Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2012, Mheshimiwa Mnyika alisimama hapa Bungeni akasema tumefika hapa tulipo kwa sababu ya udhaifu wa Bunge. Akasema tumefika hapa tulipo kwa sababu ya udhaifu wa CCM na tumefika hapa tulipo kwa sababu ya udhaifu wa Rais
Kikwete, mlimzomea, mkachukua Polisi mkamtoa. Leo wale wateule wa JK toka Magufuli ameingia amewaporomosha zaidi ya 30. Leo mnapiga makofi mnasema majibu yanatumbuliwa lakini miaka mitano iliyopita tulizungumza mambo ya safari za JK, mlitetea humu ndani na mkapiga makofi. Miaka mitano iliyopita tulizungumza sherehe, kofia, miavuli isiyo na tija mlipiga makofi, leo wengine mnajitoa ufahamu mnasema majipu yanatumbuliwa.
(Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza hotuba ya Mheshimiwa Rais hii nchi ni ya wote. Mheshimiwa Rais tumempa kazi na Bunge hili lina wajibu wa kumsimamia, Tanzania ni yetu sote. Kwa hiyo, hatujaja hapa kumpambapamba, ana kazi anayotakiwa kuifanya kwa
Watanzania. Nikisema simuungi mkono katika mambo mengine anayofanya nitakuwa mwongo na nitakuwa mnafiki. Sisi kama Wabunge tunawajibu wa kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lililopita lilikubali kutokuwa na meno na Mnyika alisema mkamzomea akatoka nje, tunataka turudie makosa yale yale ya kuwa na Bunge butu.
Wananchi wametutuma tuisimamie Serikali pamoja na kumwambia ukweli Mheshimiwa Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Magufuli anasema anataka kubana matumizi, jambo ambalo ni zuri na Mbunge yeyote mwenye akili ataunga mkono. Hata hivyo, matumizi anayoyabana tumezungumza sana hapa, kuna idadi kubwa ya Wakuu wa Wilaya wanaendesha mashangingi hawana tija katika nchi hii akitaka kupunguza matumizi awatoe hao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unamkuta Mkuu wa Wilaya naye ana chumba cha mikutano, kikao kikubwa anachoweza kufanya ni cha kuwa na wale walinzi na kazi yao ni kudhibiti mikutano ya CHADEMA. Hiyo kazi anaweza akafanya OCD, hatuhitaji Mkuu wa Wilaya. Wala Mkuu wa Mkoa hatumhitaji, kama ni kupunguza matumizi tumtoe huko. Kazi za Wakuu wa Wilaya wameishia kuomba hela kwa Wakurugenzi, abishe mtu kama haombi hela kwa Wakurugenzi hapa. Haya ndiyo mambo tunatakiwa tujadili kama tunataka tuisaidie Serikali ipunguze matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia masuala ya utawala bora, Mheshimiwa Mbarawa, wewe ni Mzanzibar na wenzako ambao hamjaapishwa, mnaondoka Zanzibar mnakuja kutaka kupiga kura Dar es Salaam, kuna utawala bora hapo? Hayo ndiyo majibu
mnatakiwa mumwambie Magufuli ayatumbue na muanze kutumbuliwa wenyewe. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina kaka yangu Maige kutoka Iringa, mwanadiplomasia, ameshiriki kwenye vikao vingi vya kutatua migogoro duniani hapa na yeye anaondoka mwanadiplomasia, Waziri wa Nchi za Nje, hajaapishwa anaenda kutaka
kupiga kura Kinondoni, huo ndiyo utawala bora? (Makofi/Kicheko)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hypocrisy of the highest order. Kama Rais anataka utawala bora haya ndiyo mambo tunatakiwa tujadili ili Taifa tuliweke katika misingi bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kesho Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje kama ingemwagika damu Dar es Salaam angekwenda Rwanda kusuluhisha migogoro? Hebu tuwe wa kweli, tusijitoe ufahamu hapa. Hii nchi wote tunaipenda tuzungumze mambo ya msingi, hayo ndiyo mambo ya utawala bora?
