Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ambaye ameniwezesha jioni ya leo kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kuchangia hotuba ya Waziri wa Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri mwenye dhamana na Wizara hii, Naibu Waziri, Katibu Mkuu ndugu yangu Sanga, Injinia wetu wa Mkoa wa Mtwara, Injinia wangu wa Wilaya ya Nanyumbu na watendaji wote wa Wizara ambao kwa njia moja au nyingine wameshiriki kikamilifu katika uandaaji wa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru mashirika ya dini. Tunalo shirika kule kwetu linaitwa Life Ministry ambao kwa kweli wamechangia sana katika harakati za kupambana na shida ya maji ndani ya Jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani za pekee zimwendee Rais wetu, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Sisi watu wa Nanyumbu tuna kila sababu za kumshukuru sana mama huyu. Tangu ameingia madarakani kuna mapinduzi makubwa ya maji ndani ya jimbo langu. Wananchi wa Kata ya Mikangaula ni mashahidi. Kijiji cha Mikangaula, Kijiji cha Chang’ombe wao walikuwa hawajui maji ya bomba. Tangu mama ameingia madarakani, sasa hivi ninavyozungumza wanakunywa maji ya bomba. Hongera sana mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kamundi Kijiji cha Nawaje walikuwa hawajui maji ya bomba. Hivi ninavyozungumza, kuna DP zaidi ya 10 ndani ya Kijiji. Kwa kweli mama anafanya kazi kubwa sana na sisi watu wa Wilaya ya Nanyumbu tunasema yule anayemsema vibaya mama, alaaniwe. Kwa sababu ameonyesha mapinduzi makubwa sana ndani ya wilaya yetu. Kijiji cha Mkoromwana kulikuwa kuna shida kubwa ya maji leo kuna maji. Ukienda Kata ya Nangomba kuna DP zaidi ya 23. Kijiji cha Nangomba, Kijiji cha Kilimanihewa leo wana maji ya bomba, mambo ambayo huko nyuma hayakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, mama anafanya kazi, tuwe wakweli. Leo sisi tunalo bwawa, tuna mabwawa mawili Mheshimiwa Waziri. Ulikuja Bwawa la Maratani tukakushtakia kwamba hapa kuna mchezo mchafu umefanyika ndani ya lile bwawa, ulichukuwa hatua pale pale. Hivi ndivyo inavyotakiwa. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri na Menejimenti yako yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge tunapoleta malalamiko, hatumwonei mtu. Tunazungumza ukweli. Kwa hiyo, nakupongeza sana. Rai yangu Mheshimiwa Waziri, pale Maratani uliahidi kwenye Mkutano Mkuu mbele wa wananchi kwamba kwa kuwa bwawa lile lilichezewa na yule Injinia, kwanza ulimfukuza kazi siku ile, nakupongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia aliahidi kutoa visima viwili kila Kijiji, jambo ambalo mpaka leo halijatekelezwa. Sasa hili Mheshimiwa Waziri nakuomba, kesho utakapokuwa una- wind-up ni kutamka tu vile visima viwili kila Kijiji unatupatia. Wananchi tutakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ukienda Kata Nandete kule kulikuwa na mradi mkubwa sana wa maji, nami nilikuomba, hebu leta timu ya wakaguzi, watu wamechakachua ule mradi kule Nandete. Mradi umetumia fedha nyingi, lakini ule mradi hautoi maji ya kutosha. Ule mradi hatutakubali fedha za Serikali, fedha za walipa kodi watu wachache wanufaike nazo, hili jambo halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, tukitoka hapa atoe maagizo watu wakaufanye ule ukaguzi. Holola Kata ya Mnanje kuna mradi wa World Bank. Wananchi pale walijua wamepata mkombozi, lakini ule mradi tangu umezinduliwa haujatoa ndoo hata moja. Naomba waliohusika na ubadhirifu wa ule mradi wachukuliwe hatua. Hili jambo halikubaliki. Muda wa kuchezea maji, muda wa kuchezea fedha za Serikali kwenye miradi ya maji, ndani ya wizara yako, mbele ya wewe Waziri, najua muda umekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi 28, miji 28. Wilaya yangu ya Nanyumbu ni mmoja wanufaika wa miji 28. Wilaya ya Nanyumbu iko ndani ya Mkoa wa Mtwara. Mimi nasema hongera sana Mheshimiwa Waziri. Mradi huu unatoka Kilometa 65 kuja Mji wa Mangaka. Mahali ambapo bomba litapita kutoka Masuguru kuja Mangaka, vijiji vyote vitanufaika na mradi huu. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu, umeongea katika bajeti hapa kwamba unategemea Rais azindue huu mradi. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, ufanyike uzinduzi hapa hapa Dodoma kabla Bunge lako hili halijavunjwa. Wabunge wa miji 28 tupo hapa Dodoma, tuwaombe viongozi wetu wa Mikoa wa Chama cha Mapinduzi, viongozi wetu wa Wilaya waje Dodoma washuhudie utiwaji wa sahihi wa miradi hii. Jambo hili litakuwa na manufaa sana na afya sana kwa Chama cha Mapinduzi kwa sababu ndani ya ilani yetu tumeongea bayana, tutatoa maji kwenye miji 28. (Makofi)

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI. Taarifa Mheshimiwa Yahya.

