Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami kuchangia mchango katika Wizara ya Elimu. Kwanza naipongeze Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri wanayoifanya, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri katika vitu ambavyo wanavifanya vikubwa ni kwenda kuangalia changamoto za elimu kwenye majimbo yetu. Tunawaalika, wanakubali kuja; unapiga simu, wanapokea nawaombeni sana mwendelee na kazi hiyo Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na mchango kuhusiana na mitaala ya elimu. Hii mitaala ya elimu inatakiwa iingie kwanza kwenye kumbukumbu wajue Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwamba leo Tanzania huu ni mtaala wa ngapi unabadilishwa? Mtaala wa kwanza katika nchi hii ulianzwa na Mjerumani mwaka 1905 hadi 1913; miaka minane Mjerumani alikuwa na mtaala wake katika nchi hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Mjerumani, mwaka 1913 mpaka 1967, miaka 54 tunatumia mtaala wa Mwingereza. Baada ya mwaka 67, Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alibadilisha mtaala wa kwanza, huu ukawa ni mtaala wa tatu katika nchi hii. Mtaala huu ulikwenda mpaka mwaka 1977, miaka 10. Ukafuata mtaala mwingine wa nne 1977 mpaka 1984. Baada ya mtaala wa mwaka 1984 ukaja mwingine mwaka 1984 hadi 1997 kwa Marehemu Mheshimiwa Mungai, ndio tukaanzia hapo sasa kuteleza mtelezo wa hatari huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mungai wakati anabadilisha mtaala mwaka 1997 alipiga marufuku michezo, mambo mengi yakafutwa, lakini wakaweka kitengo kinaitwa Book Management Unit. Hapo sasa elimu ya Tanzania ikaanza kuingizwa katika biashara. Kitengo hiki cha Book Management Unit kwenye mtaala huu wa mwaka 1997 yakaruhusiwa makampuni sasa kuanza kuuza vitabu. Yalitengenezwa makampuni mengi, watu wakawa wanachukua vitabu Nigeria na wapi, wanakuja kutafsiri kwa lugha ya Kiswahili, anapata ithibati inakwenda kwenye mashule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya moja kama yangu ya Sengerema, kuna shule zaidi ya 210. Kila shule inasoma kitabu chake, halafu mtihani ni mmoja unatoka katika Wizara. Kichekesho cha ajabu kabisa duniani! Kigoma wanasoma Mtue and company, sijui Ben and company, Tanzania Publishers, sijui wapi, sijui Kigamboni Publishers. Yaani kila mtu mwenye pesa zake alikuwa anakwenda ku-lob katika kitengo hicho cha Book Management Unit, wanapata order kwa Wakuu wa Shule vitabu vinasomwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili jambo, elimu yetu ndiyo ilianza kuharibikia hapo. Mtaala mwingine ukabadilishwa mwaka 2004. Baada ya 2004, mtaala mwingine, wa saba unakuja kubadilishwa. Huu mtaala umekuja mpaka 2014. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Profesa anatakiwa kukaa sasa afikiri, afanye research katika hii mitaala. Hawa waliosoma mtaala wa Mwingereza wana manufaa gani katika nchi hii? Sisi tuliosoma mtaala huu wa mwaka 1967 wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: Je, tunalinganishwa na hawa waliosoma mtaala wa mwaka 1997?
