Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi pia niweze kuchangia kwenye Bajeti hii ya Wizara ya Maji. Kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mradi wa UVIKO ambao tuliupata Biharamulo Mjini. Mradi unaendelea vizuri tumetandaza mabomba pale kwa takribani kilomita 20 na tunajenga tenki kubwa tu kwa ajili ya kutusaidia pale Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, pale ambapo mtu anastahili heshima na anastahili pongezi ni lazima tumpe. Mheshimiwa Waziri wakati unasoma Bajeti yako hapa, nadhani Wabunge wengi walikuwa in vibrant mood wamepiga makofi, wakashangilia, wakakushukuru lakini wanakushukuru kwa sababu ya mahusiano uliyonayo na Wabunge humu ndani. Yawezekana wanashida ya maji kwao, yawezekana wana matatizo mengine lakini matumaini wanayo kwa sababu life style yako humu ndani inakuunganisha na Wabunge karibu wote. Kwa hiyo, hilo tunaomba tukushukuru, maana kila tunapokufuata mtu unamwambia twende DUWASA. Saa nne kamili uko pale. Muda mwingi tunakuta foleni lakini mara nyingi unahudumia Wabunge. Kwa hiyo, bwana kwenye hilo naomba nikupongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si wewe tu pamoja na msaidizi wako Mheshimiwa Injinia Maryprisca nakupongeza pia. Ulinitembelea Biharamulo, tukaenda Mubaba, tukaenda Kabindi maji sasa hivi maeneo yale tuliyotembelea mambo yanaenda vizuri. Lakini siwezi kuwapongeza ninyi wawili bila kujua kwamba kuna Watendaji nyuma yenu. Mhandisi Anthony Sanga, tumpongeze pia lakini pia na Nadhifa Kemikimba Injinia naye anastahili pongezi kwa sababu wamefanya kazi kubwa. Wote tunajua tulichonacho ndio hichi tunagawana kidogo kidogo lakini wanafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi upande wa RUWASA kwa kweli siwezi kumsahau Injinia Kivegaro kwa kazi kubwa ambayo ameifanya yeye na Taasisi yake ya RUWASA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nachangia kwenye Bajeti iliyopita nilisoma kwa uzoefu wangu, bahati nzuri nimekuwa karibu sana na hii Wizara kabla ya kuingia humu Bungeni. Kero kubwa ilikuwa ni miradi ambayo ilikuwa imekwama kwa muda mrefu. Tumesikia wote Bajeti iliyopita na Bajeti hii pia. Kitendo cha kukwamua kutoka miradi 177 kichefuchefu na leo imebaki 57 tunaamini tunakoelekea ni kuzuri zaidi kuliko kule ambako tulikuwa tumekwama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati wa uchangiaji mwaka jana nilieleza kitu kimoja ambacho kilikuwa ni concern yangu. Kama Mhandisi kilio changu kikubwa ni kuhakikisha kwamba tunatengeneza fursa kwa ajili ya watu wetu hasa ambao ninajua kwamba wamesoma course kama za kwetu hizi waweze kupata nafasi ya kufanya kazi na hatimaye watengeneze kipato kwa familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kilichopita miradi mingi tulikuwa tunafanya kwa Force Account ikafikia stage watu wamesoma course zetu hizi walifungua kampuni zao lakini hawakuwa na ajira. Bajeti iliyopita mmerudisha wakandarasi kufanya miradi ya maji. Kwa hiyo, kwenye hilo naomba niwapongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kulikuwa na issue ya vifaa vinavyotumika kwenye miradi ya maji. Tumeona miradi mingi sasa hivi inayosimamiwa