Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye hii Wizara muhimu kabisa ya Maji.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, nimezisikiliza vizuri sana taarifa zote mbili. Nawapongeza sana Kamati ambayo imefanya kazi kubwa na taarifa yake iko wazi kabisa inajionesha. Vile vile nampongeza sana Waziri kwa taarifa yake ambayo hakika ametuonesha mwanga sisi Wabunge wenzake tunaowawakilisha Watanzania wengi wenye kiu ya kupata maji ya uhakika. Siku zote wanasema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Mheshimiwa Aweso nakupongeza sana ndugu yangu, wewe pamoja na timu yako nzima Naibu wako, Katibu Mkuu. Hata yale makofi wakati wa utambulisho yalikuwa yanaashiria kazi nzuri mnayoifanya hasa kwenye upande wa usikivu na kutekeleza majukumu yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais; kwenye sekta ya maji ama hakika amefanya kazi kubwa ambayo inaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natoka Kamati ya PIC. Tumekwenda kwenye Mikoa takribani mitatu kuangalia miradi ya maji ukiwemo Mkoa wa Arusha, Dar es Salaam, pamoja na Mwanza. Kazi ambayo inafanyika ni ya mabilioni ya fedha, lakini nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Wakurugenzi wa Mwanza (MWAWASA), Arusha (ARUWASA) pamoja na Dar es Salaam wa DAWASCO, wamefanya kazi nzuri sana ya usimamizi wa miradi mikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukizungumza Arusha, unazungumzia zaidi ya Shilingi bilioni 520; Mwanza zaidi ya Shilingi bilioni 69 mradi uko kazini, na Dar es Salaam vile vile.

Sasa nataka nizungumze mambo machache sana leo, lakini kubwa zaidi tuone namna gani tunavyoweza kuisaidia Wizara ya Maji katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa wanayoitaka wananchi wetu kule tunakotoka ni kuona maji yanapatikana; maji, maji, maji. Yako maeneo kama Mwanza, tuna mahitaji ya maji zaidi ya lita milioni 160 kwa siku. Uwezo wetu kwa sasa ni lita milioni 90 peke yake. Hata hivyo, namshukuru sana Waziri na Mheshimiwa Rais kwa sababu hivi ninavyozungumza tunao mradi wa zaidi ya Shilingi bilioni 69 ambao unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwaomba sana wananchi wenzangu wa Jimbo la Nyamagana waendelee kuwa watulivu kwa sababu mradi huu utakapokamilika, utatusaidia kuongeza zaidi ya lita milioni 48 na kufanya tuzalishe lita milioni 138 kwa siku na tutabaki na upungufu wa lita milioni 22 peke yake. Hii ina maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Wizara ya Maji kazi yake ni kuhakikisha fedha hizi zinapelekwa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Wizara ya Fedha kufanya kazi karibu sana na Wizara ya Maji, kwa sababu bila hivyo, leo inawezekana mkandarasi anataka fedha, lakini fedha kutoka Wizara ya Fedha; kuchukua fedha BoT na kuzifikisha kunakohusika, zinahitaji miezi miwili mpaka mitatu. Tunawakwamisha Watendaji wa Wizara ya Maji lakini tunakwamisha wananchi wetu kupata maji kwa wakati. Kwa hiyo, nawaomba Wizara ya Fedha tufanye kazi hii kwa muunganiko mkubwa ili kuweza kusaidia wananchi wetu walio wengi.

