Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hii mada ya maji kwa sababu maji ni uhai, maji ni ibada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Juma Aweso. Kwa kweli ana haki ya kupongezwa ana haki ya kufanyiwa kila kitu kwa sababu, Aweso amekuwa ni msikivu hata katika Kamati yetu ya Maji, Mheshimiwa Aweso tukienda kumuona sisi Wabunge wenzie amekuwa na msaada mkubwa, kwa hiyo tuna haki ya kukusifia. Pia tumsifie Naibu Waziri amekuwa ni mama ambaye anafanyakazi vizuri sana, anatuwakilisha vizuri sana katika miradi ya maji ni Engineer ambaye kwa kweli anajituma sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe hongera nyingi sana Katibu wetu Mkuu Kaka yetu Sanga ambae amekuwa akifanyakazi kubwa, Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni mama amekuwa akifanyakazi nzuri sana katika Wizara ya Maji. Niwapongeze wafanyakazi wote wa maji wanasema wao ni ndugu na ndio maana wanaelewana wanafanyakazi vizuri hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema kwamba Mheshimiwa Aweso anafanyakazi vizuri, leo ametuletea mawifi wawili kwa kweli tena jasiri hasa na tumeamini kwamba umetulia, umetulizwa na unafanyakazi vizuri kwa sababu wale wakina mama ni jasiri sana na tumewaona kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitoe pongezi zangu nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia. Mama Samia amefanyakazi nzuri sana kuhakikisha kwamba fedha nyingi zinaelekezwa kwenye miradi ya maji, fedha za UVIKO zinaelekezwa pia kwenye miradi ya maji na sasa hivi tunaamini kabisa tunakwenda kumtua mwanamke ndoo kichwani. Kumtua ndoo mwanamke kichwani tunataka maji yafike mpaka pale alipo nyumbani kwake siyo tunayafuata kilomita 10 au tuyafuate kwenye Kata hapana, tunaomba Mheshimiwa Aweso uangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi nyingi sana kwa Mkurugenzi wa RUWASA na yeye maji vijijini kwa kweli inafanyakazi yake vizuri sana, hongera sana. Lakini naomba pia nimpongeze Mkurugenzi wetu wa IRUWASA Iringa na yeye amekuwa akitusaidia sana katika miradi yetu ya Iringa, anafanyakazi nzuri sana. Lakini siwezi kumsahau Meneja wa RUWASA ambaye ni Engineer Joyce Bahati huyu ni mama jasiri na yeye amekuwa na ushirikiano mzuri, pamoja na Meneja wake wa Wilaya zote za Mkoa wa Iringa, wamekuwa na ushirikiano mkubwa sana kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe katika Kamati ya Maji kwa kweli tumefanya ziara yetu katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, tumeenda kuona miradi mizuri, miradi mikubwa sana, naomba nitoe pongezi kubwa sana kwa Mkurugenzi wa DAWASA ambaye miradi ile mingine ilikuwa imeshindikana muda mrefu, lakini sasa hivi miradi inafanyakazi vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa Diwani Dar es Salaam kulikuwa kuna changamoto kubwa sana ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini sasa hivi maji yanapatikana ila changamoto yake sasa ni usambazaji wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Iringa pia ulikuwa na miradi sita, miradi ambayo ilikuwa kila siku ukienda kwenye ziara akina mama wanalalamika maji hakuna, ile miradi ni chechefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya Izazi, Mnadani, Fyome, Magunga Wilaya ya Iringa DC, pia kulikuwa na miradi ya Sawala, Mtwango, Ikiziminzowo na Ukami katika Wilaya ya Mufindi, miradi hiyo tuna imani sasa hivi imeanza kufanyiwa kazi na tuna imani sasa akina mama tunaenda kuwatua ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi ambayo tayari inatoa maji natoa pongezi, leo hii niseme miradi ambayo inatoa maji kumpongeza Meneja wa RUWASA pamoja na IRUWASA, ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana pamoja na Mama Samia ambaye ametuletea fedha nyingi katika Mkoa wetu wa Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi kama Ruaha Mbuyuni, Msosa, Mgowelo, Kitelewasi na Lundamatwe, Image, Mawambala na Vitono hii miradi iko katika Wilaya ya Kilolo. Lakini kuna mradi wa Ikweha, Ihigo, Lulanda, Kusonga, Idumika, Uhambi, Lingetu, Nyololo katika Wilaya ya Mufindi, pia tuna miradi kama Mafuruto, Ndiwili, Kilamambo, Mkumbwanyi katika Wilaya ya Iringa DC. Tuna kila haki kwa kweli ya kuwashukuru sana wenzetu wa RUWASA na IRUWASA katika Mkoa wetu wa Iringa hasa Engineer Joyce siku zote umekuwa na sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kuna changamoto ambazo tumekuwa tukizikuta katika miradi hii ya maji, kwanza kabisa TRA kutokutoa vibali vya msamaha vya kodi kwa hiyo inasababisha hii miradi mingi sana kucheleweshwa. Sasa naomba Serikali iangalie hawa TRA vibali vipatikane kwa wakati hii miradi iweze kukamilika kwa wakati, lakini tulivyokwenda pale Dar es Salaam tulikuta wafanyakazi wengi sana ni vibarua au wanafanyakazi kwa mikataba walioajiriwa ni wachache sana. Mimi naomba Serikali waamini hizi mamlaka waweze kuajiri, kuna ngazi ndogo sana kwa nini wasiwaajiri wenyewe? Kwa sababu kwanza kabisa kuna miradi mingine inatekelezwa kwa fedha yao wenyewe ambayo wameikusanya. Sasa kuwaajiri wafanyakazi hawa wachache ni vizuri sana kuliko kusubiri kibali kutoka kwenye Wizara ya Utumishi inasababisha changamoto nyingi sana hata kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri, kwamba maji yanapatikana kwa mfano hata huko kwetu Iringa kuna mito kuna kila kitu lakini tuna miradi mikubwa katika kila maeneo, tatizo ni fedha ya usambazaji wa yale maji, unakuta wanawake bado wanahangaika wakati tunasoma hapa tumepewa miradi mikubwa ya maji lakini fedha ya kusambazia maji inacheleweshwa sana. Kwa hiyo, niombe Wizara ihakikishe kwamba sasa hivi inatenga fedha nyingi kwa ile miradi ambayo imekamilika ili maji yaweze kusambazwa katika vijiji vyote ambavyo vinatakiwa kupatiwa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna changamoto ya mradi unaweza Kijiji kingine kikarukwa halafu sehemu ile kuna ufugaji kwa hiyo unakuta miundombinu inatobolewa watu wanatoboa lile bomba ili either mifugo wapate maji au wao wapate maji. Kwa hiyo, naomba pia wakati wanasambaza haya maji wahakikishe kwamba kila Kijiji kinapatiwa maji ili kusiwepo na uharibifu wa miundombinu ambayo inasambaza hayo maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba kuwepo na program ya uvunaji wa maji kwa sababu, tunaona kwamba tumekuwa na maji mengi ya mvua ambayo yamekuwa yakiharibu barabara, tukiwa na program ya kuvuna maji hasa katika mashule, katika vituo vya afya, katika nyumba zetu itasaidia hata watoto wetu watakuwa na mazingira mazuri, watakuwa wanatengeneza maua kwa sababu maji yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba niunge mkono hoja nakushukuru sana. (Makofi)