Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Alhaj Aweso kwa juhudi zake na nyingi sana katika kubadilisha Wizara hii. Lakini nimshukuru vilevile Naibu Waziri dada yangu Engineer Maryprisca, vilevile kwa juhudi zake nyingi. Nimshukuru lakini Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Watendaji wote katika Wizara hii. Tumeona kwa kiasi kikubwa sana tulikotoka, tulipo na tunakoenda nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Njombe kama unachangamoto kubwa kuliko zote ni maji. Ukiniambia changmoto tatu nitazitaja maji, maji, maji. Laikini Mji huu una kitendawili kikubwa sana wengi hapa wanalalamika maji kwa sababu maji inabidi yavutwe kutoka sehemu nyingi. Njombe ni tofauti, Njombe tuna maji mengi ya kutosha, tuna vyanzo vingi vya maji, lakini cha ajabu ni kwamba bado kuna malalamiko makubwa sana ya ukosefu wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wetu wa Njombe pamoja na Vijiji ambavyo vipo katika Jimbo la Njombe Mjini tunapata maji kwa kiasi, wakati mvua kwa kiasi cha kama asilimia 60 mpaka 65. Lakini wakati wa masika tunapata maji kwa kiasi cha asilimia 40. Huwezi kuamini kama hii ni sehemu ambayo ina mvua nyingi, ina maji mengi, ina chemchem nyingi, ina vyanzo vingi vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yametokana na kutokuwa na mipango thabiti ya kuwekeza katika Miradi ya Maji kwa muda mrefu sana wa takribani miaka 20. Na Mji wa Njombe ni Mji unaokuwa kwa haraka sana kwa hiyo ulihitaji kuwa na mipango thabiti. Ndiyo maana nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Watendaji wote kwa kuwa na mipango thabiti sasa ya huko tunakokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nipende kusema kwamba pamoja na changamoto hizi lakini bado wananchi wa Njombe wana matumaini na nitasema kwa nini wanamatumaini. Katika hiki kipindi cha bajeti iliyopita wananchi wa Njombe tumeweza bado kunufaika na yale ambayo niliyaleta hapa kama kilio. Tumepata Mradi wa Kibena Howard Awamu ya Pili kiasi cha kama milioni 800 tulitengewe na Rradi ule umeshatekelezwa kwa asilimia 90 bado kiasi kidogo kuna tank kubwa sana linajengwa katika maeneo yale litakaloleta lita 150,000. Ni maendeleo makubwa na watu wameanza kupata maji katika maeneo yale. Tunamshukuru sana na Mheshimiwa Naibu Waziri alitutembelea na alitia changamoto katika kuhakikisha jambo hili linafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kutuangalia na sisi watu wa Njombe. Pamoja na matatizo yetu na vilio vyetu, tulipata fedha za UVIKO kiasi cha Shilingi milioni 520. Tumeweza kuongeza mtandao na kuboresha mtandao wa maji ingawa bado tuna shida kwenye vyanzo. Kwa hiyo, tuna Kilometa 12 mpya za mtandao wa maji ambazo zimekwenda katika mitaa mbalimbali kama SIDO, Posta, Matalawe, Mgendela na maeneo ya Ngalanga ambayo bado yalikuwa na tatizo kubwa la maji. Tumeanza kuona dalili nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na miradi mingine ya vijijini. Jimbo hili lina Kata za Vijijini na Kata za Mjini. Tuna miradi ambayo imekamilika, kama mradi wa Lugenge, Kisilo, Ihalula mpaka Utalingoro umeanza kutoa maji kwa mara ya kwanza. Tuna mradi wa Iduchu umezinduliwa tayari. Tuna mradi wa Kidunda na wenyewe kwa kiasi fulani umeanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru sana Serikali kwa maendeleo haya pamoja na hizo changamoto ambazo tunazo na bado ni kubwa na nitazielezea. Tuna miradi mingine midogo midogo ya vijijini ambayo tuna matumaini makubwa sana kwamba nayo itatekelezwa. Miradi hiyo ni kama vile Kijiji cha Kilenzi, wamekuwa na mradi wa muda mrefu ambao wao wenyewe walijitolea kutaka kuanza, tukawazuia tukisema Serikali yenu itawasaidia. Mradi huu najua sasa umetengewa fedha na nina uhakika katika kipindi hiki utatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna Kijiji cha Idihani na chenyewe kimeingia katika mpango wa utekelezaji katika mwaka huu wa fedha. Ombi langu kubwa kwa Wizara ni kuhakikisha kwamba fedha hizi ambazo zimetengwa hata kama ni kidogo kwa kuanzia, ziweze kupatikana kwa wakati ili Mkandarasi atakapoteuliwa aendelee na kazi mwanzo mpaka mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mingine miwili mikubwa ambayo na yenyewe ni muhimu sana katika kukomboa Mji wa Njombe kwa suala la maji; mradi wa Livingstone na Ijunilo wa kiasi kama cha Shilingi bilioni kama 10 hivi, ambazo na zenyewe tunajua ndiyo zinazohitajika lakini zilizotengwa ni fedha chache kwa muda huu kama shilingi bilioni moja. Tunaomba sana Wizara ituangalie, mradi huu uweze kupata fedha za kutosha ili uweze kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kwenda kwenye matumaini makubwa na masikitiko makubwa ya watu wa Njombe. Mradi wa Miji 28 Njombe tulikuwemo, tumekuwemo siku zote, na namshukuru Mungu kwamba bado tumo katika mradi huu. Nimekuwa nikiwaambia wananchi wa Njombe kwamba Serikali yenu bado ina mradi huu na bado mradi huu utatekelezwa. Imekuwa ni vigumu kuamini kwamba ni kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya tarehe 16 Aprili, 2022 wananchi wa Njombe waliniweka Kitimoto kwa kupitia mtandao mmoja mashuhuri sana unaitwa Uwanja wa Siasa, wakitaka maelezo ya mradi huu. Niliwapa maelezo ambayo namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwamba ameweza kukamilisha nilichokisema kwa kusema, mradi huu upo, utatekelezwa na fedha zitapatikana. Hiyo ni habari njema na niwatie moyo wananchi wa Njombe Mjini kwamba mradi tulioungojea kwa miaka sita, sasa unakwenda kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ombi. Mradi huu umechelewa sana, ulitakiwa uanze muda mrefu. Tunafahamu jitihada ambazo Mheshimiwa Waziri pamoja na Timu yake wamejitahidi kuondoa changamoto zote zilizokuwa zinakwamisha mradi huu. Tunafahamu na tunaelewa mchango mkubwa wa Mheshimiwa Rais katika kuukwamua mradi huu katika yale majadiliano na Serikali ya India. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa hapa kwamba kilichobaki ni Saini tu. Tuseme kweli, kwa wananchi jambo la kikwazo chochote hawaelewi, wanachotaka ni maji. Hata ukiwaambia kwamba Mkandarasi atakuja site wiki ijayo, hawaelewi, wanachotaka kuona ni maji.