Mheshimiwa Naibu Spika, leo unaweza ukaacha chakula ndani; umeacha mahindi, umeacha mpunga, gesi ipo, watoto hawajui hata kusonga ugali? Sasa huyo unategemea aje akusaidiaje? Kwa sababu shuleni hilo jambo halifundishwi. Tulikuwa tuna elimu ya Sayansikimu sisi, tulifundishwa haya. Tulitoka shuleni tunapika keki, tunajua kila kitu, tunajua kuosha vyombo, kupiga pasi, tulifundishwa hizo kazi. Sasa leo inakuja mitaala hii ya kompyuta; haya endeleeni, lakini ninachotaka kukwambia, hiki kizazi chetu kikiisha, tegemeeni bomu linalokuja sasa, litataka ajira kwa sababu hamkuwaandaa katika jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine ambalo tunataka tuwasaidie hawa watu wa Wizara. Kwa kuwa ni wasikivu nina imani watasikia. Kuna suala la vyuo, wenzetu wa Thailand baada ya kumaliza machimbo, nchi hiyo waliichimba sana Thailand, wakabakiza sehemu moja angle ya utalii. Kule kwenye utalii wakaona na kwenyewe sasa kunakuwa na hali mbaya, waliwekeza katika vyuo vya ufundi vya kati. Hivi vyuo vya ufundi vya kati, walipeleka mtaala mmoja tu wakausimamia kwa nguvu kubwa ya ushonaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye kushona walipeleka watu kwenda kuwa ma-designer kule Hongkong, wakapeleka ma-designer kule China, walifundishwa kushona, wakawa wanaagiza vitambaa kutoka Pakistani, kutoka China. Leo Thailand, kila nyumba unayoiona Thailand ni kiwanda ndani. Leo order zote za nguo za watoto duniani, nguo zote nzuri zinatoka Thailand.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna soko hapa, tunazungukwa katika nchi za Afrika Mashariki, tunashindwaje sisi kushona? Tunashindwaje kupeleka kule kwenye vyuo vya ufundi? Ila kule kwenye vyuo vya ufundi, ada ni shilingi 60,000 day; na ukilala boarding ni shilingi 120,000. Hawa mkiwakopesha kama wanaokopeshwa wenye degree, wanaotoka kwenye elimu ya msingi, wanaotoka kwenye elimu ya sekondari wakafeli. Wakopesheni wakasome VETA.
Kwanza mkopo ni mdogo, anasoma miaka miwili shilingi 120,000, huyo analipa tu. Kule anafundishwa welding anafundishwa kutengeneza simu; ni kazi, leteni kozi za watu wanaokwenda kufanya, akitoka pale miezi sita anaweka meza anatengeneza simu. Atashindwaje kulipa deni la shilingi 60,000?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mnakuwa na mitaala ya ajabu kabisa. Yaani watu wanatoka kule hawawezi hata kukata kucha, unakaa unamwona mtu anapakwa na rangi. Yaani hata hawezi hata kupaka rangi kwenye miguu yake, anapakwa na mwanaume, anashikwa namna hii anapakwa rangi, hajui hata kupaka rangi. Mitaala gani katika nchi hii? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri katika jambo lingine kwa ndugu zetu wa Wizara ya Elimu. Elimu ya Sekondari; O’level na Advance pamoja na vyuo lazima mvichukue kutoka TAMISEMI. TAMISEMI ina mizigo mikubwa, mnakimbia jambo lenu. Kwa hiyo, ninyi sasa hivi Wizara ya Elimu mnatusaidia nini sisi watu wenye elimu huku chini?
Mheshimiwa Naibu Spik,a kwa sababu sasa hivi mmebakiza kukaa kwenye mitihani peke yake. Baraza la Mitihani ndiyo lenu. Sasa mtoto anatoka huku TAMISEMI, wana shule 14 za msingi bado mnataka kuwaongezea sekondari, zipo zaidi ya 5,000 halafu ninyi mnafanya kazi gani? Kwa nini mnamkimbia mtoto wenu? Chukueni elimu ya sekondari TAMISEMI, huku chini tuachieni elimu ya msingi na chekea. Sisi tuwaandalie na ninyi mwendelee na kazi, lakini habari ya kukimbia hiyo nafasi, siyo sawa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja nimalizie mchango wangu, nakuomba.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tabasam ahsante kwa mchango mzuri.
MHE. TABASAM J. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Naomba wachukue shule zao za sekondari; advance na O’level zichukueni Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)