na Wizara ya Maji. Miradi ya RUWASA na hata miradi ya UVIKO ambayo imetokea pale material mengi yaliyotumika kwenye kufanya hizi kazi ni material yanayozalishwa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kitendo cha miradi ya maji kutumia mabomba na kutumia viungio na vitu vingine ambavyo vinatoka ndani ya nchi hapa ni fursa kwa wawekezaji wa ndani lakini vilevile ni fursa kwa vijana wa kitanzania ambao wameajiriwa kwenye haya makampuni. Kwa hiyo, kwa sehemu kubwa mmetubeba na mmesaidia ile adhma na hali ya kutengeneza ajira kwa ajili ya vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu kizuri ambacho nimefurahia napenda nikipongeze kabla ya kurejea kwenye miradi sasa ambayo inaelekea Jimboni kwangu. Mheshimiwa Waziri kama Mhandisi kuna kitu nilikuwa najiuliza, mnajenga Kituo cha Afya cha shilingi milioni 550 au milioni 500 kinakuwa na watu wa kukisimamia pale kila kitu. Ila unapeleka mradi wa maji wa milioni 700 unawaachia wanakijiji tu pale hawana Technician hawana nini. Kwa hiyo, hii ambayo mmekuja nayo sasa ya kuweka Technicians na Wahasibu maana yake hata Vyuo vyetu vya VETA ambavyo tunajenga kila sehemu wale vijana wanaenda kupata ajira za kuwa wasimamizi. Wengine wanaotoka kwenye Chuo chetu cha Maji wanaenda kusimamia pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwangu naona mmetu-boost lakini vilevile ile miradi itadumu kwa sababu ina watu wataalam ambao wanaelewa nini maana ya mradi wa maji. Kwa hiyo, nawapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa nikirejea kwenye miradi ambayo inaendelea Jimboni kwangu, Mheshimiwa Waziri kwanza naomba nikupongeze. Ninalo eneo moja linaitwa Nyakanazi. Nyakanazi ni Mji unaopanuka sana na ni Mji mkubwa sana pale Biharamulo ni center kubwa kwa kweli kwenye Wilaya yetu ya Biharamulo. Kitendo cha kupata sasa kwamba signing ya Mkandarasi ambaye anaenda kutekeleza mradi mkubwa wa maji Nyakanazi nimeambiwa muda wowote watasaini Mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwangu nishukuru kwa sababu ilikuwa ni kilio cha wanabiharamulo na hawa watu wa Nyakanazi wapate maji waweze kufungua pale fursa za kiuchumi na shughuli nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru kwa miradi inayoendelea kwenye Kata ya Nyabusosi eneo la Mbindi, Nyamigele, Mavota tunajenga tenki pale lakini Mheshimiwa Waziri alikuja pale maeneo ya Mubaba Sekondari, Naibu Waziri ulikuja, tunamalizia ule mradi pale lakini kuna miradi mipya pia ambayo naona nimeipata huku kwenye Bajeti hii ambayo imesomwa leo. Nina mradi wa Nemba, nina mradi wa Kikomanabusili, nina mradi wa Nyamigogo, Songambele na Kagoma, nina mradi wa Migango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii naomba niwashukuru. Lakini mwaka jana mwezi wa kumi tulipita eneo la Nyakahula na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nadhani pale kesi kubwa ilikuwa ni maji na baada ya kuwepo pale tulikuwa na taarifa kwamba tunaenda kufanya design pale ya mradi mkubwa wa maji wa kuhudumia lile eneo. Mwanzo tulitegemea kutumia mto lakini kwa sababu ya jiografia ya Biharamulo visima ukitaka kuchimba lazima vinakauka, viwe vya muda mfupi.

