Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kuchangia katika Wizara hii muhimu inayogusa maisha ya watu wetu Wizara ya Maji. Kwanza kabisa ningependa kabisa ningependa kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Wizara ya Maji kwa kazi kubwa wanayoifanya lakini pongezi za pekee nizipeleke kwa mamlaka yangu ya maji ya KUWASA Eng. Mbike ambaye ni Mkurugenzi Bodi ya Wakurugenzi, pamoja na watumishi wote wa KUWASA kwa kazi nzuri wanayoifanya katika mamlaka yetu ya maji yaliyowezesha kushika nafasi ya 10 bora katika Mamlaka za Maji ambazo zipo Makao Makuu ya Mkoa, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu katika mwaka wa 2015/2020 walipewa malengo na Chama chetu kupitia Ilani ya Uchaguzi, wakawatoa watu wa vijijini kupata maji kutoka asilimia 47 hadi asilimia 70.1, na watu wa mijini kutoka asilimia 74 hadi 84. Kulikuwa na kazi kubwa sana, vijiji walikwenda mpaka asilimia 23 waliongeza. Kwa hiyo, walifanyakazi kubwa kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepewa lengo ukisoma Ilani ya Uchaguzi Ibara 100 tumepewa lengo mwaka wa 2020/2025 tutoke vijijini kwenye asilimia 74 hadi tufikie asilimai 85, na mijini tutoke kwenye asilimia 84 hadi asilimia 95 na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii ni kubwa na ninaona tumeanza kukata miaka sijui kama tutaifikia, lakini namuamini sana Mheshimiwa Waziri na timu yake wakiwa serious kama walivyo sasa na wakaendelea kusimamia bila kulewa sifa tunaweza tukafanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mamlaka yetu ya maji mpaka sasa tumefikia asilimia 87 maana yake tumeongeza asilimia tatu tu kutoka lengo au kutoka tulipokuwa mwaka wa 2015/2020 sasa bado tuna asilimia nane kufikia 2025, kazi ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na wote wanaomsaidia, fedha zinakuja na kazi inakwenda. Hivi karibuni sambamba na fedha za bajeti tulipata fedha za UVIKO na kazi imekwenda, tumeweza kuongeza mtandao wa maji kutoka kilometa 354 kufika hadi kilometa 464. Bado tunazo kama kilometa 135 zinatudai katika kusambaza mtandao wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo mamlaka ambazo zimepewa jukumu la kujitegemea katika kuendesha miradi ya maji, mamlaka yetu ya KUWASA ni mojawapo. Mamlaka hii imepewa jukumu hilo ikiwa bado ni changa na hili ningependa Waziri anielewe vizuri na ikiwezekana kesho anaposimama hapa kufanya majumuisho afanye mapitio kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka kubwa ambazo zinajiendesha kama vile za Dar es Salaam, Mwanza, Iringa zimeweka utaratibu mzuri sasa wa kutoa ruzuku ya kuwaunganishia maji watu ambao wana low income, wameanzisha kama REA yao ya umeme vile kwamba watu ambao wapo kwenye low income wanawaunganishia maji bila kulipa gharama za kuunganisha ili watakapoanza kuyatumia yale maji waweze kuendelea kulipa bili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mpango mzuri sana hamuwezi kuwa REA katika umeme mkaacha katika maji lazima mjue kwamba maji hayana mbadala. Umeme mtu akikosa atawasha hata kibatari lakini maji hayana mbadala lazima sasa Wizara ije na mpango wa hawa watu wa low income wawe wanaunganishiwa maji ili kazi yao iwe ni kulipa bili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri ningekuomba kesho unapofanya majumuisho hapa uzieleze Wizara nyingine ambazo zinakukwamisha zinazuia kazi yako isifanikiwe, kama umeunda mamlaka na unataka zijitegemee lakini zipo Wizara ambazo zinatenga pesa kwa Wizara hizo kwa ajili ya kulipa maji halafu hawalipi maji na wanasababisha mamlaka zetu zishindwe kufanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, pale kwenye mamlaka yangu ya Kigoma Wizara ya Mambo ya Ndani inatukwamisha sana Polisi wanadaiwa Milioni 141 katika Mamlaka Ndogo kama ya kwetu. Magereza wanadaiwa Milioni 226, JWTZ wanadaiwa Shilingi Milioni 40 kiasi cha Shilingi Milioni 405, kwa Mamlaka Ndogo kama ile, hicho ni kwa mamlaka tu hizi za Serikali sitaki kutaja wengine ambao wanadaiwa Milioni Tatu, Nne, Tano, sasa hii hawa wanakushika mkono wewe kazi yako isifanikiwe, utakapo kuja hapa nataka nikusikie namna unavyosema na watu wa Wizara hizi ambazo wanatengewa bajeti ya kulipa maji halafu hawalipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri unajua kwamba vyombo kama hivi Polisi, Magereza, JWTZ ni ngumu Mamlaka ya Maji kwenda kukata maji kwao lakini mamlaka hiyohiyo ambayo inajiendesha isipolipa TANESCO kwenye pump za maji wanakatiwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri tulikuomba fedha Bilioni 1.2 utusaidie ili tuweze kuendeleza mradi, naona kwenye bajeti hii umetungea Milioni 600, hebu angalia namna ya kutusaidia kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mradi wa Ziwa Tanganyika umekwama, ulianza mwaka 2013 leo ni miaka Tisa utafikiri ni Stiegler’s Gorge mradi wa maji miaka tisa haujakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mlianza na kampuni ya Spencon mkaipiga chini, mkaja Shanxi imemaliza kazi yake sasa hivi tunawale Sinohydro na ninasikia kwamba hata mwezi Saba mwaka huu hawatakuwa wamemaliza kazi. Tatizo kubwa lililopo ni usimamazi tu maana fedha ipo lakini usimamizi tu. Nikuombe sasa Wizara iwe makini kusimamia ili tuweze kufika mahala tunapotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mikoa mingine inapata maji au inawekewa mpango wa maji kutoka katika Ziwa Victoria, kwanini sisi tunafika mahala leo Kasulu kuna shida ya maji, Kibondo kuna shida ya maji, Kakonko kuna shida ya maji, Wilaya ya Uvinza kuna shida ya maji na maji yapo Lake Tanganyika hivi hawa nao tena wafike mahala wainue mikono kwa Mungu kuomba maji na maji yapo kwenye Mkoa wao? Kuyasogeza tu kuyafikisha Kasulu! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba Mheshimiwa Waziri utakaposimama kufanya majumuisho utueleze namna gani chanzo cha maji cha Ziwa Tanganyika kitakavyosaidia kuondoa tatizo la maji siyo tu kwa Kigoma Mjini bali kwa Mkoa mzima wa Kigoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)