Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, shule za vipaji maalumu ni shule ambazo ziliwekwa kwa ajili ya wanafunzi ambao wanafaulu kwa kiwango cha juu cha elimu. Lengo la kuweka shule hizi ni kuhakikisha wanafunzi ambao wapo katika shule hizi ambao tunasema wana akili yenye kiwango cha juu kidogo, wanafundishwa kwenye shule hizi ili kwa ajili ya kuimarisha ustawi wao. Lengo la shule hizi ni kuhakikisha tuna cream ya wanafunzi ambao wanaweza kuja kulisaidia Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sasa kwa trend ya shule za vipaji maalumu zilivyo nachelea kusema kwamba nina mashaka kama shule hizi bado zina- qualify kuwa shule za vipaji maalum kwa sababu hazizalishi matokeo. Shule za vipaji maalum zilipaswa kumsaidia mtoto na kumwendeleza kuanzia anavyoingia, anavyoendelea mpaka Vyuo Vikuu. Yaani tuwe tuna Database ya kumfuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mtoto leo hii ana uwezo mkubwa kwenye kutatua mathematic concept au ana uwezo mkubwa kwenye fizikia ama biolojia ama kemia, alipaswa kusaidia ili zile akili alizonazo kwenye masomo hayo zizae maarifa na kisha baadaye zisaidie kwenye tafiti au bunifu ambazo zitasaidia Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ilivyo kwa sasa hivi, wanafunzi hawa na akili zao nyingi kinachobakia ni kuwasifia kwamba wamepata A kwenye masomo. Yaani leo hii mwanafunzi mwenye akili tunamsifia amepata A, mwisho wa siku yupo mtaani anahangaika kutafuta ajira kama mwanafunzi mwingine aliyesoma kwenye shule za kawaida, wakati wanafunzi hawa walipaswa kusaidiwa kuwa lengo la kutatua changamoto za ajira katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwa sababu kama mtindo ndiyo huu, basi hizi shule za vipaji maalum hazina kazi yoyote. Kwa sababu mwisho wa siku mwanafunzi huyu hana tofauti na mwanafunzi aliyepo kwenye shule nyingine yoyote ya kawaida. Halafu bora wanafunzi wote kwenye shule hizi wangepata alama ya A; trend ya ufaulu kwenye shule za vipaji maalum imebadilika na ningependa nitoe mfano mchache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nitasema shule nne. Mwaka 2018 Kilakala O’ Level kitaifa ilishika nafasi ya 76, A‘ Level ikashika nafasi ya 14. Msalato ilishika O’ Level nafasi ya 102, hii ni shule ya vipaji maalum A’ Level ikaja kushika nafasi ya 17. Tabora Girls O’ Level mwaka 2018 ilishika nafasi ya 90 Kitaifa A’ Level ndiyo ikajitahidi ikaja kuwa nafasi ya 11. Tabora Boys ilikuwa nafasi ya 67 A’ Level ikaja kuwa nafasi ya 15. Mwaka jana, 2021 Kilakala O’ Level Kitaifa ilishika nafasi ya 30 na A‘ Level ikashika nafasi ya 56. Ilboru O’ Level nafasi ya 23, A’level nafasi ya 18.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu hata trend yao ya ufaulu, wanafaulisha zaidi advance kuliko O’ Level kwa sababu gani? Kwa sababu wanashindwa ku- groom watoto kuanzia huku walikotokea. Kwa hiyo, ikifika advance wanaletewa watoto ambao walikuwa groomed na wengine. Hii siyo trend sawa kwa shule za vipaji maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, walimu wanaofundisha kwenye shule hizi ni wa kawaida sasa kama tulikuwa tunahitaji wanafunzi wenye vipaji maalumu wanafundishwa vipi na walimu wa kawaida ilipaswa tuwe tuna mpango wa kuhakikisha walimu wanaofundisha kwenye shule hizi ni walimu wa kipekee ili kuendena na akili ya mwanafunzi. Ndiyo maana shule hizi O’ Level hazi-perform kwa sababu wanafundishwa na walimu ambao wao wamewazidi akili, sasa watafaulu vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shule za vipaji maalum lazima ziwe redefined, la sivyo, kama Taifa tutasota sana.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimpe taarifa mchangiaji kwamba hata walimu wanaowafundisha hawa watoto hawawafundishi kwa namna ya kipekee kwa sababu wanaamini wale watoto wana uwezo wa kipekee. Kwa hiyo, wanawacha wajisomee badala ya kuwekeza kwao kuhakikisha wanafanya vizuri.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kapinga, taarifa hiyo.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa lazima tujitafakari upya kuhakikisha kwamba wanafunzi wenye vipaji maalum wanawekewa mpango maalum ili wasaidie Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo Watanzania wengi wenye akili nyingi wamechukuliwa na wenzetu na wengine hata wanafanya kazi google huko Marekani, wanasaidiwa, wameendelezwa lakini hata sisi hatuna database ya kufuatilia. Kwa hiyo, kama Taifa tujifunze kutumia watu wetu na tuwekeze kwenye bajeti ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya elimu ina changamoto. Bajeti ya sekta ya elimu imegawanywagawanywa, ipo kwenye Wizara tofauti. Sasa Wizara ya Elimu wana bajeti yake, lakini bajeti kubwa ya Sekta ya Elimu ipo TAMISEMI. Kwa hiyo, hata kwenye ufuatiliaji wake wa masuala ya msingi yenye kuendeleza watoto kama hao wenye vipaji maalum inakuwa ni changamoto. Kwa hiyo, tuangalie bajeti ya Sekta ya Elimu iwe centralized ili tuweze kujua tuna-prioritize vipi mambo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa nizungumzie suala la pili kuhusiana na watoto ambao wapo kwenye shule za binafsi ambao wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu wazazi wao ama walezi wao hawawezi kuwalipia ada. Shule za Serikali ni za kila Mtanzania. Kila Mtanzania anapaswa kwenda kwenye shule ya Serikali bila kigezo ama bila kikwazo chochote kile. Nasi wenyewe tunasema kwamba kila mtoto wa kitanzania ana haki ya kupata elimu bila kikwazo cha namna yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanafunzi aliyekuwa kwenye shule binafsi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Kapinga kwa mchango mzuri. Ni kengele ya pili.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.(Makofi)