Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye bajeti ya Wizara hii ya Maji na nipate kuleta salamu za wananchi wenzangu wa Muheza kwa Serikali yao. Nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali na uwezo wa kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu leo na niwashukuru sana wananchi wa Muheza kwa kuendelea kunipa ushirikiano, imani na kunitia moyo kijana wao niendelee kuwapambania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kututeulia na kuwaacha vijana wake aliowatuma kwenye Wizara hii ya Maji waendelee kufanya kazi aliyowatuma ya Watanzania.

Nitumie fursa hii kumpongeza nugu yangu, kaka yangu, rafiki yangu Mheshimiwa Al-habib Jumaa Hamidu Aweso, kidume kwelikweli kwa kazi kubwa anayoifanya. Pia nimpongeze Mheshimiwa Maryprisca Mahundi, Engineer, Naibu Waziri na Engineer Antony Sanga na Nadhifa Kemikimba na wasaidizi wao wote kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nina mambo mawili; jambo la kwanza ni kuhusiana na bilioni 6.05 ambazo Wilaya ya Muheza imezipata kwa miezi 18 hii ambayo mimi ni Mwakilishi wao. Bilioni 6.05 ni fedha nyingi na siwezi ku-capture zote kwa mnyumbulisho wake jinsi zinavyoenda kutumika, lakini nina matukio mawili - matatu ambayo nataka kuyataja.

Mheshimiwa Spika, kwanza tulipokea Milioni 300 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu kwenye Kata ya Tanganyika, Majengo ya Ndani na Masuguru ambazo zilienda kubadilisha mabomba kwa sababu, tulikuwa na mabomba ya chuma yaliyooza ambayo yalikuwa hayapitishi kabisa maji na hata yanapopitisha maji mengi yalikuwa yanamwagika njiani, hela hii ilienda kufanya kazi inayostahili.

