Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kukushukuru kunipatia fursa hii ya kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya hasa za kuwaletea maendeleo wananchi wetu katika Mkoa wa Kagera na hususan Wilaya ya Muleba. Kusema kweli wananchi wa Muleba wanampongeza sana na tunaomba salamu hizo zimfikie popote alipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake nzima; Naibu Waziri, dada yangu Maryprisca, alitembelea pale Muleba akajionea mahitaji makubwa ya maji wananchi wa Muleba waliyonayo. Pia nawashukuru Watendaji wa Wizara hii, kwa kweli mnafanya kazi nzuri, mnatupa ushirikiano mkubwa na ndiyo chanzo cha mafanikio ya Wizara hii. Tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru watendaji wa MURUWASA Mkoa wa Kagera na Muleba. MURUWASA pale Muleba mwaka huu wamekuwa watu wa nne kati ya Mamlaka Ndogo za Miji Midogo ambao wamefanya vizuri, ambayo inatolewa na EWURA. Kwa kweli wanastahili pongezi kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi wetu. Naomba Mheshimiwa Waziri hawa uwe unawaangalia mara nyingi sana. Wanaofanya vizuri hata kwenye bajeti yako uwe unawaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mheshimiwa Waziri, Muleba ametupatia karibu Shilingi milioni 328 kwa ajili ya kupanua mradi wa maji wa Wilaya ya Muleba. Pamoja na hizo fedha ambazo ametupatia, bado hazitoshi. Vile vile tunashukuru kwa kazi kubwa inayoendelea, na miradi inayoendelea katika Wilaya ya Muleba. Tuna mradi wa Maji Kata ya Buganguzi, tunaishukuru Serikali; tuna mradi wa maji Kishanda, Bureza, Gwanseli, Kasharunga, Kyebitembe, Kagoma, Rutenge na Ngenge. Kwa kweli tunashukuru kwa kazi kubwa inayoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa Mheshimiwa Waziri, hii kazi ambayo imeanza isije ikafika katikati tukaanza kusuasua au tukaanza kukimbizana. Tunajua kazi mnayoendelea nayo ni kubwa na tunaomba sasa hii kazi ambayo imeanza iendelee kama kauli ya Mheshimiwa Rais kwamba kazi iendelee. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri kwa miradi tuliyonayo Muleba isije ikaanza kusuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru kwa miradi mipya ambayo tutaietekeleza mwaka kesho tunawashukuru. Hata hivyo, ukitembelea Wilaya ya Muleba, tuna ukanda wa juu ambao kwetu tunaita Mgongo; lakini tuna ukanda wa chini Muleba Magharibi, hiyo ukanda wa chini wana matatizo makubwa sana ya maji. Kata za Kyemitembe, Kasharunga, Mbunda, Burungula, Ngenge, Butoro, kwa kweli Mheshimiwa Waziri chonde chonde tunakuomba, Kata zile zina matatizo makubwa sana ya maji. Katika miradi ambayo inatekelezwa, hakuna hata mradi mmoja ambao upo kwenye zile kata za ukanda wa chini ambazo zina matatizo makubwa sana ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri, endapo mtapata fedha kidogo nje ya bajeti, tunakuomba Mheshimiwa Waziri hiyo fedha ielekeze kwenye hizi Kata na wenyewe wakafurahie matunda ya Serikali ambayo inaongozwa na Mama yetu, mpendwa wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Watakushukuru sana na wataishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wilaya ya Muleba tuna visiwa 39 na tuna Kata tano ambazo zipo katikati ya ziwa, katikati ya maji mengi, lakini hazina maji safi na salama. