Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami jioni hii niweze kuchangia Wizara hii ya Maji. Kwanza niweze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo naomba nianze kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Katani Ahmadi Katani. Ninakuomba nikuambie kwamba kile ambacho Mheshimiwa Katani amekisema ndiyo sauti, ndiyo kauli ya wananchi wa Kusini wanavyoiona siyo tu Wizara ya Maji, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, miradi kusuasua ya Kanda ya Kusini siyo miradi tu ya maji. Mimi ninayo mifano, kuna mradi wa mbolea kiwanda cha mbolea cha Kilwa haieleweki kiko wapi, kuna LNG Mtwara haieleweki, kuna reli hii ya Mtwara Mbamba Bay haieleweki, kuna hii miradi ya REA, nenda ukafanye sensa miradi ya REA Vijiji vilivyokamilika Kusini na Vijiji vilivyokamilika sehemu zingine havifanani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa upande wa barabara, barabara za Kusini zilizokamilishwa upembuzi yakinifu mwaka 2014 lakini mpaka leo zinatafutwa fedha hazijapatikana, lakini ziko barabara zitakamilika upembuzi yakinifu mwaka 2018 leo zinazo Wakandarasi zinajengwa nchi ni hii moja! Kwa hiyo, mimi nataka niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Katani kama ni kweli ndivyo watu wa Mkoa wa Lindi na Mtwara tunavyoiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna watu wamekaa wamefikiria kuyatoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka Tabora na kuna watu leo wanakaa wanafikiria kuyatoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka Dodoma, watu hao hao hawafikirii kuyatoa maji Mto Rufiji kuyapeleka Lindi siwaelewi! Watu hao hawakai kufikiria kuyatoa maji Rufiji kuyapeleka Liwale haieleweki! watu hao hao wanakaa hawawezi kufikiria kuyatoa maji Mto Ruvuma kuyapeleka Mtwara haieleweki! Kama unaweza kuyatoa maji Ziwa Victoria kuyaleta Dodoma ukashindwa kuyatoa Ruvuma kuyapeleka Mtwara, ukashindwa kuyatoa Rufiji kuyapeleka Lindi siyo sawa sawa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso huu msalaba siyo wa kwako peke yako ndiyo maana nikatoa mifano mingine, tukae tufikirie. Mwaka jana nilichangia nikasema keki ya Taifa tunapokwenda kuigawa basi tuangalie tunaigawaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso mimi nikushukuru sana, mimi na wewe tumepambana kutafuta chanzo cha maji kwa Mji wetu wa Liwale, bahati nzuri sisi kwa sababu ni watu wa visima virefu mnatufikiria hilo tunashukuru kwa hilo, maana kuna watu wanafikiria kupatiwa miradi ya maji kutoka kwenye vyanzo vikubwa vya maji, sisi tuendelee na visima virefu, mimi nakushukuru kwa visima virefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa miradi nimeona kwenye kitabu chako kuna visima virefu vinaenda kuchimbwa Makata, Kiangara, Naujombo, Ngorongopa, Nangano, Hangai na Ngongowele, nakushukuru kwa hilo. Nakuomba kwa sababu miradi hii kuiona kwenye vitabu siyo mara kwanza, naomba hii iwe mara ya mwisho kuviona itakapokuja tena naomba iwe imekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunavyo vijiji vya Mlembwe, Nahoro, Mkutano, Kipulungwe hivi vijiji bado sijaviona, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri shida ya maji Liwale unaijua, Naibu Waziri amefika na wewe mwenyewe umefika, nakuomba sana sisi kwa sababu level yetu ni ya visima virefu mtuletee hivyo visima angalau tuone kwamba tunapata miradi hii ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunao mradi mkubwa wa maji kwa ajili ya Liwale Mjini. Tayari Mheshimiwa Waziri ninakushukuru umeshaleta Mkandarasi ameshatuchimbia visima virefu vitatu kwa ajili ya maji katika Mji wa Liwale