Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya jana na leo imesomwa hapa Bungeni. Ni kazi kubwa ambayo Watanzania wengi tulikuwa tunaisubiri na sasa amewaachia kazi Mawaziri mfanyie kazi. Watanzania hatutaki kusikia namba, kwamba tutawapa Bilioni 100 halafu Watanzania wasiosoma wenye elimu ya kawaida wanauliza hiyo ni bei gani imepungua kwa lita? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mpaka tarehe moja hiyo mliyotangaza mnatakiwa muwe mmeshatamka kwamba lita itauzwa bei gani ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ninakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa taarifa nzuri, umeongea vizuri, umeeleza vizuri, pamoja na Kamati pia. Mheshimiwa Waziri mimi nina machache sana kuhusiana na suala la elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kila biashara unayoifanya lazima iwe na tathmini. Naongea kitu ambacho pengine naweza kuwa tofauti kidogo na wenzangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la elimu bure, Mheshimiwa Waziri kuna kipindi sisi Wabunge unashindwa hata kwenda kutembelea Shule za Msingi huko Vijijini na shule zingine kwa sababu ukifika pale yaani ni kitu cha aibu sababu ni elimu bure. Unakuta darasa moja watoto wanasoma 500, Mwalimu mmoja anafundisha, sasa kwa hatua kama hii unakuta watoto wako Darasa la Tatu hajui hata kuandika jina na wewe bahati nzuri ni Profesa nataka uniambie kwenye majibu yako, hivi ungekuwa wewe una vipindi vitatu vya watoto 400 - 400 ungewezaje ku-concentrate kusahihisha halafu na kupanga masomo hata ya baadae. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, ni vizuri tukafanya tathmini kama tulikosea ni vizuri tukarekebisha. Huu mfumo tunaoenda nao elimu bure tunalundika tu pesa, watoto wanaenda mashuleni lakini hawapati elimu na Serikali inazidi kutumbukiza hela ambazo hazirudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakupa mfano mimi nina shule ina watoto 3,500 ina Walimu Tisa. Hebu jiulize ungekuwa ni wewe ungewezaje kufundisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba Mheshimiwa Waziri ukipata nafasi ya kuwa unazunguka huko Mikoani jaribu kufanya ziara za kushtukiza kwenye shule unaweza ukawa unaongea na Wabunge nataka kutembelea shule fulani ukafanya ziara ya kushtukiza usiende na ving’ora vya magari watajiandaa, ukakuta kile kipindi cha Saa Nne mtu anasahihisha hata haangalii daftari anatia tu hivi watoto wamepanga mstari watu Zaidi ya mia nne. Sasa tunatumbukiza hela kwenye sehemu ambayo kiukweli baadae mtakuja kutulaumu. Mnatengeneza bomu ambalo hatuna uwezo wa kuja kulikabili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumza kuhusu elimu ya juu. Serikali inatoa mikopo tumeambiwa hapa kwenye taarifa kwamba wameshapewa bilioni 400 sasa wameongezewa mpaka bilioni 500, lakini ningekuwa mimi ninayefanya biashara, hili suala nafikia mahali najiuliza, kama Serikali inatoa hizo hela na hatuna uwezo wa kuzikusanya, nimesikia mjumbe mmoja anasema tufungue benki yaani tuajiri wataalam wazidai kama benki, halafu mwisho wake itakuwaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina wazo, kwa kuwa Serikali ina watu wasomi na wabunifu na tuone namna ya kwamba watu wanapopewa mikopo na wanafanya research, mtu anaanza mwaka wa kwanza anafanya research mpaka mwisho wa elimu yake, ana-submit research yake, ana-graduate, kwa nini ile research isigeuke kuwa biashara? Kwa sababu research ile kwa kila mtu aliyefanya research yake hiyo tayari ni hela na wewe unaikubali unamfaulisha, unampa cheti. Sasa kuliko kumpa mtu hela halafu anamaliza degree yake umekopesha asilimia 50, hawajaajiriwa wote, wameajiriwa asilimia 15, halafu hizi hela zimepotea wengine wanakufa bila kurudisha deni, wengine wamekaa wamekuwa machinga hwajulikani waliko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningeomba tukubaliane na wenzetu wanaosimamia hii mikopo ya elimu ya juu kwamba tuwe na madirisha mawili tuwe na dirisha moja kwa ajili ya kukopesha ili mtu asome, lakini akifanya vizuri wewe ukitoa GPA, kile cheti chake kiwe bond kiwe dhamana kuwe na dirisha la kukopesha kulingana na research yako hata kama ni milioni tatu. Huwa najiuliza kweli ndugu zangu tunaweza tukawa tunaonekana kama tunaongea vitu vya ajabu, lakini naomba niulize swali la moja kwamba leo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaandaa utaratibu kwa machinga mtu ambaye hajulikani leo atakuwa hapa kesho atakuwa hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaandaa utaratibu tunatengeneza utaratibu waanze kukopeshwa na mabenki na tumesikia taarifa tayari wameanza kukopesha sijui Dar es Salaam na wapi, inakuweje machinga anakopeshwa kwa kitambulisho, wameshindwa kutengeneza utaratibu kwa mtu cheti cha degree akapata mkopo akaenda kuwa machinga ambaye amesoma na watu wangekuwa na nia hata ya kusoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo langu naomba Serikali ifikirie kuwa na madirisha hayo mawili; tukopeshe kwa ajili ya kusoma; halafu tukopeshe kwa ajili ya mitaji kwa ajili ya watu kwenda kujitegemea. Mimi binafsi ungeniuliza ningesema hata leo tuondoe hiyo elimu bure ya msingi, unamtengenezea msingi usiojitambua, akifika huko juu anakuwa machinga mzigo ambaye hajui kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nadhani tuwe tuna madirisha mawili kwenye Vyuo Vikuu, mtu anapomaliza Chuo Kikuu apate elimu ya mkopo na atumikie mkopo alipe na deni pamoja na ile aliyeikopea mwanzo. Faida ya pili, nimesikia Serikali baadhi ya mabenki yameanza kutoa mikopo kwenye elimu ya kati certificate na diploma, nikajaribu kujiuliza hiki ni kitu kizuri sana, lakini nikawa najaribu kuwauliza watu wa NMB hii inakuwaje, dhamana ni kitu gani kwa sababu certificate, hiki cheti hakikopesheki.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanakopesha kwa dhamana gani wanasema tumeanza na watoto wa wafanyakazi. Hii ni aibu kubwa sana yaani watoto wa maskini ambao wana akili nyingi wanashindwa kwenda kusoma kwa kukosa hela, tunaenda tena kuchukua mtoto wa mfanyakazi, tunamtengenezea utaratibu wa kukopa, kwa nini wasianze na watoto wa maskini na vyeti vyao viwakopeshe wao wenyewe. Kwa nini tukimbilie kukopesha watoto wa watu ambao wana uwezo wa kusomesha watoto wao, kwa hiyo nilikuwa naomba...