Kwa hiyo, tumeona sasa kwenye Bajeti hii imetengwa pesa kwa ajili ya kwenda kufanya upembuzi yakinifu na design ili tuweze kupata mtu wa kutekeleza mradi mkubwa wa maji ambayo utaondoa tatizo la Nyakahula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimshukuru Katibu Mkuu, tukiwa pale na Waziri Mkuu baada ya ile ziara nilim- contact tukaletewa pesa ya pampu mbili za kilowati 22 pale, zimeshafungwa na kazi inaendelea. Lakini sasa kikubwa ambacho kipo, lile bwawa la Nyakahula ni bwawa ambalo limejengwa tangu wakati wa Mkoloni. Limeshajaa tope sana, sasa kwa taarifa nilizonazo tulishaleta maombi hapa ya pesa milioni 148 kwa ajili ya kwenda kusafisha lile bwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri kesho utakapokuwa unahitimisha nipate majibu sasa zile pampu tulizozifunga pale kwa pesa nyingi zisivute udongo impeller zikaharibika, tukanunua tena pampu nyingine. Kwa sababu uwekezaji umefanyika ni vizuri tukamalizia ili kazi ya kuwapatia maji wananchi wa Biharamulo hususan Kata ya Nyakahula iweze kumalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu kikubwa kabisa kabisa ambacho ninacho leo napenda nishukuru kampuni au Shirika la CBHCC hawa ni wadau wa maendeleo wametusaidia sana maeneo yetu ya Biharamulo kwa kutekeleza miradi katika Kijiji cha Kasiro na Kijiji cha Luganzu wametusaidia kujenga miradi ya maji pale. Lakini vilevile tuna tunatarajia kwamba katika Mwaka huu wa Fedha wametuahidi watachimba visima 12 katika maeneo mbalimbali ya Biharamulo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wana ujenzi ambao unaendelea katika maeneo ya Ntumagu na Lusenga. Kwa hiyo, lazima niwashukuru kwa sababu ni wadau wa maendeleo ambao wanatuunga mkono kwa sehemu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikirejea jambo langu la mwisho wakati namalizia. Mheshimiwa Waziri naomba nikushukuru. Naomba nikushukuru kwa sababu Biharamulo ni sehemu ambayo tumekuwa na kilio kikubwa sana cha muda mrefu cha maji. Ziwa Victoria liko hapo umbali wa kilomita 50 tu kutoka Biharamulo. Tumekuwa tunajiuliza yaani maji yanaenda sehemu nyingine, Biharamulo hatuna chanzo cha kudumu cha maji. Mwaka juzi wakati wa kampeni aliyekuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi aliahidi mradi mkubwa wa maji wa kuondoa kero ya maji ya muda mrefu kwa Wilaya ya Biharamulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikushukuru kwa sababu kwa meeting ambayo tumefanya nadhani jana na juzi mmenihakikishia na mkamwambia Meneja kwamba asiondoke Dodoma bila kupata barua ya kwenda kutangaza ule mradi. Kwa hiyo, kwa niaba ya wananchi wa Biharamulo walionituma hapa, sina budi kukushukuru, nakupongeza sana lakini zaidi nimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu mnafanya kazi ya kumuwakilisha humu ndani na kilio chetu watu wa Biharamulo kimesikika. Tufikishieni salamu kwa sababu sasa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria unaenda kuingia katika Wilaya ya Biharamulo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata sisi kwa mara ya kwanza tunayaona maji ya ziwa pale ambapo tulikuwa tunakutana nayo huku tukisafiri wakati ziwa lilikuwa karibu na sisi pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo Mheshimiwa Waziri nadhani nina ombi moja maalum. Tumekuwa na kijana huyu Meneja wa RUWASA ni Injinia mwenzangu, Injinia Matina amekaimu muda mrefu sana. Sasa hata kukaimu kwenyewe inafikia stage unakata tamaa. Kijana huyu anashinda maporini kule, anashinda anahangaika mkizingatia maeneo yetu kule, hebu basi mtoeni kwenye kukaimu mu-approve sasa awe Meneja wa Wilaya. Hilo tu ndiyo ombi langu nikuombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namshukuru sana Meneja wa Mkoa, Injinia Sanya amekuwa msaada mkubwa hata katika miradi midogo midogo kwa sababu mara nyingine tumekuwa tunashauriana kitaalam. Anapokuja ni mwepesi hata wa kufika Biharamulo, ukimpigia simu anafika anatutendea haki. Kwa hiyo, ninaomba ombi langu Meneja wa Wilaya naomba Mheshimiwa Waziri kesho tamka neno ili roho yangu ipone na roho ipone. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)