lakini Mkandarasi mpaka leo hajafanya pump test kwa sababu hajapata fedha za mradi ule. Ninakuomba sana tumpatie fedha Mkandarasi afanye pump test aone kama maji yako salama, basi mradi mkubwa uanze tuyalete maji Liwale Mjini. Watu wa Liwale wanasubiri sana maji kutoka kwako, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba nitoe ushauri, tunalo tatizo kubwa sana la maji, vyanzo vikubwa tunavyovizungumza hapa ni mito, maziwa na visima virefu lakini haya maji ya Mungu ambayo yanateremka yanamwangika kila mahali tunafanya mkakati gani ya kuvuna haya maji yakatusaidia? Mimi ninaiomba Wizara mkae muangalie miradi ambayo itawezesha kuvuna maji ya mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwenye hiyo miradi ya uvunaji wa maji tuje na sera, kwamba majengo yote ya taasisi ikiwemo shule, hospitali na ofisi zote za Serikali tuvune maji, kama tumeshindwa kuvuna maji kwenye majumba ya watu binafsi kila mtu na matakwa yake lakini kwanini tusitoke na sera kwamba kila jengo la Serikali liwe na utaratibu wa kuvuna maji ili tupunguze adha ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niende kwenye utunzaji wa vyanzo vya maji, wako wataalam wetu wanahamasisha watu kupanda miti kuzunguka vyanzo vya maji lakini utaalam wa kujua miti gani inafaa kupandwa ili kulinda vyanzo vya maji haujafanyika kikamilifu. Wako watu wanapanda miti ambayo inanyonya maji badala ya kutunza maji, maana kiutafiti iko miti ambayo, hata kienyeji wazazi wetu kule nyumbani wanajua kabisa mti fulani ukiwepo kwenye mto huo mto haukauki miaka nenda rudi ndiyo maana inaitwa miti maji.
Sasa naomba Wizara mje na utafiti mnapohamasisha watu watunze vyanzo vya maji kwa kupanda miti muangalie miti gani wapande, kwa sababu kuna mahali ambapo unakuta kuna mto lakini baada ya miaka mitano ukipanda miti mto unakauka kwa sababu mmepanda miti ambayo inakausha maji badala ya kutunza maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye Jimbo langu nizungumzie kuhusu vitendeakazi. Mheshimiwa Aweso unajua jiografia ya Liwale, Fundi wa maji kumtoa Ngong’owele kumpeleka Mpigamiti, kumtoa Mpigamiti kumpeleka Liwale Mjini akafanye kazi, anakwenda kwa usafiri gani? Gari pale Liwale liko moja tu tena bovu na hilo gari ni la Meneja kwa hiyo wale mafundi wengine wote hawana usafiri, hawana gari wala pikipiki. Ninakuombe sana tupatiwe vifaa, vitendea kazi ili miradi yetu ya maji iweze kusimamiwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niendelee kukushukuru kwa ule mradi wetu wa fedha za UVIKO zilizokuja Liwale kwa ajili ya kupata maji, maji ya Liwale ni maji salama lakini siyo safi, ili yale maji yawe safi tumepata mradi mkubwa wa kujenga mtambo wa kuchuja maji, ule mradi unasuasua na usipoutolea macho ule mradi ile fedha inaenda kupotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumekwenda pale na mwenge kwa kweli aibu tuliyoipata pale, hata mimi mwenyewe nimekwenda na ile gari ya mwenge nikapata aibu, kwa kweli ule mradi hauendi, shida kubwa ni Mkandarasi, hatuna Mkandarasi. Liwale tunatatizo kubwa sana la kuwapata Wakandarasi wanaoweza kusimamia miradi ya maji na matokeo yake yule anae-tender kama ni mtu mmoja kwa sababu ni mtu mmoja na lazima mradi utekelezwe lazima tumpe huyo huyo na matokeo yake mradi hauendi. Kwa hiyo, mimi naomba utusaidie katika hilo miradi hii ya maji kwanza ipate Wakandarasi ambao wanafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho mwanzo nilianza na kulalamika sasa hivi silalamiki nashauri, maji ya Mto Rufiji tunayahitaji Mkoa wa Lindi na Mtwara na inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)