MHE. STANLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. STANLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba nimtaarifu mzungumzaji kwamba wanaokopeshwa sio watoto ni wazazi kwa sababu moja tu kwamba, mtoto aliye chini ya umri wa miaka kumi na nane wa mujibu wa sheria za nchi yetu hawezi kukopeshwa na benki na watoto wanaokwenda kusoma hivi vyuo vya kati ni wale waliomaliza kidato cha nne hawajaenda kidato cha tano wala cha sita. Kwa hiyo bado ni under 18 na ndio maana anaanza kukopeshwa mzazi kwanza.

NAIBU SPIKA: Mhesimiwa umeipokea taarifa?

MHE. DKT. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea. Nilichokuwa naongea mimi hana tatizo na mawazo yangu lakini ombi langu ni kwamba kwa nini tukaanze na watoto wa dizaini hiyo wa wafanyakazi hawa watoto wa maskini wenye akili wanaotaka kuendelea tuweke masharti nafuu kwenye benki zetu hizi, tuwakopesha hata wazazi maskini wenye watoto wao wako tayari kuweka bond hata mashamba, sio lazima tukaweke pesa ikubali isikubali benki kwamba tunaweza kuweka hata mashamba, au mbuzi au kondoo ili mtoto wangu asome na hiyo ndio kazi ya Serikali kusaidia watu wasiokuwa na uwezo, tunasaidiaje mtu ambaye ana uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hayo tu kwa leo nakushukuru. (Makofi)