Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nami nishukuru kwa kupata nafasi niweze kutoa mchango wangu. Awali ya yote nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana, nasi kama Wabunge tupo pamoja nao kuhakikisha kwamba tunatekeleza azma ya Mheshimiwa Rais katika kumaliza changamoto ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru kipekee sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ameendelea kuhakikisha kwamba Watanzania anawatua ndoo kichwani hususan wanawake wa Tanzania. Yapo mambo mengi yameelezwa ikiwepo miradi mbalimbali ambayo Mheshimiwa Rais ameendelea kuitekeleza ikiwa ni pamoja na mradi wa miji 28. Vile vile wanawake wa Mkoa wa Songwe wamenituma nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea mradi wa zaidi ya Shilingi bilioni 4.9 katika Wilaya ya Ileje. Ni imani yetu kwamba mradi huu utakapokamilika, utasaidia sana kutatua changamoto ya maji hasa katika Kata ya Itumba pamoja na Isongole ambazo zilikuwa na changamoto kubwa sana ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwa sababu tayari hizi fedha zipo kwenye bajeti, wananchi wa Ileje wana imani kubwa sana naye. Tunategemea kwamba fedha ambazo zimebaki, kwa sababu mpaka sasa hivi tumeshapata kama Shilingi bilioni moja, tuna imani kwamba hizo fedha zitaletwa kwa wakati ili kuweza kuwapunguzia adha ya maji wananchi ya Jimbo la Ileje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba nijikite kwenye kueleza hali ya upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Songwe. Katika Mkoa wetu wa Songwe, Mkoa ambao ni mpya tuna changamoto kubwa sana ya maji.
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu ameshafika siyo mara moja, siyo mara mbili kwenye Mkoa wetu wa Songwe. Kwa hiyo, ninavyozungumza changamoto hizi, Mheshimiwa Waziri anazifahamu. Zipo ambazo amezifanyia kazi nasi tunamshukuru sana na tunampongeza. Hata hivyo bado changamoto ya maji kwenye Mkoa wetu wa Songwe ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye takwimu, zinasema kwamba upatikanaji wa maji kwa vijijini ndani ya Mkoa wa Songwe ni asilimia 73 lakini kiuhalisia ukienda kule site hizo asilimia 73 hazionekani, zinaonekana tu kwenye makaratasi kama ambavyo Kamati imesema kwamba kuna shida kwenye hizi takwimu za maji, uhalisia wake hau-reflect hali halisi ya upatikanaji wa maji katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati akielezea bajeti yake. Ameeleza mambo mengi na ya msingi sana, lakini upo mradi wa miji 28 ambao Mheshimiwa Waziri ameutaja, lakini kwenye Mkoa wetu wa Songwe tunayo miji mikubwa mitatu; kwa maana ya Mji wa Mloo, Mji wa Vuawa pamoja na Mji wa Tunduma. Miji hii ina changamoto kubwa sana ya maji na Mheshimiwa Waziri analifahamu hilo, ameshakuja kama ambavyo nimesema awali. Unapozungumzia suala la maji, moja kwa moja unamgusa mwanamke. Wanawake wenzangu wa Mkoa wa Songwe wa Miji hii mitatu wanapata shida sana ya maji. Kwa hiyo, mimi kama Mbunge wa wanawake Mkoa wa Songwe ni jukumu langu kuweza kuwasemea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri wakati akiwasilisha, nikawa nina shauku sana kuweza kusikia, huenda mji mmoja kati ya hii mitatu itasikika kwenye hii miji 28. Kwa kweli sisi wananchi wa Mkoa wa Songwe nionyeshe masikitiko yetu makubwa kwa sababu hata mji mmoja haujaingizwa katika hii miji 28. Wabunge wenzangu wamesimama wameishukuru Serikali kwa sababu wamepata angalau mji mmoja au miji miwili, lakini Mkoa wa Songwe ambako changamoto ya maji ni kubwa; kuna Mji wa Tunduma una wakazi