Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Assa Nelson Makanika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara ya Maji ambayo ni muhimu sana, Wizara ambayo haina mbadala hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimwia Mwenyekiti, pili namshukuru kaka yangu Aweso kwa kazi kubwa sana ambayo anaifanya. Kama Waziri kijana anatufundisha namna ya kutenda na sisi vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha tatu namshukuru Mheshimiwa Rais, ametoa Shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya miradi ya maji jimboni kwetu. Kwa kweli hii ni hatua kubwa sana. Pasi na kuchukua muda sana nitajielekeza kwenye mambo makuu mawili ambayo ndiyo itakuwa msingi kabisa wa hoja yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni namna gani ambavyo nimeona ya kwamba Wizara hii kaka yangu Aweso inatengewa fedha nyingi sana na zinakwenda huko majimboni kwetu, lakini ufanisi wa fedha hizo ni mdogo sana. Nitakupa mfano halisi wa kwa Jimbo letu la Kigoma Kaskazini, tuna miradi zaidi ya tisa, na mwaka huu umeipatia fedha miradi hiyo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tuna mradi wa Mkigo. Kata ya Mkigo umetupatia Shilingi milioni 986, tunashukuru sana, na Kata ya Nyarubanda na Mradi wa Kalinzi umetupa Shilingi milioni 387. Hizo nazo tunashukuru sana, na hata bajeti iliyopita ulikuwa umeshatupatia fedha. Ukiangalia huu mradi wa Kalinzi umeshapeleka Shilingi milioni 900 na mradi umekwisha, lakini mradi unatoa maji yenye matope. Hakuna ufanisi wa ile fedha ya kwanza ambayo umeipeleka na sasa umeongeza fedha. Tunashukuru, ni kweli tunakwenda kutatua tatizo hili kwa kuweka Solar, lakini nakuomba sana huko chini ushuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimeona ulichokifanya kimenifurahisha, huku Watendaji wako watasema maji yapo na kwenye makaratasi wanakuonesha ufanisi mkubwa sana, lakini kwa wananchi ukienda hauoni ule ufanisi wa fedha uliyoitoa. Kwa hiyo, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri uweze kuona, hali ya mradi wa Mkongoroani unafahamu nimefika ofisini kwako mara nyingi, tumesaidiwa na Kampuni ya Enabel na Serikali imeweka nguvu yake humo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi unahudumia Vijiji Saba, kuna Kijiji cha Mkongoro, Kijiji cha Nyabigufa, Bitare, Nyamuhoza, Mkwanga na Kizenga. Mradi huu fedha imeshatolewa asilimia robo tatu yake, lakini ufanisi wake ukienda maji yanatoka mara moja kwa wiki hii haitupi afya sisi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri uweze kupita, tuna miradi mingi ya Mwandiga, Mungonya, miradi ya Matendosamwa na hii miradi ya Kidahwe. Miradi yote hii unatoa fedha vizuri sana lakini moja ya jambo ambalo ningeomba niishauri Wizara yako, kitu cha kwanza kabisa katika hii miradi, jambo la manunuzi limekuwa ni tatizo kubwa sana huko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano mmoja suala la manunuzi liko kwenye ngazi ya Mkoa lakini ukiangalia mradi wa Mungonya umekwishatoa Shilingi Milioni 412 na zimeshatoka zote. Ukiongea na Meneja wa Wilaya anakuambia changamoto ni viungo vinne kuja kuunganisha kwenye vijiji viwili vipate maji, ameweza kuagiza vile viungo viweze kununuliwa amekwenda Mkoani anasema watu wa manunuzi walichanganya. Mpaka sasa havionekani ni mwaka mzima watu hawapati maji kisa tu viungo viwili vya Shilingi Milioni Mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya manunuzi inaleta shida sana, ningeomba sana nimesikia mnataka kuipeleka kwenye ngazi ya Kikanda itasumbua zaidi. Mimi ninashauri badala ya ngazi ya Mkoa ambayo inaleta changamoto ni vema tungeshusha ngazi ya Wilaya kwenye hali ya manunuzi ili Wilaya ikiona kuna changamoto iweze kuchukua hatua haraka kuliko kusubiri iende ngazi ya Mkoa. Hilo jambo naomba ulitazame sana ili liweze kuleta ufanisi zaidi wa miradi hii ambayo unatoa fedha lakini haiwezi kukamilika kwa wakati na hata ikikamilika hakuna ufanisi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuna hali ambayo umeiona katika Bunge hili, Wabunge wapo walionyanyuka wakapongeza wapo Wabunge wamekupigia makofi kwa sana na Wabunge wengine umeona hapa kama Wabunge wa Mtwara wanalia kwa machozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma ni sehemu ya hilo jambo, Kigoma tunashindwa kuelewa kuna changamoto gani, Kigoma na Rukwa, Kigoma na Katavi tunashindwa kuelewa kuna changamoto gani?

Mheshimiwa Waziri wewe ni msomi, unakwenda unachukua maji kutoka Mwanza na Wabunge wa Mwanza wamekupongeza yanafika mpaka Dodoma kilomita 687 lakini pale Kigoma nina Ziwa kilomita tano watu wanalia maji, just five kilometers! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda hata vijiji vingine nusu kilometer hakuna maji, mfano Kijiji cha Kiziba kwa nini isifike hatua kama mnaweza mkapeleka shilingi bilioni 500 kule Arusha, mimi ni mjumbe wa Kamati ya PIC tumekwenda Arusha, tunaona jinsi ambavyo mnaweka miradi mikubwa kwa nini msiifikirie na Kigoma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma tuna vyanzo vingi ukiacha Ziwa tu hata hii Mito. Mto Malagarasi una mwinuko mzuri tu, ukichukua Mto Malagarasi sehemu moja unapeleka kabisa kwenda kuhudumia Wilaya ya Kibondo na unahudumia Kasulu ule utakaohudumia Kasulu unashuka mpaka Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana tunaomba sana wazee wa Kigoma inafika mahali wanajiuliza iko shida gani? Sisi tuwe na ziwa hapo mlangoni kwetu, wengine hawana hata ziwa, leo hii wanapongeza na sisi tutapongeza endapo mtaweza kututazama. Lazima Dodoma wapongeze kama mnatoa maji kilometer 687 wanaachaje kupongeza? Sisi Kigoma tunasema nini tuwekeeni mradi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano tu wa hii miradi mnayotupa ni kweli inakuja kutatua matatizo ya maji lakini sio endelevu. Mfano mmoja ni thabiti mwaka 2020 tumekwenda Wilaya ya Kibondo, Waziri Mkuu amekwenda kutembelea mradi mmoja mradi wa Shilingi Bilioni Sita lakini mpaka dakika ya sasa unatoa maji kwa kusuasua, hizo fedha pelekeni kwenye chanzo cha kuaminika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupeni mradi ambao unatoa maji kwenye chanzo cha kuaminika ili nasi Bunge lijalo tuje tupige makofi, tufanane sawa na wa Mwanza, tufanane sawa na wa sehemu zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo machache naomba sana Kaka yangu Mheshimiwa Aweso uweze kukaa chini ujifikirie, ufikirie sana una msemo wako mzuri sana “wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani” lakini Kigoma punje ni mbili kwenye sahani. Sasa hatuuoni huo wali wa kushiba, tunaomba sana na sisi uweze kutujazia wali wa kushiba kwenye sahani ili Kigoma tuone fahari yako wewe kuwa Waziri.(Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga hoja mkono. (Makofi)