T A A R I F A

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Yahya Mhata kwamba mradi huu wa miji 28 tumeuzungumza toka 2016, na ndani yake wamepita Mawaziri sio chini ya wanne. Nami nilishashika Shilingi hapa zaidi ya mara tatu.

Kwa hiyo, kwa kuwa sasa tumefikia hatua ya kusaini na wakandarasi, nami naomba kumpa taarifa kwamba hiyo itakuwa ni heshima kubwa sana, viongozi wa Mikoa hiyo wa Wilaya na Halmashauri hizo kuweko kwenye hiyo signing ceremony na wakandarasi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya, taarifa hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Cosato Chumi.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kwa mikono yote. Kwa hiyo, ni matarajio yangu kama nilivyosema, jambo hili litafanyika haraka iwezekanavyo ili Wabunge tushiriki na twende tukasimamie utekelezaji wa miradi hii. Kuna watu wanadhihaki, wanasema tunadaganya. Twende tukawathibitishie, muda ule wa uongo umepita, tunataka kazi na kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Katibu Mkuu wa Wizara hii, ndugu yangu Sanga, mwezi wa kumi alikuja Nanyumbu. Tulimpeleka kwenye chanzo cha maji cha Masuguru, aliona adha iliyokuwepo. Kwa uchungu mkubwa, ndugu yangu Sanga aliahidi kwenye Mkutano kwamba signing ceremony itakuja kufanyika kijijini hapa mkandarasi atakapokabidhiwa mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nami niliahidi…

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Yahya Mhata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aliposema kwamba kuna baadhi ya watu walikuwa wanasema tunadaganya, mwaka 2020 kwenye jimbo langu na Diwani wa Upinzani alikuwa anasema mimi mwongo. Nikawaambia wananchi, kama mimi ni mwongo, mpeni kura. Mkimpa kura, kwenye Kata yenu tutawaondoa kwenye mradi. Hawakumpa kura. Kwa hiyo, wananchi wanasubiri kwa hamu sana maji. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa sababu kuna watu wamezaliwa kwa kusema uongo. Sasa muda wa kuthibitisha uongo wao umefika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu alipokuja pale Mangaka aliona adha kubwa ya akina mama; ndoo ya maji tulifikia hatua tunanunua kwa shilingi 2,500. Katibu Mkuu kwa uchungu mkubwa alitoa shilingi milioni 100 ili zitumike kutatua tatizo la maji ndani ya Mji wa Mangaka na Kilimanihewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchungu na masikitiko makubwa fedha zile mpaka leo hii hazijatoa matokeo. Nakuomba ukafanye ukaguzi wa ile Shilingi milioni 100. Haiwezekani Katibu Mkuu aje pale, atoe shilingi milioni 100 mwezi wa Kumi, mpaka tunapozungumza leo hakuna hata tone la maji. Cha kuchangaza, jirani kwa ule mradi, kuna mtu binafsi ametoboa na anauza maji ndoo shilingi mia 500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa Shilingi milioni 100 mwezi wa Kumi mpaka leo hakuna maji. Hiki kitu akikubaliki. Hawa watendaji wanaotuchezea, hatukubali wawe ndani ya wilaya yetu. Ndiyo maana nilimwambia Mheshimiwa Waziri, hii MWANAWASA ni Masasi na Nachingwea, Nanyumbu unahusisha vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani sisi watu wa Nanyumbu tuwe chini ya Mamlaka ya Mji wa Masasi na Nachingwea. Ndiyo maana tunachezewechezewa kama mpira wa kona. Haiwezekani Unatoa Shilingi milioni 100 kuja kutatua tatizo la maji kwa Mji wa Mangaka na Kilimanihewa, maji hayapatikani. Naomba usipeleke hata senti tano. Kakague kwanza ule mradi tuone matokeo ya ule mradi. Hili jambo halikubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka Mheshimiwa leo au kesho utoe kauli, ni lini Wilaya ya Nanyumbu itakuwa na Mamlaka yake ya Maji? Sisi Masasi tunawajibika vipi na Kilometa 54 kutoka Nanyumbu? Hili jambo siyo sahihi. Ile ni Wilaya kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nanyumbu ni wilaya kamili, inajitegemea, ina wataalam wake. Lazima tuwe na mamlaka yetu ya maji ili tuwe na maamuzi ya kufanya. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Naomba yale ambayo nimeyaeleza kesho nitayafuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Yahya.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga sana mkono hoja. Naomba yale ambayo nimeyaeleza kesho nitayafuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)