Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hii Wizara nyeti, Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika nchi yetu. Pia nimpongeze sana Waziri wa Elimu pamoja na timu yake yote ya Wizara kwa kazi nzuri wanaoyofanya katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba, ukitaka kuwa na elimu bora lazima uangalie walimu bora. Usipo andaa walimu bora huwezi kuwa na elimu bora; na walimu bora hutokana na mafunzo bora wanayopata katika vyuo.

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu wetu kwa sasa ubora wao unapungua siku hadi siku. Nasema hivi kwa sababu gani; tunashukuru Wizara ya TAMISEMI imetoa ajira kwa walimu wapya, lakini walimu hawa wapo waliomaliza elimu yao au mafunzo ya ualimu kwa miaka mitano au saba. Walimu wale wamekaa nyumbani wakiwa wanafanya shughuli zingine za kiuchumi. Wapo wanaofanya shughuli za mama ntilie, wapo wanaofanya shughuli za bodaboda, wapo wanaofanya shughuli za kilimo na mifugo. Walimu hawa kwa miaka saba au kwa miaka mitano waliokaa nyumbani ni ukweli kwamba wameshasahau yale yote waliyofundishwa katika mafunzo yao ya ualimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi, ni wakati wa Serikali kuweka utaratibu, kwamba wanapoajiri walimu wapya wawapeleke kozi fupi fupi ili waweze kufanya kazi yao na kuleta tija. Lakini sambamba na hilo ni miaka mingi sasa walimu hawapati semina, ni miaka mingi walimu hawapati kozi fupifupi. Serikali iangalie namna gani ya kuwa- brush walimu ili waweze kuwaongezea maarifa na ujuzi katika kufanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu pia bado wanamazingira magumu ya kazi. Mazingira ya walimu yasipoboreshwa bado elimu yetu haitakuwa bora. Tunapoongelea elimu bora ni kumuongelea pia na mwalimu yule anayetoa hiyo elimu. Mazingira yao bado ni magumu ukizingatia na kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwalimu bado ana majukumu mazito sana. Mwalimu anaandaa lesson notes, lesson plan pamoja na scheme of work. Vilevile mwalimu anatakiwa asahihishe, na pia anatakiwa afundishe. Kazi zote hizi zinamtegemea mwalimu. Sasa, ukiangalia mazingira hayo inamuia vigumu kwa sababu uwiano kati ya mwalimu na mwanafunzi haupo. Mwalimu mmoja anakuwa na wanafunzi zaidi ya 200 au 100 darasani. Ukiangalia kazi ya namna hiyo ni ngumu sana mwalimu kufanya kazi yake ili kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Serikali basi iangalie mazingira ya ufanyaji kazi ya walimu ili walimu hawa waweze kufanya kazi. Vilevile kuangalia uwiano kati ya mwalimu na mwanafunzi. Tukifanya hivi tutaenda mbele kwenye hii sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo nizungumzie suala la motisha; walimu wanahitaji kupata motisha kwa sababu ni muda sasa walimu hawapati motisha. Wapo walimu wanaofanya vizuri, hivyo Serikali iangalie namna nzuri ya kuwapa motisha wale walimu ili waweze kufanya kazi yao kwa moyo. Katika suala zima la kufanya kazi motivation ni muhimu sana. Motivation moja wapo ni pamoja na kuwaongezea mishahara lakini na kupandisha madaraja. Niishukuru Serikali kwa mwaka huu na mwaka jana imepandisha madaraja. Hata hivyo bado tunahitaji kuwapa motisha walimu wale wanaofanya vizuri kwa kuwanafanya wanafunzi wetu wafaulu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine nishauri Serikali kuna TRC vituo vile vya mafunzo au vituo vya walimu wanaofanyia mafunzo, TRC ziboreshwe katika kila kanda, zikiboreshwa walimu watapata muda wa kwenda kujifunza baada ya masomo. Watajifunza, watabadilishana mawazo, walimu watakusanyika pale, watajadili mada zile ambazo zinawasumbua ili waweze kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nipongeze Serikali kwa kuanza mchakato wa mtaala mpya wa elimu. Tunapongelea mtaaala mpya wa elimu ni mtaala unaoenda kuendana na mahitaji ya jamii husika. Mtaala huu ulenge nini jamii inahitaji. Tunapozungumzia elimu bora ni lazima tuanze kuanzia chini. Tunapoanza kuboresha elimu ya vyuo tukasahau huku madarasa ya awali, shule za msingi na sekondari hakika hatutafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie namna ya kuboresha kuanzia darasa la awali, tunaboreshaje? Tunahitaji mwanafunzi anapomaliza au anapohitimu elimu yake aweze kujitegemea. Yale masomo ambayo yanatakiwa apewe ujuzi wa mwanafunzi kwenda kujitegemea akiwa uraiani yaanzie kuanzia darasa la awali ili kuendelea kuwajengea uwezo wanapoendelea kujifunza anapomaliza elimu yake ya msingi anakuwa tayari amepata ujuzi na maarifa; anapoenda chuoni anakuwa tayari anaujuzi na maarifa kuanzia kule chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumesahaulika kwa sababu kuna masomo ambayo walikuwa wanafanya wanafanya vizuri. Yapo masomo ambayo yalikuwa yanawashughulisha watoto wanafanya kazi za mikono, siku hizi hakuna. Turudishe yale masomo ambayo yanawafanya wanafunzi wanafanya shughuli za mikono ili kuweza kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima sasa tuanze reforms kuanzia chini kwenda juu. Tukifanya hivi ninaamini kwa kiasi kikubwa tutafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikisema haya naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)