Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi hii ili na mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia kwenye hotuba hii muhimu ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Wabunge wenzangu ambao wamempongeza kwa dhati Waziri wetu wa Maji, Mheshimiwa Naibu Waziri lakini na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya ambayo matokeo yake chanja yanaonekana katika maeneo yetu kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba bado kuna maeneo mengi katika Jimbo langu la Bukene ambayo bado yana changamoto ya upatikanaji wa maji lakini jitihada za dhati za kuhakikisha tatizo la maji linapatiwa ufumbuzi zinaonekana na nichukue fursa hii kumpongeza sana Waziri wa Maji, kwa kweli katika eneo ambalo kasi ya kutatua changamoto inaonekana kwa macho ni eneo la miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka uliopita nitataja tu baadhi katika Jimbo langu la Bukene, tumepatiwa Milioni 177 kukamilisha mradi wa maji wa Mwamala, pia tumepatiwa Milioni 264 kukamilisha mradi wa maji wa Kayombo mradi umekamilika na wananchi wanakunywa maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepatiwa Milioni 296 kukamilisha mradi wa maji wa Kijiji cha Mogwa mradi umekamilika wananchi wanatumia maji safi na salama. Tumepatiwa pia Milioni 331 kukamilisha mradi wa maji kwenye kijiji cha Lakuhi mradi umekamilika wananchi wanakunywa maji na maji kutoka kwenye kijiji hiki tumeyapeleka mpaka kijiji cha Itobo center kwa sababu maji haya ni ya baridi, pale Itobo walikuwa na maji lakini yalikuwa yalikuwa ya chumvi, kwa hiyo, sasa wananchi wa Lakuhi pamoja na wananchi wa Itobo center wananufaika na maji safi baridi kutoka katika Kijiji cha Lakuhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi bado Wizara ilitupa Shilingi Milioni 360 kukamilisha mradi wa maji kwenye kijiji cha Kabanga, mradi unaendelea vizuri na sasa hivi umefikia karibu asilimia 85. Kama hiyo haitoshi bado tumepata Milioni 504 kwa ajili ya miradi ya vijiji viwili kwa mpigo kijiji cha Mambali na kijiji cha Kikonoka. Mradi huu unaanza utekelezaji wake fedha ipo kwa hiyo utakamilika na wananchi watapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado katika Jimbo langu tumepatiwa Milioni 450 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji wa kijiji cha Sigili na Iboja na kazi inakwenda vizuri, zaidi ya asilimia 80 kazi imekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa na kwa namna ya kipekee nimshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Maji kwa ujumla kwa kukubali kilio chetu cha miaka kadhaa sasa cha kuyatoa maji ya Ziwa Victoria kutoka Nzega Mjini kuyafikisha katika Jimbo langu la Bukene ambako hapo njiani maji yatakapopita zaidi ya vijiji Ishirini na Vitongoji mia moja vinakwenda kunufaika na maji haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa Ziwa Victoria ulikuwa unayatoa maji Ziwa Victoria kupitia Nzega kuyafikisha Tabora Mjini, sasa ukiyafikisha Nzega pale mimi Jimbo langu ni kilometa 40 ndani sasa tangu yafike Nzega tumekuwa tukipambana tunajenga hoja kwamba maji yatoke Nzega Mjini sasa yafike kilometa 40 mpaka Bukene, sasa kilio hicho siyo hadithi tena wala siyo porojo ni kwamba jambo limetimia na Mkandarasi PNR ameshasainishwa mkataba wa Bilioni Tatu na Milioni Mia Saba kwa ajili ya kuyatoa maji Nzega Mjini na kuyafikisha umbali wa kilometa 40 katikati ya Jimbo langu la Bukene. