Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia Wizara hii ya Maji. Lakini kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kunipa afya njema na kuweza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji Nyamtukuza Bukwimba. Mradi ule kwa kweli ulikuwa ni mradi ambao Mheshimiwa Waziri wa Maji anasema kichefuchefu. Lakini mradi ule ulikuwa ni kichefuchefu zaidi kwa sababu mradi ule ni tangu 2014 tuliuanza kutekeleza lakini kulitokea mambo mbalimbali ambayo yaliwasababisha baadhi ya Mawaziri kuja kuutembelea mradi ule. Naomba niwataje wale Mawaziri waliokuja kuutembelea mradi ule ambao ulikuwa na matatizo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo uliweza kutembelewa na Waziri wa kipindi kile Profesa Mbalawa alifika kwenye mradi ule lakini pia Injinia Kamwelwe na yeye alifika kwenye mradi ule. Lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa na yeye alifika kwenye mradi ule. Lakini pia Waziri wa sasa wa Maji Aweso pia amefika kwenye mradi ule pamoja na Naibu wake Waziri amefika kwenye mradi ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, mradi ule uliweza kutembelewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maji wa kipindi kile Kitlya Mkumbo naye alifika. Lakini Katibu Mkuu wa sasa naye alifika kwenye mradi huo wa maji wa Injinia Sanga. Kwa kweli nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ulipofika kwenye ule mradi kwa kweli ulitoa maagizo makali na mradi ule ukaanza kwenda. Lakini alivyokuja Waziri Aweso yeye ndiye alikuja na moto mkali, aliwatia pingu baadhi ya Makandarasi na mradi ule ukaenda speed. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, Naibu Waziri na yeye alikuja na moto mkali kwa kweli tunashukuru mradi ule mpaka sasa hivi umeanza kutoa maji. Wananchi wa Nyang’hwale wanaipongeza sana Serikali lakini pia wanakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Aweso pamoja na Naibu wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna vitu nataka niviseme. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji wa Nyang’hwale. Lakini pia nizidi kumpongeza Waziri wa Maji rafiki yangu Juma Aweso pamoja na Naibu Waziri wake Prisca Mahundi pamoja na Katibu Mkuu Sanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu umeenda kukamilika lakini nizidi kuipongeza Serikali kwa kuendelea kukamilisha miradi mikubwa nchini ikiwemo mradi huo wa Nyamtukuza, Nyang’wale lakini pia Bukwimba. Mradi huu kwa bahati mbaya umekuwa na maji ambayo si mazuri kwa matumizi ya binadamu. Mradi huu umeenda kukamilika, hauna chujio la maji. Mpaka sasa hivi wananchi walio wengi wanaogopa kuunganisha maji na kuyatumia maji yale kwa sababu yanaweza kuharibu afya zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba Serikali Mwaka wa Fedha 2022 tuliweza kutengewa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi 2,400,072,000/= lakini fedha hizo tumeweza kupokea bilioni mbili peke yake. Ina maana kuna upungufu ambao hatukupata hizo pesa karibu milioni miatatu naa. Na Mwaka huu tumetengewa 2,098,000,000/= kwenye Bajeti hii ambayo tunaenda kuipitisha hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu sikivu iweze kuzitoa fedha zote hizo ili tuweze kukamilisha mradi huo ikiwemo kujenga chujio la maji kwa sababu ndiyo kipaumbele chetu. Lakini cha ajabu nimeweza kuangalia kwenye kabrasha tenki letu lile limeshafanyiwa usanifu. Tenki la uchujaji wa maji ambalo litagharimu bilioni 1.8. Lakini Wizara mmetutengea milioni 220. Huu mradi wa kujenga hilo chujio utakamilika lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi wanamatumaini makubwa sana, Mheshimiwa Aweso kwamba utatupa hiyo bilioni 1.8 tuweze kujenga hilo chujio la maji ili tuweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nikwambie ukweli, mradi ule tumeusubiri kwa muda mrefu sana tangu mwaka 1975 wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale hawajawahi kunywa maji ya bomba. Kwa hiyo, matumaini yao ni makubwa sana kwamba sasa hivi mradi huu utaenda kukamilika. Tutaweza kuyasambaza maji haya kwenye Kata zifuatazo; Kata ya Nyamtukuza, Kata ya Kakola, Kata ya Nyugwa, Kata ya Karumwa, Kata ya Kafita, Kata ya Nundu, Kata ya Bukwimba, Kata ya Busorwa, Kata ya Kaboha, Kata ya Nyang’wale, Kata ya Shabaka, Kata ya Izunya, Kata ya Nyabulanda, Kata ya Mwingilo, Kata ya Nyijundu na Vijiji vyake. Tuna matumaini makubwa sana ya mradi huu kupunguza kero ya maji ya tangu mwaka 1975. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe Wizara ya Maji kuhusu mradi mkubwa ambao unatekelezwa kutoka Mangu kwenda Ilogi. Mradi wa pamoja kati ya Serikali na Mgodi wa Bulyang’uru. Mradi ule tayari umekamilika, naiomba Wizara sasa iruhusu maji haya yaanze kutumika kwenye Vijiji vifuatavyo. Maji haya yako tayari kutumiwa lakini tunashangaa kwa nini Wizara haijatoa kibali ili maji yale yaanze kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuomba Mheshimiwa Waziri Aweso toa kibali ili maji haya wananchi waanze kuyatumia kwa sababu maji haya ni safi na salama ambayo yanatoka Ihelele kwenda Shinyanga. Maji haya yanapita kwenye Kijiji kifuatacho; yanapita Ngushimba, yanapita Nyugwa, yanapita Mwamakiligwa, yanapita Kafita na Lushimba. Toa kibali ili wananchi hawa waanze kunufaika na haya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri naamini kabisa utendaji kazi wako na uchungu ulionao, kibali hiki hutachelewa kukitoa, Viongozi wengine wote walioko hapa wa Wizara ninaamini wamenisikia kilio cha wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale lakini mradi huu wa Ilogi-Mangu upewe kibali ili wananchi waweze kuyatumia maji haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nitumie nafasi hii ya kuwapongeza Mameneja wafuatao; kwanza Meneja wa Mkoa wa Geita, Injinia Jabir lakini pia Meneja wa Wilaya ya Nyang’hwale Injinia Moses. Ukweli watu hawa tunashirikiana nao vizuri sana, kama Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale pamoja na Wabunge wa Mkoa wa Geita tunaamini na tunawaamini kazi zao wanachapa kazi. Kama kuna promotion zaidi ya hapo basi jaribuni kuwaangalia. Lakini tunaomba wabaki pale angalau hata kama ni miaka mitano sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nadhani kilio changu leo kikubwa ilikuwa ni chujio la maji. Zitolewe hizo bilioni 1.8 na zitolewe hizo bilioni 2 tuweze kusambaza maji kwenye Kata ambazo nimezitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)