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri na watendaji wako, hizi kata ambazo ziko visiwani zile huwa zinasahaulika kwa mambo mengi sana. Wana matatizo ya umeme, maji na wana matatizo ya kila kitu. Tunakuomba, Kata za namna hii ambazo kweli zimetengwa kijiografia, zimetengwa sijui na nini, lakini tuzipe faraja kwa kuzingalia kwa jicho la pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya Kata sita. Nimeuliza maswali ya nyongeza hapa Bungeni, na niliwahi kuleta swali la msingi na mara zote nimekuwa nikijibiwa kuwa, “Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huo mradi usanifu umekamilika na huu mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwa ajili ya kata sita za Wilaya ya Muleba ambazo ni Kata za Gwanseli, Magatakarutanga, Muleba Mjini, Buleza, Kikuku na Kagoma.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi ulianza kusanifiwa tangu mwaka 2009. Leo nilitegemea niukute kwenye bajeti, nimesoma vitabu vyote, hakuna kitu. Mwaka 2000 usanifu ulikamilika na nikaambiwa kwamba utakuwa kwenye bajeti ya mwaka huu. Kwa masikitiko makubwa; na nikuombe Mheshimiwa Waziri, hebu tuangalie. Wilaya ya Muleba ni Kati ya Wilaya ambazo zina matatizo na changamoto kubwa ya maji, ingawa tupo karibu na ziwa. Sisi tupo karibu na Ziwa, lakini hatuna maji. Ni mambo ya aibu. Najua kwa kazi na speed mnayoenda nayo na kwa mapenzi makubwa ya mama yetu, Rais wetu. Mheshimiwa Waziri ukija kuhitimisha hoja yako kesho, hebu tuambie, huu mradi unaanza kutekelezwa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua mnapata fedha nyingine, sehemu nyingine Mheshimiwa Waziri. Hebu tuangalie watu wa Muleba, tunawapenda sana na tuna matumaini na mapenzi makubwa sana na Serikali yetu. Tunakuomba huu mradi wa maji wa kata sita za Wilaya ya Muleba kutoka Ziwa Victoria uanze kutekelezwa sasa. Ni muda mrefu sana tumesemea haya mambo, tunaomba hili suala la kuja kuongea kila mwaka, kila siku, lipate suluhisho na hitimisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru sana kwa kazi ambazo zimefanyika. Kwetu wanasema, “Usiposhukuru kwa kidogo hata kile kikubwa hutakipata.” Mwisho, kuna tatizo la bei za maji. Ukiangalia miradi ambayo iko chini ya Mamlaka za Miji Mikubwa na Miji Midogo, ukilinganisha na hii miradi ambayo ipo chini ya RUWASA, kuna tofauti kubwa sana ya bei. Jana nilikuwa naongea na mtaalam wetu mmoja, nikamwuliza, kwa nini?

Mheshimiwa Spika, pale kwangu Muleba bei ya MURUWASA, Mamlaka ya Mji Mdogo; unit moja wanauza kati ya shilingi 800 mpaka shilingi 1,200 kulingana na matumizi; lakini nikienda kijijini kwangu, Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja pale akamtua mama ndoo, unit moja tunanunua kwa shilingi 2,500. Ukiangalia tofauti na pengo lililopo kati ya kipato kwa watu waliopo mjini na vijijini, vise versa nadhani ingekuwa applicable. Kwa watu vijijini kulingana na kipato chao kidogo tulitegemea bei ya maji iwe kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, tutafute namna nzuri ya ku-train hizi Kamati zetu za Maji hasa Makatibu wa hizi Jumuiya za Watumia Maji ili waweze kupunguza matumizi. Hayo matumizi yakishapunguzwa yawe reflected kwenye bei ya unit moja kwa watumiaji kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie tunapeleka fedha nyingi sana vijijini kwenye miradi ya maji, lakini hatuna watendaji ambao tumewaandaa kwa ajili ya kuhudumia wananchi kule vijijini, hasa kuunganisha maji. Matokeo yake tumeishia kupigwa fedha. Tunachukua mtu tumemwokotezea pale, unamweka pale akusanye fedha, wakati mwingine anakimbia hata na zile fedha. Tutafuta namna bora na sahihi ambayo itatusaidia kule vijijini kuhakikisha kwamba hii miradi tunayoijenga iwe endelevu na iweze kutumika kwa vizazi vyetu na vizazi vijavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)