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora Waziri anajua na Watendaji wa Wizara wanajua, Mkoa wa Tabora unashida sana ya upatikanaji wa maji chini ya ardhi miamba ya Mkoa wa Tabora kuna wakati tulikuwa tunachimba visima 20 kati ya hivyo 20 ni viwili tu ndiyo vinapatikana na maji au wakati mwingine mnachimba mnapoteza hela nyingi hata kisima kimoja hakina maji. Kwa hiyo, Mkoa wa Tabora huwezi kuyategemea maji kwa chini ya ardhi kuna shida kubwa. Kwa hiyo, suluhisho la kudumu na pekee kwa Mkoa wa Tabora ni kufanya usambazaji wa maji ya Ziwa Victoria ambayo sasa yamefika pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ushauri wangu kwa wizara ni kwamba sehemu kubwa ya nguvu za kutatua tatizo la maji la Mkoa wa Tabora ni usambazaji wa maji ya Ziwa Victoria ambayo sasa yameshafika pale Makao Makuu ya Mkoa. Kwa hiyo, nguvu kubwa wala isielekezwe katika kutafuta maji chini ya ardhi kwa sababu imeshakuwa proven bila shaka yoyote kwamba miamba ya Mkoa wa Tabora inashida sana ya kupatikana maji chini ya ardhi. Kwa hiyo, nguvu kubwa ielekezwe katika usambazaji wa maji ya kutoka Ziwa Victoria. Ninajua Urambo wanasubiri, najua Sikonge wanasubiri, Ulyankhulu wanasubiri kila mahali wanasubiri. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba usambazaji wa Maji ya Ziwa Victoria ndiyo suluhisho la maji katika Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni mwaka jana Wizara ya Maji iliendesha program ambayo inaitwa program for the result (P4R) ambapo Mikoa 17 yenye jumla ya Wilaya 86 ilishirikishwa kwa vigezo mbalimbali kulikuwa na kigezo cha wingi wa watu waliounganishwa kupata huduma ya maji, kulikuwa na kigezo cha uendeshaji mzuri wa Jumuiya za Utumiaji Maji, na ninashukuru kwamba katika Halmashauri zote 86, Wilaya 86 na Mikoa 17 Wilaya yangu ya Nzega ndiyo iliibuka mshindi wa kwanza. Kutokana na hilo Wizara ya Maji imetupatia Shilingi Bilioni 10.2 baada ya kushinda hiyo program ya P4R. Kwa hiyo, tunaomba fedha hizo kwa sababu mkataba ni kwamba zitapatikana mwaka huu wa fedha zije tumejipanga kuzitumia katika kuimarisha upatikanaji wa maji lakini kuimarisha jumuiya za utumiaji wa maji kuhakikisha zote zinaajiri Wahandisi, zinaajiri Wahasibu, zinakuwa na wasimamizi na wananchi wanapata elimu ya utumiaji wa maji.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwa dhati kabisa nitumie fursa hii nimpongeze Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Nzega Bwana Gaston Ntulo kwa usimamizi mzuri sana akisaidiwa na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tabora, kwa kweli wapo karibu sana kuisimamia miradi kuifuatilia na kuhamasisha usimamizi mzuri wa miradi ya maji na kuhakikisha kwamba huduma hii inapatikana vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hii Bilioni 10 ambayo tumepata baada ya kuwa washindi wa kwanza ndiyo imetuwezesha kutenga Bilioni Nne ambazo sasa ndiyo zinayatoa maji Nzega Mjini kuyafikisha Bukene ambapo vijiji vya Shigamba, Kagongwa, Itobo, Lakuhi, Chamwabo, Udutu, Lububu, Kasela, Nindo, Senge, Mwamala, Seki, Chamiwa na Kishili, Kabanga, Uduko, Uswongahala na Bukene vinakwenda kunufainika na maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nimalizie tena kumpongeza sana Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kweli suala la maji amelivalia njuga lakini Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Viongozi wote wa Wizara ya Maji wanatekeleza majukumu yao kwa weledi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja asilimia 100. Nashukuru sana.(Makofi)