Mheshimiwa Spika, pia tumepata Milioni 150 kuimarisha miundombinu kutoka NHC kwenda Mdote, Milioni 700 kwa mradi mpya wa Kata ya Kwemkabala ambayo ilikuwa haijawahi kuwa na mradi wowote. Tunatarajia kupokea milioni 370 kwa mradi wa Muheza Estate wakati wowote na tumepokea bilioni moja kwa ajili ya mradi wa majitaka na Mkandarasi yupo kazini. Miongoni mwa mambo anayofanya ni kutujengea sehemu ya kuhifadhia majitaka, pia kutununulia gari la majitaka na miradi mingine midogomidogo kama kuweka matundu nane ya vyoo kwenye Shule ya Sekondari ya Bonde, nane ya vyoo kwenye Shule ya Msingi niliyosoma mimi ya Mdote na matundu Sita kwenye Soko jipya la Michungwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile wiki iliyopita tu tumepokea milioni 408 kwa ajili ya miundombinu, Mabanda ya Papa kwenda Ngwaru. Milioni 91 Makete kwenda Masuguru, milioni 38 Swafaa kwenda KKKT, milioni 33 Majengo Ndani, maeneo ya Elephant milioni 40.7, Tanganyika Milioni 119, Majengo ya Nje ambapo panahitaji milioni 220 kwa sasa pamepata milioni 70 na ninategemea mtaenda kugonga mlango kwa mzee wa mnara, Engineer Antony Sanga na ataniongezea fedha hizi wakati wowote mradi huu uende kukamilika na hiyo ni kwa Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwa RUWASA tumepokea fedha PDR Milioni 735.3, Mfuko wa Maji Bilioni Moja na Mradi wa UVIKO Milioni 506 ambao umeenda kutekeleza mradi wa Mizembwe ambao kwa sasa umefikia asilimia 86 na tarehe 20 wananchi wataanza kupata maji. Wiki ijayo tunasaini pia mradi wa Mbomole Sakario ambao unagharimu milioni 664, Mradi wa Kwatango Milioni 591 na DDCA wanatuchimbia visima karibu 20 kwenye Kata za Kilulu, Mtimbilo, Mkuzi, Tingeni, Kwebada, Kwakifua, Kwafungo na Makole ambao wanaanza hivi karibuni. Kwemdimwa wameshakamilika na unatoa maji na Kilongo umefika asilimia 83 na mwezi ujao Vijiji Sita vitaanza kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimetaja yote haya siyo kwa sababu na ninajua nilikuwa na uchache wa muda kwa sababu sitaki kuwekwa kwenye kundi lile analolisema Mheshimiwa Waziri la mioyo isiyo na shukrani ambayo inafifisha yaliyo mema. Mimi nimeyasema haya ili Mheshimiwa Waziri ajue kwamba tunamshukuru, lakini tuna mapendekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Shilingi Bilioni 6.05 ni fedha nyingi. Ukiniuliza kama zimefika, zimefika. Ukiniuliza kama hali ya upatikanaji wa maji Wilayani Muheza imeimarika, nitakwambia imeimarika kutoka asilimia 50 kipindi cha masika mpaka asilimia 18 wakati wa kiangazi ilipokuwa mwaka 2020 mpaka sasa asilimia 65 kipindi cha masika mpaka asilimia 50 kipindi cha kiangazi kwa hiyo, tumepiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ukiniuliza kama nafikiri Bilioni Sita zimefanya kazi niliyokuwa naitarajia kichwani kwangu, nitakujibu hapana. Ningetegemea Bilioni Sita zitengeneze siyo tu kwa kuonekana kidogo tofauti ya ilivyokuwa 2020 na 2022, lakini zifanye upatikanaji wa maji Wilayani Muheza angalao ufike kile kiwango cha Kitaifa cha asilimia 74. Kwa hivyo, naamini Mheshimiwa Waziri atanisikia nikiomba kutoa mapendekezo ya kwamba, fedha hizi zinapopelekwa kwenye Wilaya basi ziangaliwe, zikaguliwe sawasawa ili kuhakikisha kazi zilizopangwa kufanyiwa zinafanyiwa kweli na hatuwi na miradi chefuchefu tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ninalotaka kulisema ni kuhusiana na mradi wa Miji 28. Kusema kweli, sijawahi kuongea na Mheshimiwa Waziri au Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na nikamaliza maongezi yangu, hata kama yalikuwa yanahusu kitu kingine nisiulizie mradi huu. Mradi huu uliwapa matumaini mengi akinamama wa Wilaya ya Muheza na Miji mingine 27 ambayo inakwenda kufaidikanao na umetumia muda mrefu sana, una miaka Nane sasa haujatekelezeka.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili nililotaka kulisema ni kuhusiana na mradi wa miji 28 kusema kweli sijawahi kuongea na Mheshimiwa Waziri au Katibu Mkuu wa Wizara ya maji na nikamaliza maongezi yangu hata kama yalikuwa yanahusu kitu kingine nisiulizie mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu uliwapa matumaini mengi akinamama wa Wilaya ya Muheza na miji mingine 27 ambayo inakwenda kufaidika nayo na umetumia muda mrefu sana una miaka nane sasa haujatekelezeka. Lakini taarifa ambazo nimezipata mpaka mwisho ambazo ni za kutia moyo kusema ukweli naamini kwamba mradi huu sasa unakwenda kutekelezeka na haubaki tena kwenye makaratasi. Nafahamu hili la signing ceremony lipo juu ya viwango vyetu vya mishahara wote siyo sisi kama Wabunge na nyinyi kama Wizara. Lakini Mheshimiwa Rais ratiba yake siyo rafiki sana na ana mambo mengi tunaomba kila nafasi mnayoipata kama ambavyo sisi wengine tulikuwa wasumbufu kwenu mkumbushe Mheshimiwa Rais mmuombe na mumuulizie kuhusiana na mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua kama kuna wakati akinamama wa nchi hii wanaamini kwamba matatizo yao ya maji yanakwenda kuisha, ni wakati huu ambapo nchi hii ina Rais mwanamama. Kwa hivyo nitumie fursa hii kuomba tena mkumbushe, mmuombe na mmuulize kwa unyenyekevu mkubwa Mheshimiwa Rais kuhakikisha sherehe hii inafanyika haraka na mradi unakwenda kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kauli mbili suala la upatikanaji wa maji halifai tena kuwa suala la kisiasa linafaa kuwa suala la kibinadamu watu wetu wengi wanafikiri mradi huu uko kwenye makaratasi na tunawaletea siasa tu kwenye masuala ya utekelezaji wa mradi huu, kwa sababu umechukua muda mrefu. Naomba kama kuna uwezekano masuala ya upatikanaji wa maji kuanzia sasa yawe ni masuala ya kibinadamu na kama linaweza kutusaidia huko mbele kwenye siasa zetu basi lifanye hivyo. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, najua umeshawasha mic nikushukuru naomba kuwasilisha naunga mkono hoja. (Makofi)