Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Wizara ya Maji imetekeleza miradi mingi ya Kitaifa ambayo kwa kweli ukifika unajivunia. Kwa hiyo, tunapo mpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Katibu wake maana yake ni kwamba wanafanya kazi ambayo inaonekana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji kama ambavyo ndugu yangu Ng’enda pale amemaliza halina mbadala. Kwetu Magu tulikuwa na shida kubwa sana, ninakuomba sasa ndugu yangu Mheshimiwa Aweso kama itakupendeza mradi ule wa Magu Mjini umekamilika mwaka 2019 ni vizuri sasa ukazinduliwa ili uweze kuonekana kwamba ni mradi ambao kwa kweli unafanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapokupongeza wewe tunampongeza Ndugu Sanga tunawapongeza na Watalaam ambao mmetuletea. Engineer Msenyele kwa upande wa MWAUWASA kwa kweli anasimamia vizuri sana. Ule mradi wakati unakamilika ulikuwa una mapungufu mengi, Ndugu Sanga unajua lakini kwa kweli mpaka sasa hivi Watalaam ambao tunao pale wanafanya kazi vizuri mapungufu yamepungua sana. Tunaomba muwape ushirikiano kwa sababu wanawasaidia sana miradi hiyo kuhakikisha kwamba inafanyakazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC tumepita Arusha kuna mradi mkubwa sana. Kule Arusha ule mradi kwa kweli vyanzo vyake ulivyojengwa unaweza ukalisha Mikoa hata mitatu. Arusha yenyewe, Kilimanjaro na Manyara, ni mradi mkubwa mno nanimradi wa kielelezo kwa kweli tunawapongeza mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam tulipita Ndugu Luhemeja kwa kweli unafanyakazi kubwa sana, miradi yako haina query ni miradi inayoonekana na kwa kweli inawasaidia wananchi wa Dar es Salaam, endelea kumsaidia Waziri wa Maji pamoja na Katibu Mkuu mnafanyakazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina matatizo bado makubwa ya maji kule Magu. Ukiwa pale Mji wa Kisesa Kata ya Bujola, Kata ya Bukandwe, Kata ya Bujashi ile Miji ndipo sasa Jiji linapanukia kuja kuongeza Mji ule. Jiji la Mwanza na Ilemela wote wanahamia kwenye Kata hizo, bado kuna tatizo kubwa la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri unafahamu sana Ndugu Sanga tatizo hilo, kwa sababu hatua sasa hivi ule mradi wa Butimba ndiyo tunaoutarajia na kwa sababu tayari tenki pale limekamilika na nimeambiwa na Ndugu Msenyele kwamba tayari Mtalaam Mshauri ameshapatikana wa kusanifu ule mradi na mwezi ujao unaanza, ninaomba msaidieni Waziri ili uweze kwenda kwa kasi na Kata hizo Nne ziweze kupata maji ambayo yatatosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Kisesa, Bujora, Bukandwe na Bujashi ndiyo Mji wa kisasa sasa hivi, tusipowapatia maji hatuwatendei haki Watanzania hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tunawapongeza kwa sababu mnatusikiliza nyinyi, tunapokuja ofisini kwenu mnatusikiliza na kwa kweli tunaomba muendelee kuwa na moyo huo. Kwa sababu leo umeomba bilioni 700 lakini tunaona kumbe bilioni 700 hazitoshi ni vizuri sisi Wabunge hapa na Serikali tuone njia mbadala ya kuongeza bajeti tupate hata trilioni moja ili miradi hii iweze kukamilika kwa sababu kumbe tatizo siyo nyie watu wa Wizara tatizo ni fedha kidogo. Kwa hiyo, ni kazi yetu sasa sisi Wabunge kuhakikisha kwamba tunasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Ndagalu, Tarafa ya Ndagalu...

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa subiri taarifa, Mheshimiwa Amar.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mchangiaji Mbunge Kiswaga, Mbunge wa Magu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majuzi nilikuwa kwenye msiba pale Magu kwa kweli wananchi wa Magu wanakupongeza na wanaipongeza sana Serikali kwa kukamilika ule Mradi wa Magu wanampongeza sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, taarifa hiyo umeipokea?

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili kwa sababu Magu ilikuwa ni janga la Kitaifa kukosa maji na hicho ndicho kilichonirudisha humu na nitaendelea kurudi Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule Mradi wa Magu ni Mradi mkubwa Tarafa ya Ndagalu ina Vijiji 16 tayari tumeshafanya design tumeshaleta Wizarani hebu ione hata kama si bajeti hii, bajeti zijazo tuweze kuwapelekea maji watu wale kwa sababu ni mteremko kule anaenda kwa gravity hatutakuwa na gharama kubwa san Mheshimiwa Waziri. Mlione hili kwa sababu tunaamini kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuwahudumia wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli lazima nimpongeze Mkurugenzi wa RUWASA, Mkurugenzi Clement kwa kweli ni msikivu sana nilikuwa na matatizo makubwa sana kwenye Jimbo langu. Mradi wa Solar Bubinza ulikuwa umekwama kabisa leo maji yanapatika kwa usimamizi wake mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapowapongeza tunamaanisha, Serikali hii tunapoipongeza tunamaanisha kwamba inawatendea haki watanzania. Mradi wa Lugehe tunataka kuoboresha, Mradi huu utahudumia kata tatu, Kata ya Kitongosima, Kata ya Bwamanga na Kata ya Kahangara. Na kwa kweli mradi huu upo ukiboreshwa utasaidia sana wananchi hasa wale ambao akina mama wanapata tabu ya kuchota maji umbali mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi pia pale Nyambuge sasa pamekuwa ni Mji Mradi ule ni mdogo unapaswa uongezwe kwenda kule Matera na tayari tumeshaleta maombi haya Wizarani nazani Sanga unajua, tunaomba sana hili nalo uliangalia. Kule Sanjo maji yako kuanzia nukta moja ambapo wananchi wanakaa na tumeshaleta design katika Kata ya Rutare, Kata ya Kongoro, Kata ya Chabula ili waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana jambo hili Waziri wa Maji aweze kuliona ili tuweze kuwasaidia watu ambao wako karibu sana na maji lakini hawapati majisafi na salama. Maji wanayo lakini siyo safi wala salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana, tunajua nchi hii ni kubwa mahitaji ya wananchi ni mengi na hata tunajionea hapa swali likiulizwa la maji, nusu ya Wabunge wewe ni shahidi wanasimama wote kuuliza maswali ya nyongeza kwa ajili ya maji. Kwa kweli tuombe Serikali bajeti zijazo tuone mbadala tungeweza kusema tuongeze tozo mahala fulani lakini kwa ajili ya mfumuko wa bei tunakaa kimya ili tuweze kuangalia namna ambayo inaweza kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu hatujamkosea tutapata fedha nyingi kwenye mapato yetu ya ndani yakisimamiwa na wafadhili mbalimbali ambao wanaonyesha kutusaidia katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kazi hii ni ya kwenu, kazi ya usimamizi ni ya kwenu na sisi tutawasaidia kwenye Majimbo yetu, wale wataalam ambao mmetuletea tunashirikiana nao vizuri tunaamini kwamba tutaendelea kushirikiana nao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono hoja, ahsante sana.