Mhshimiwa Spika, tumeona hapa bajeti imesomwa, Shilingi bilioni 657 fedha zinazokwenda kwenye miradi ya maendeleo. Nadhani Waheshimiwa Wabunge tunayo haja ya kutazama upya bajeti ya maendeleo ya maji. Fedha hizi ni kidogo sana ukilinganisha na mahitaji tuliyonayo kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikupe mfano, baada ya Mheshimiwa Rais kupata fedha za UVIKO na kuamua kuzielekeza kwenye miradi ya maji, fedha nyingine, mimi peke yake Nyamagana nimepata karibia Shilingi bilioni moja, Mamlaka ya Maji ya Mwanza. Hii Shilingi bilioni moja imegawanywa Kata ya Ilemela na Nyamagana, lakini wananchi ambao ninawawakilisha leo maeneo ya Buhongwa kule Mitaa ya Ihila wamepata maji kwa sababu ya fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kule Butimba, Kambarage wamepata maji kwa sababu ya fedha hizi; ukienda Nyamazobe, Nyegezi wamepata maji kwa sababu ya fedha hizi. Maana yangu ni nini? Kama fedha hizi za UVIKO zimekuja kutuongezea tija kwa kiwango hicho, ni vipi tukiwa na uhakika wa bajeti yetu kutoka angalau Shilingi milioni 657 tukaenda Shilingi milioni 800 mpaka Shilingi milioni 900 na ikiwezekana hata tupate Shilingi trilioni moja kwenye miradi ya maji. Kama hatutawasaidia Wizara ya Maji kuwa na uhakika wa fedha za kutosha, tutaendelea kuomba fedha nyingine kutoka maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ukiona hata miradi ninayoitaja leo ni fedha ambazo tunazipata kutoka kwa wadau. Tunayo miradi mikubwa ya Ziwa Victoria, tunategemea mradi wa Farkwa hapa, tumesikia hii EFDB wamepeleka fedha, lakini tunayo miradi mingine huko Dar- es-Salaam sijui Kidunda, Rufiji na kwingineko, hatuwezi kutekelea miradi hii kwa Shilingi Bilioni 657 peke yake. Maana yake ni nini? Turudi nyuma sasa, Mheshimiwa Rais ametembelea nchi nyingi, tumeona sasa hivi amekutana na wadau mbalimbali, anahamasisha watu kuja kuwekeza Tanzania na watu wamejitokeza, lakini kwa sababu watu wamejitokeza tutumie utaratibu ule ambao watu wengi wanakuja nao sasa hivi, watu wako tayari kuisaidia nchi na Wizara kupata fedha kwa ajili ya miradi ya maji. Tutumie utaratibu huo wa EPC ili kuhakikisha fedha hizi zinapokuja Wizara ya Maji inapokubaliana, Wizara ya Fedha iweke utaratibu mzuri watu hawa wapokelewe wakubaliane, waweke makubaliano sahihi na yenye tija kwa wananchi, fedha zipelekwe ili miradi hii tunayoizungumza mikubwa, huwezi kuhamisha maji kutoka Ziwa Victoria kuja Dodoma kwa kutegemea bajeti ya Wizara peke yake ya Bilioni 657, ni lazima sasa tufungue milango kwa sababu, Mheshimiwa Rais ameshatuonesha njia, ameshatufungulia njia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami nampongeza sana Mama huyu msikivu, Mama kipenzi huyu, Mama anayewapenda watu na amedhamiria kutusaidia hivi.

Mimi zamani nilikuwa simuelewi sana Mheshimiwa Aweso akisema wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani, nilikuwa najiuliza huu wali ukishauona unashibaje? Kumbe ukishauona wali kwenye sahani ndivyo appetite ya kula inavyozidi, ni sawa na wananchi wetu wanavyoona miradi mikubwa ya maji sasa hivi wanakuwa na matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Nyamagana kuna maeneo hawajawahi kufungua maji ya bomba, lakini leo kwa sababu kuna mradi wa Shilingi Bilioni 69 Butimba utakapokamilika mwakani mwezi wa Nne wananchi wangu wa kule Fumagila, mradi wa kule Rwanima, wa kule Nyamazobe, watakuwa na uhakika wa kuona maji ya bomba kwa mara ya kwanza. Kwa hiyo ni lazima tuwasaidie sana watu wa Wizara ya Maji. Mheshimiwa Aweso ni kijana kwa kweli anajitahidi sana, kwa umri wake na kazi anayoifanya anastahili pongezi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami nataka nikuhakikishie…

MHE. ERICK J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ERICK J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nataka kumpa tu taarifa mzungumzaji ya kwamba haya mambo yanayofanyika kwenye Jimbo la Nyamagana kule Buchosa kuna Bilioni 15 za mradi wa maji ambao unaendelea hivi sasa. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Stanslaus Mabula, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, naipokea Taarifa hii kwa mikono miwili. Na ninawaomba tu Waheshimiwa Wabunge…

SPIKA: Mheshimiwa una sekunde 30 malizia mchango wako.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, tumpe nguvu Mheshimiwa Aweso akafanye kazi hii kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ahsante. (Makofi)