozi, wanasema Udhibiti wa Elimu, wakati kwenye Utumishi ukienda hakuna ajira inayohusisha Mambo ya Udhibiti wa Elimu. Wale wameanzisha kozi ambayo wao na TCU wameelewana lakini hakuna mawasiliano na Wizara ya Utumishi. Kwa hiyo, tunaenda kuzalisha watu ambao baadaye wanakwenda kukaa kwenye benchi, wanaanza kulalamika kuhusu ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, pitia vyuo vyote; kama SUA tulianzisha kwa ajili ya kilimo, angalia kozi zinazotolewa pale ziwe za Kilimo. Kama DUCE ilianzishwa kwa ajili ya Education, DUCE ina uwezo wa kuzalisha branch nyingine kwa ajili ya Education. Siyo kwenda ku-impose kwenye vyuo vingine. Leo tutashangaa IFM nao wanaanza kutoa Education. Itakuwa ni nchi hii Mheshimiwa Waziri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba na kumsihi sana Mheshimiwa Waziri, yeye ni academician, ni msomi, tunategemea sana kwamba ataenda kufanya reformation kwenye mfumo wetu wa elimu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Mama Ndalichako aliamua kufuta majoho, maana yake mliamua kuidhalilisha elimu yetu, hadi chekechea wakawa wanavaa majoho, na nyie mpo tu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Mama Ndalichako, leo hii angalau; kwa sababu ilikuwa mtu ukivaa joho lazima ulipambanie. Siyo tu mtu kutoka chekechea anavaa joho; ataona wapi umuhimu wa elimu? Ni kwa sababu nyie Mawaziri mnafanya business as usual, mmetulia, mmekaa, nawaomba mfanye reformation. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaenda sawa sawa na mlundikano wa vitabu kwenye mfumo wetu wa elimu. Leo hii Eng. Chiwelesa akiamua kuandika kitabu, anakiingiza kwenye mfumo wetu wa elimu na kinatumika. Hakina ithibati, hakina chochote, na ukienda kila darasa vitabu vipo vingi, havina utaratibu wowote ule, kiasi kwamba tumeanza kuwachanganya Watoto. Huyu definition ya geography ilisomwa hivi; huyu definition ya geography anaijua hivi; huyu definition ya biology anaijua hivi, huyu definition ya biology anaijua hivi. Tumeruhusu mlundikano wa vitabu kwenye mfumo wetu wa elimu, vitabu ambavyo havina ubora havina ithibati ya Serikali kwamba viweze kutumika kwenye mfumo wetu. Ninakutegemea sana kama yangu Mheshimiwa Mkenda, utatusaidia kubadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sheria iletwe hapa ili na wewe usifanye maamuzi unayojisikia kwanza leo unataka uibadilishe elimu yetu unavyotaka. Lete sheria tuweze kubadilisha ili sheria yetu tuweze kuiwekea ukingo, isianze kutumika ovyo ovyo. Tunaomba pia kwenye vyuo; vipitie vyote ujue vinavyofanya ndiyo yale malengo yaliyokusudiwa au ni pressure ya kupata fedha ili waweze kuendesha vyuo vyao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Nami niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hili alilolifanya leo. Hiki alichokifanya Mheshimiwa Rais kuweka fedha kwenye mafuta ndicho ambacho Watanzania wengi leo mioyo yao imetibiwa. Nampongeza sana Rais wangu kwa niaba ya wananchi wa Makete, tunampogneza Mheshimiwa Rais kwa niaba ya bodaboda, bajaji na wananchi wote wa Taifa hili kwa kusikiliza kilio cha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)