Mheshimiwa Naibu Spika, jana Kilombero Mbunge mwenzetu anapigwa na kubebwa mzobemzobe na Polisi kwenye Jimbo lake mnakuja mnapiga vigelele hapa mnasema, utawala bora! Mbunge anazuiliwa kupiga kura kwenye Jimbo lake, haya ndiyo mambo tunayotakiwa
tuzungumze hapa lakini tunarudi kwenye mambo yale yale kwa akili ileile. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnasema utawala bora, rafiki yangu Kigwangalla anaondoka hata hafuati taratibu za Utumishi wa Umma unaenda kufungia watu kwenye ofisi. Najua nia nzuri ya Rais ya kutaka tulete mabadiliko lakini kama hatuja-change mindset za wafanyakazi wetu ni tatizo? Kama gari lako unaweza kuliendesha lina speed ya 120 hata unune, ukemee, haliwezi kwenda speed 200. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mmewajengea uwezo kiasi gani hawa watu? Human resources tuliyonayo ndiyo hii, hamjawajengea uwezo wa kufikiri vizuri, hamjawa-motivate, hamjawa-inspire, hamjajenga uwezo wa kwenda na kasi hii. Sasa hivi tunakwenda kwenye transformation hamjafanya hayo mambo kazi yenu ni kufukuzafukuza. Inawezekana nia ya Rais ni nzuri ya kutaka kuleta mabadiliko sasa wengine kwa sababu mmepewa vyeo siyo kwa merit mnataka muonekane eti mnafanya kazi, mnafungia watu milango, mnawafokea watu, anatoka hata Mkuu wa Mkoa anaenda kufokea watendaji wa mitaa ambao hawako chini yake wako chini ya Mkurugenzi, huo ni utawala gani bora wa sheria? Hebu tujihoji ndugu zangu.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumekuja hapa tunapoanza hebu tuache kujitoa ufahamu. Tena nashukuru sasa hivi wengi mmekuja mnaufahamu, tuisimamie Serikali kama kweli tunataka maendeleo katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, akina Wassira wameondoka walikuwa hivyo hivyo, akina Malima walikuwa hivyo hivyo walikuwa kimbelembele, hebu tuwe wakweli tusijitoe ufahamu hapa. Kiukweli watu mnajitoa ufahamu matokeo ya Zanzibar yanaeleweka kabisa tunaanza
kuongea ngonjera na mashairi, tunaacha kusimamia ukweli. Kama tunataka tumsimamie Rais majipu ndiyo hayo, tuanze na majipu hayo, tusimame kiukweli tuitetee Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unasema tunapunguza matumizi lakini matumizi yako pale pale. Wakuu wa Mkoa wana kazi gani? Mnasema msimamizi wa usalama kwani RPC hawezi kufanya? Ni kazi ipi ambayo hawezi kufanya RPC mpaka awepo Mkuu wa Mkoa, ndiyo kazi
kubwa wanayofanya. Hawa hawana kaz, kama kweli tunataka tupunguze matumizi ndiyo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hatutabadilika na hatutasimama kama Bunge ambalo wajibu wetu ni kuisimamia Serikali siyo kumpambapamba tu Magufuli na Serikali ya CCM, hizi ni kodi za wananchi na wananchi wametuleta hapa tuisimamie Serikali. Kwa hiyo, niombe tusijitoe ufahamu ndugu zangu. Tulizungumza haya mambo mkatuzomea, mkaimba ni walewale na Kinana aliwaambia muisimamie Serikali lakini leo Mbunge wa CCM unasimama hapa unaipamba, unajikombakomba kwa Rais baada ya dakika mbili barabara ni mbaya, maji
hayapo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninayezungumza pamoja na figisufigisu ambazo Chama cha Mapinduzi kilijaribu kuleta, nina barabara nzuri Iringa Mjini, nina maji asilimia 98, taa barabarani zinawaka, halafu wewe unakuja unajikombakomba hapa badala ya kuisimamia Serikali iwasaidie wananchi wako. Unajikomba kwa lipi, hiyo siyo kazi ya Kibunge! Wengine wamegeuka hapa wamekuwa Procurement Management Unit, siyo kazi yenu. Hata Halmashauri nimechukua pamoja na figisufigisu, nadhani Nape salamu anazipata hizi. Kwa
sababu nimefanya kazi ya kuwatumikia wananchi tuache unafiki, tuache kujikombakomba, tuisimamie Serikali.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naona naishiwa muda, Mungu akubariki sana. (Makofi/Kicheko)