Kwa hiyo, naomba lifanyiwe haraka, signing ifanyike kwa haraka na tumwombe Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyepo hapa aweze kuli-raise na Mheshimiwa Rais ili liweze kuangaliwa kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee mradi mwingine mkubwa ambao ulikuwa ni chechefu; mradi wa Igongwi wa Shilingi bilioni 4.5. Mradi huu ni wa maji ya mserereko. Namshukuru sana Waziri pamoja na Katibu Mkuu, kwani tulikuwa tumekata tamaa; ni mradi ambao utapita katika Kata tatu, katika Vijiji mbalimbali kama Kitulila, Kona, Danceland, Madobole, Lukonde, Njomlole na Majengo na unaishia kwenye Kijiji changu cha Uwemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana fedha zipatikane. Nime-check kwenye kitabu, fedha iliyotengwa ni kama Shilingi milioni 600. Tunafahamu kwamba Mkandarasi alishapewa kama Shilingi bilioni 1.6 katika mradi huu. Fedha ambazo zinahitajika bado ni Shilingi bilioni tatu ziweze kutekeleza. Huu ni mradi ambao utakuwa na matunda makubwa na matokeo makubwa kwa watu wengi kwa mufa mfupi ukitekelezwa. Naiomba sana Serikali itekeleze mradi huu kwa haraka, umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Njombe unakuwa kwa haraka na uko katika mchakato wa kuwa Manispaa. Moja ya mambo yanayochelewesha Mji wetu wa Njombe kuwa Manispaa ni kukosekana kwa majitaka. Mifumo ya majitaka hatuna mpaka leo. Nimefurahi kuona kwamba Mheshimiwa Waziri katika bajeti yake ameweka fedha kidogo ambazo zitatusaidia. Tunamshukuru sana kwa hilo, lakini naomba mradi huo na wenyewe utekelezwe kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumalizia kwa kuelezea jambo moja kwamba maendeleo yanakuja na changamoto nyingi. Mji wa Njombe unakua kwa haraka, mahitaji ya maji ni makubwa na yataendelea kuwa makubwa. Miradi hii iliyotajwa hapa itakwenda kumaliza hili tatizo na nina uhakika tutafikia kiwango ambacho Ilani ya Uchaguzi inatutaka tukifikie katika mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, changamoto kubwa ambayo tutaipata, watu wengi wamechangamkia jitihadi za kulima parachichi katika Mkoa wa Njombe na hasa Mji wa Njombe na Vijiji vinavyozunguka Njombe. Parachichi watu wanazidi kuigundua kwamba bila maji huwezi kuizalisha kwa tija. Kwa hiyo, huko mbele tunaona tatizo la mashindano ya kugombea maji. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Wizara hii ifanye coordination na Idara ya Umwagiliaji ili wanaotoa vibali kwa ajili ya umwagiliaji wa parachichi watoe wakitambua kwamba kuna watu wengi wanahitaji maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa kumalizia, wakulima wa parachichi walio wengi hawatoki Njombe tu, wanatoka karibu Tanzania nzima wanakwenda kulima parachichi Njombe. Wengine hawawi wakazi wa Njombe, interest yao kubwa ni wafanyabiashara walime parachichi, wapate, wanahitaji maji. Katika hali hiyo, tunahitaji kutunza vyanzo vyetu vya maji visiingiliwe. Tu-balance kati ya matumizi ya maji kwa ajili ya wakulima wa parachichi pamoja na matumizi ya maji kwa ajili ya wananchi walio wengi ambao ni wakazi wa Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niwapongeze sana watendaji wote wa RUWASA pamoja na NJUWASA wa Njombe pamoja na Ma-Director General na hasa Injinia Kyauri wa NJUWASA na Injinia Malisa. Tunawashukuru sana kwa kunipa ushirikiano wa kuwatia moyo na kuwafikisha wananchi wa Njombe kule ambako wanakutegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)