Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Maji. Kwanza ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenipa afya njema niweze kusimama hapa kuchangia jioni hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwa kazi nzuri anayoifanya na ni Kijana mahiri kabisa. Mheshimiwa Waziri Aweso una nidhamu kiasi kwamba wewe ni kijana rijali hata siku hii ya leo umekuja kututambulisha mawifi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi, Mheshimiwa huyu wa Naibu Waziri wa Maji sisi hapa wote ni mashahidi. Wabunge wa Majimbo wanapokuwa wakiomba aweze kuwafikia Majimboni mwao amekuwa hasiti kufika anawaahidi na anafika, nakupongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Maryprisca Mahundi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango mkubwa sana kwenye Mkoa wetu wa Mbeya. Kwanza kabisa lengo kubwa la Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ni Kumtua Ndoo Mama Kichwani, na mama yetu huyu amekuwa na juhudi kubwa sana juu ya hilo. Lakini kwetu Mbeya kuna Mradi wa Kiwira ni Mradi mkubwa sana ambao utalisha Mkoa mzima wa Mbeya, mradi ule ni wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 200. Cha kusikitisha mradi ule umetengewa fedha kiasi cha shilingi bilioni tano, napata wasiwasi sana bilioni tano kwa kugawa hiyo bilioni 200 ina maana ni miaka 40 ijayo ndipo mradi huo uje ukamilike nikiwa tayari nimekuwa kikongwe kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wa Mkoa wa Mbeya wako busy sana kutafuta fedha kwa ajili ya kulisha familia zao. Wanawake wa Mkoa wa Mbeya huwezi ukamkuta mwanamke wa Mkoa wa Mbeya yuko kibarazani anapiga story, anacheza draft, anacheza sijui miboi sijui vitu gani. Wanawake wanatafuta pesa, sasa wanaacha kutafuta pesa kwa ajili ya kulisha familia zao wanahangaika kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata akina baba hapa ni mashahidi kwenye hili siyo Mbeya peke yake ni Tanzania nzima wanawake ndiyo wanahangaika na familia. Sasa wanawake wanabadilika kuacha kutafuta fedha za familia wanahangaika kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaongea hili kwa uchungu sana, Wilayani Rungwe kuna Mradi wa Maji ambao una thamani ya 4,500,000,000.00 niliongea hapa ule Mradi mabomba peke yake kwenye kutandaza kutoka kwenye chanzo cha Mto Mbaka inatakiwa fedha shilingi 1,800,000,000 ilitolewa 5,000,000,000. Lakini wakati huohuo Serikali ikatoa shilingi milioni 200 hiyo shilingi milioni 200 hata Kiwandani kwa ajili ya kwenda kuongeza mabomba haifai, wamekataa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naiomba sana Serikali naomba sana kwa dhati, ninaomba hii fedha kwa ajili ya mabomba ni force account inatumia nilikuwa naomba kwenye suala la kujenga tenki la maji, wamtafute Mkandarasi ili aanze kujenga tenki la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Tukuyu Mjini ni za kwanza kuathirika juu ya kutokupata maji, Kata ya Bagamoyo, Kata ya Msasani, Kata ya Makandana kwenye Kata ya Makandana eneo la Kioski ndiyo shida kabisa. Kuna Kata ya Kawetere, kuna Kata ya Idigi, kwa masikitiko makubwa hata kata ambapo anatoka mama mzaa chema nako maji hakuna ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana tuchukulie serious suala hili, sasa hivi kwenye hiyo bajeti imetengwa shilingi milioni 500 peke yake, milioni 500 itasaidia nini. Mabomba yale ile fedha mliyotota kwanza ile milioni 700 ya awali ni kilomita tatu tu kati ya kilometa 9.5. Mheshimiwa Waziri ninakuomba sana, sina lengo hata kidogo la kusema naweza kushika shilingi yako kwa sababu natambua wewe ni msikivu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni msikivu na hapa utakuja kuongea hiyo siku ya kesho wakati unavyohitimisha kwamba utapeleka fedha kwenye Wilaya ile ya Rungwe ili mradi uendelee. Narudia kukuomba tena kuhusu suala la kujenga tenki, kuhusu kujenga ninaomba atafutwe Mkandarasi ninashauri Serikali, naomba suala la fedha ya mabomba iongezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Halmashauri ya Busokero ninazidi kumshukuru Mheshimiwa Rais Mama Samia, nilikuwa nikiwalaumu watumishi kwamba hawafanyi kazi ipasavyo. Lakini fedha Busokero kule kulikuwa na changamoto mwaka jana kulitokea mafuriko kwenye Kata ya Isange na Kata ya Lwangwa. Lwangwa ndiyo halmashauri ndiyo mjini pale, watumishi wa Serikali na wananchi wote wanasumbuka na maji. Fedha ipo lakini utendaji wa kazi haupo, nawapongeza sana na mlipeleke. Kilichosikitisha zaidi Watendaji kwenye halmashauri kumbe wanatakiwa watoke kwenye Wilaya ya Rungwe. Lakini Watendaji hawa wa Wilaya ya Rungwe hawana usafiri wa kufika kule. Hawa watu wa RUWASA fedha za kununulia magari waliomba Benki Kuu ya Dunia walipewa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupewa fedha zile hawa watu wa GPSA ndiyo walipewa fedha miezi mitano iliyopita mpaka sasa hivi hawajaleta magari yale. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Ofisi ya Waziri Mkuu iingilie kati kutoa kibali ili magari yale yaweze kufika na Watendaji wale wapate magari ili waweze kufika site kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitashukuru sana kama hili litachukuliwa kwa uzito. Kwenye Mkoa wetu wa Mbeya nilikuwa naomba sana kuna fedha ambazo zinatoka Benki Kuu ya Dunia kwa mkopo nafuu, kuna Mikoa nane tu ambayo imeingizwa humo kwenye orodha. Ninaomba na Mkoa wa Mbeya uingizwe kwenye P4R ninaomba sana. Mheshimiwa Aweso ni msikivu sana wewe kaka, ninakuomba wakati unakuja kuhitimisha naomba nisikie kwamba Mbeya imeingizwa kwenye utaratibu wa P4R nitashukuru sana. Kwa sababu nitajua kwamba matatizo ya maji Mbeya yanaenda kuisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kata ya Rujewa kwa maana ya Mbarali pale kuna Mradi ambao umejengwa miaka ya 80 wananchi wameongezeka na sasa hivi ni maendeleo zamani tulikuwa tunakimbilia tukienda washroom nitakimbilia huko nje sasa hivi ni ndani, huko ndani kunatakiwa maji. Pale kile chanzo cha maji sasa hivi kinauwezo wa kutoa lita milioni 200 kwa siku, wakati mahitaji ya watu wa Mbarali kwenye Kata husika ya Rujewa pale wanataka kutumia maji lita milioni 700 kwa siku. Sasa uone ni namna gani upungufu wa maji upo kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo yale.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma muda wako umeisha ulipigiwa kengele nilikuachia dakika moja zaidi.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Dakika moja eeh.

MWENYEKITI: Malizia hiyo sentensi yako Mheshimiwa.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali walitoa wazo zuri sana wananchi wanaoishi Wilaya ya Chunya, Wilaya ile ya Chunya walijenga kisima, walichimba kisima lakini kisima kile hakijakamilika kwa sababu ya fedha. Kile kisima kilikuwa na thamani ya shilingi milioni 199 zilizotolewa fedha shilingi milioni 100 peke yake ambapo wamefanikiwa sawa kuweka mabomba. Lakini mambomba ya kuwasambazia wananchi kuwafikishia kwenye nyumba zao ni changamoto kwa sababu fedha hazijakamilika. Ninaomba sana hiyo fedha kiasi cha shilingi milioni 99 ziwafikie wenyeji wa Chunya ili Chunya pale mjini waweze kukomboka waweze kunufaika na maji yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninakushukuru sana. Ninaunga mkono hoja, ahsante.