zaidi ya 200,000 lakini hakuna maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi kama Wabunge wa Mkoa wa Songwe tulitegemea kabisa kwamba angalau na sisi tutapata mji mmoja. Hii ndiyo maana imekuwa ni changamoto hata kwenye masuala ya ajira. Wabunge imefika mahali tukashauri kwamba ikiwezekana hizi ajira basi zitolewe kule kwenye ngazi za Majimbo yetu ili kuwe na mgawanyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesoma hii bajeti, Mikoa yote ambayo inazunguka Mkoa wa Songwe, kwa maana ya Mkoa wa Mbeya, wamepata miji miwili; Iringa miji miwili; Mkoa mpya wa Njombe ambao ni mpya kama Mkoa wa Songwe wamepata miji miwili; Katavi mji mmoja; lakini Songwe hata mji mmoja hatujapata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nioneshe masikitiko yangu makubwa na niseme kwamba Mheshimiwa Aweso tunatambua sana kazi kubwa unayoifanya lakini kwa hili sisi wananchi wa Mkoa wa Songwe tumesikitika mpaka tukahisi labda inawezekana Mheshimiwa Aweso ulidhani kwamba Songwe labda ipo Zambia. Sisi hatupo Zambia Mheshimiwa Aweso, tupo Tanzania hii hii. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe ushauri wangu kwa Serikali. Kwa sababu tumeshakosa kwenye hii miji 28, na changamoto katika miji hii ni kubwa sana, tunao mradi wetu mkubwa sana wa kutoa maji Ileje kuyapeleka Tunduma pamoja na Mji wa Vuawa; mradi huu ni mkubwa sana na kwa bahati mbaya sana Marais wote kuanzia Mkapa, amekuja Rais Kikwete, Rais Magufuli wameendelea kuahidi mradi huu lakini mpaka sasa haujatekelezwa; kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa sababu sasa hivi ameshatutafutia mfadhili, Mjerumani kwa ajili ya kuja kukamilisha mradi huu wa maji kutoa maji Ileje kuyasambaza Mji wa Tunduma pamoja na Mji wa Vuawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanawake tuna imani kubwa sana na Rais wetu, na kwa sababu mfadhili wa kufadhili huu mradi ameshapatikana, naomba sasa Wizara iweze kusimamia jambo hili likamilike. Kwa sababu kumekuwa kuna kusuasua sana, imechukua muda mrefu. Ukifuatilia, mara wakwambie sijui upembuzi, mara sijui nini, yaani story zimekuwa nyingi.
Sisi wananchi wa Tunduma tumechoka kusubiria huu mradi. Tunataka kuona utekelezaji wake kama ambavyo Mheshimiwa Rais ametafuta fedha, ametafuta mfadhili, na mfadhili amepatikana. Mheshimiwa Aweso na sisi tuna imani kubwa sana na wewe kwamba mradi huu utaanza kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba mtukamilishie huu mradi na tunaamini kwamba ndiyo mradi pekee mkubwa kwenye Mkoa wetu wa Songwe ambao kwa kiasi kikubwa sana utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye Mji wa Tunduma pamoja na Mji wa Vwawa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba pia nijikite kwenye kuzungumzia hoja yangu ya pili. Nimesikiliza sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nilikuwa nataka sana kusikiliza kuhusiana na suala la upotevu wa maji ambao bado ni changamoto kubwa sana kwenye nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya upotevu wa maji...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Sekunde 30, kengele imegonga hapa.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, changamoto ya upotevu wa maji ni kubwa sana. Nilikuwa na takwimu za kuweza kuzitaja, lakini kwa sababu muda umekwisha, naomba sasa Wizara, inafanya kazi kubwa sana kwenye kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maji, naomba nguvu hiyo hiyo pia ielekezwe kwenye kuhakikisha kwamba tunadhibiti upotevu mkubwa wa maji. Ahsante sana. (Makofi)