Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi naomba nichukue fursa hii kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu Samia kwa namna ambavyo ametoa fedha nyingi kama tulivyoomba kwenye bajeti iliyopita. Ninaamini kama wenzangu walivyosema sidhani kama wakati wowote imetokea kuomba fedha 100% na zikatoka 100% nampongeza sana.

Mheshimiwa Spika, pili, nachukua fursa hii kuwapongeza kwanza Waziri mwenyewe Mheshimiwa Jumaa Aweso, Naibu Waziri na pia nampongeza Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na wataalam wote. Ninafahamu kwamba kweli kwa sasa tunaona mwelekeo wa Wizara. Vile vile tunaona mwelekeo kwamba changamoto za maji zinapungua. Nami namwomba Mheshimiwa Rais awabakize bakize maana ukiwa na midfield wazuri ukaingiza mwingine unaweza ukapoteza, ili angalau baada ya miaka kadhaa tunaweza tukaona tumepata mwelekeo mzuri.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme machache kwanza, kuhusu jimboni kwangu. Ni ukweli usiopingika, nanyi wataalam mnajua kwamba Jimbo la Chemba pengine ndiyo lina upungufu zaidi wa maji. Pengine ni kwa sababu ya eneo lenyewe lilivyo, maana nafahamu kwamba mmekuwa mkifanya jitihada za kuja kuchimba visima lakini maji hayapatikani. Takwimu zinaonesha kwamba kwa sasa vijijini wanapata maji kwa asilimia 87, lakini kwangu ni asilimia 28.1 mpaka leo. Sasa unaweza ukaona kama hii takwimu ya asilimia 87 imeshushwa na asilimia 28.1 maana yake changamoto ni kubwa sana. Kwa nini? Kwa sababu wakichimba maji wanakosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri sana mwaka 2021 kwenye bajeti iliyopita mlikuja na jambo zuri sana kwamba sasa tunakwenda kuchimba mabwawa mawili ya kawaida pale Chemba. Namwomba sana Katibu Mkuu, kwa sababu fedha mmepewa asilimia 95 na sasa kuna fedha zinaendelea. Maana yake hizo fedha mlizopewa na za kwangu za yale mabwawa mawili zipo, lakini mpaka leo naona kuna shida kidogo, hatujayaona hayo mabwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini moja ya kunusuru hali iliyopo, ni hizi rasilimali tugawane sawa. Kuna jambo moja kidogo linaumiza kichwa. Unaona Wilaya fulani upatikanaji wa maji ni asilimia 90, lakini miradi mikubwa ndiyo inapelekwa huko. Nawaomba sana wataalam waliopo huko, ni vizuri sasa tukawekeza kwenye maeneo ambayo upatikanaji wa maji au asilimia ya maji ni chache, ili twende wote kwa pamoja. Naamini kwamba wana kikosi kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nawashukuru maana Mheshimiwa Waziri anasema, asiyeweza kumshukuru mwanadamu mwenzake, hata Mungu hawezi kumshukuru. Kwa hatua za makusudi mwaka 2021 mmenichimbia visima kama 15, lakini bahati nzuri nafikiri target ilikuwa ni kuchimba visima 18 lakini bahati mbaya maeneo mengi yakawa yanachimbwa, maji hayapatikani. Naamini asilimia zinazokuja sasa hivi, zitakuwa pengine zimepandisha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 28 point ngapi, angalau zifike 40.

Mheshimiwa Spika, kitu ambacho ninasisistiza; nasisitiza tena na tena, nawaomba yale mabwawa tuliyoandika kwenye bajeti ile angalau mkachimbe pale ili tuweze kuwa na uhakika wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi mnafahamu mwaka 2021 niliongea sana juu ya Bwawa la Farkwa. Kipekee kabisa naishukuru Serikali. Pia nakushukuru wewe Waziri mwenyewe, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Naibu Waziri, nimekuwa mara kadhaa nikikutana nao kokote; kwenye korido au sehemu yoyote na lazima niulize hili jambo limekaaje? Kwa hiyo, nawashukuru sana. Sasa kuna mwelekeo bwawa lile linaenda kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wasiwasi wangu mkubwa, andiko la mradi ule mimi nimepitia. Andiko lile linasema, tunaenda kujenga Bwawa la Farkwa kwa ajili ya kuleta maji Makao Makuu Dodoma. Nanyi mnafahamu kule Chemba maji ni changamoto, ukichimba hayapatikani.

Mheshimiwa Spika, nawaomba twende kuweka mradi ule lakini ni lazima maji yale yaanze kutumika Chemba kabla hamjaleta Makao Makuu. Haiwezekani sisi tuwe na ng’ombe tukamue maziwa, tuyalete Dodoma, ndiyo tufungiwe kwenye packet tuletewe Chemba. Haiwezekani. Nawaomba sana mwangalie adjustment ya aina yoyote, phase ya kwanza, sisi watu wenye mradi tupate maji halafu phase ya pili ndiyo tulete huku Makao Makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika, mimi nakaa Dodoma mara nyingi zaidi, angalau maji yanapatikana kidogo. Kule Chemba maji hakuna. Tuna vijiji 114. Vijiji ambavyo angalau maji yanapatikana kidogo ni vijiji 57. Vvijiji 57 vingine hakuna maji kabisa. Mnaweza mkaona hali ilivyo ngumu. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, nakuamini sana, naamini kikosi kilichopo, na naamini jambo hili linaweza kwenda kumalizika.

Mheshimiwa Spika, la pili, nawashukuru pia kwa mradi huu ambao ndugu yangu Mwana FA anaongelea. Mradi huu wa miji 28 tumeuongelea sana Bungeni na kwenye maeneo mengine. Nawashukuru sana kwa sababu mradi huu angalau pia unakwenda kupandisha takwimu za upatikanaji wa maji kwenye Wilaya yetu ya Chemba. Nami naomba kama walivyoomba wenzangu kwamba uwahishwe basi ili uanze mapema.

Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto nyingine ambayo naiona, ni kwamba ule mradi unaenda ku-cover maeneo ya mjini Chemba na pale mjini kidogo sasa hivi tuna mradi unaendelea. Sasa sijui ni nini. Nafikiri ni lazima tushauriane; yaani lazima niwepo pia kushauri wapi tunahitaji maji zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kushukuru, niwashukuru sana na Counsenuth, hawa wenye shirika hili kwa kweli wametusaidia sana na wana teknolojia ya kisasa. Nawashauri watu wa Wizara, hebu jaribuni kuongea na wale watu. Wale watu wakipima pale ambapo sisi tumekosa, wao wanapata. Wana mpango wa kuchimba visima tisa, lakini visima sita sasa hivi vina maji. Nao wanaenda sehemu ambayo sisi tumetoa shilingi 45,000,000 tukakosa maji, wao wakienda wanapata. Sasa hii challenge naomba niwaambie, hebu tuangalie, au kama ikiwezekana yule mtu ambaye anafanya geographical survey pale, mumtumie. Kwa sababu kuna hoja ambayo mimi siielewi sana. Nimewapeleka sehemu ambapo sisi tumechimba tukashindwa, wao wakichimba wanapata maji; na wananihakikishia kwamba hapa sisi tunapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa nafasi hii naomba niwashukuru sana Counsenuth, kwa hakika mnafanya kazi ya kitume, mmetusaidia sana watu wa Chemba na asiyeweza kumshukuru mwanadamu mwenzake, hawezi kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, naona unashika mic. Baada ya kusema haya, naambiwa muda wangu umekwisha, naomba kuunga hoja mkono.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)