Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima. Niwashukuru sana pia wananchi wangu wa Jimbo la Nkasi Kaskazini kwa mapito magumu ambayo kaka yangu Aweso anayajua vizuri. Pamoja na changamoto hizo ambazo zinaendelea nikupongeze pia waziri kwa jitihada zako binafsi, lakini pamoja na timu yako, namna ambavyo mnakuwa watu wa kusiliza Wabunge wenzenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana viongozi wangu wa maji kuanzia mkoa mpaka wilaya namna ambavyo wanajitahidi kwa namna ambavyo wanaweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza namna ambavyo fedha inapotea zaidi kwenye kutafuta vyanzo vya maji. Wilaya ya Nkasi ni miongoni mwa wilaya ambazo kuanzia mbunge wa kwanza nchi ilipopata uhuru jambo la kuzungumza mara nyingi ndani ya Bunge ni maji mpaka mimi nazungumza leo maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda ni mchache nitakwenda kwenye mapendekezo. Pamoja na kwamba kuna miradi ambayo inaendelea kwenye Wilaya ya Nkasi. Tuna mradi wa Kabwe ambao umeshakamilika wa bilioni 1.7, tuna mradi wa Isale ambao ni kichefuchefu mpaka leo, leo ni mara ya tano nazungumza kwa bilioni 5.5, tuna mradi wa Katongolo wa milioni 349, tuna mradi wa Namanyere wa bilioni 1.9 ambao na wewe umekuja kulipa hiyo fedha mwezi Disemba mwaka jana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini nasema fedha nyingi zinapotea pamoja nah ii Miradi ninayoizungumza bado haiwezi kumaliza changamoto ya maji hata robo kwa changamoto iliyopo kwa Wilaya ya Nkasi. Kwanini fedha nyingi inatumikaa kwenda kutafuta vyanzo wakati chanzo kipo? Hili ni tatizo kubwa kwenye Wizara hii ya maji fedha inayotengwa ni jambo moja, fedha inayokwenda ni jambo jingine lakini miradi ambayo inakwenda kuanzishwa na kukamilika ni jambo lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushauri Mheshimiwa Waziri; pamoja na wataalamu waku walioenda darasani ni vizuri wanapokwenda kutafuta vyanzo jambo hili likawa ni shirikishi kwa watu wa eneo husika. Nimezungumza mara kadhaa hapa kwamba Mkoa wa Rukwa sisi kipaumbele chetu hatuitaji maneno mengine tunahitaji maji kutoka Ziwa Tanganyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo linahitaji miujiza gani? Linahitaji uthubutu wa viongozi mlioko madarakani. Kama kutoka Kilando kuja na manyele ambapo kuna Kata tano ni kilomita 64, hesabu walizopiga kugawanya tu maji kuyatoa pale ni kama bilioni 70 mpaka 100. Hizi fedha zote ambazo mmekuwa mnatenga kama kweli jambo ni kuthubutu tu kwanini mmeshindwa kutoa maji ziwa Tanganyika mnazidi kupoteza fedha kutafuta vyanzo ilhali chanzo kipo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana hiki ulichokiandika hapa, kwamba mnakwenda kutumia maziwa makuu lakini nikiona bajeti yako uliyopewa napata changamoto na utekelezaji wa hiki unachokizungumza. Bajeti ni ndogo sana na hamuwezi kutumia maziwa makuu kwa hii bajeti iliyopo. Niombe Serikali kama kauli mbiu ya Rais wetu akiwa Makamu wa Rais ni kumtua mama ndoo kichani twende nayo kwa vitendo kwa kuipa Wizara ya Maji kipaumbele kwa kwenda kutatua changamoto za maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wana Nkasi wameniagiza, kama unafikiri ni gharama kubwa kwenda kuchukua yale maji, kwa kuwa chanzo kipo, ina maana tumeshaepusha tayari fedha ya kutafuta chanzo, tunazungumzi habari ya ku-treat maji na kuyapeleka kwa wananchi. Wananchi wanasema wa Nkasi wako tayari kuanza leo kuchimba mtaro wenyewe kwa mikono mpaka Kilami. Naomba na wewe kama mtoto ambaye unajua maumivu anayopitia mwanamke hii lugha ni ngumu sana nimeona na mimi nikufikishie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini najiuliza, mbona kuna maeneo yana miradi ambayo ni ya milioni 600, bilioni 500, Rukwa tuna bahati mbaya gani? Hiyo bilioni 100 au 70 leo tunazungumza Habari ya maji? Wananchi wa Kata ya Kipundu walikusimamisha pale ulivyokuja. vilevile wananchi wa Kata za Namanyere, Isumta, Mkomolo pamoja na Mtenga! Yaani unashangaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niseme kati ya maajabu ya dunia ya Tanzania kuna maajabu mengine. Yaani Kata ya Kipili ninapofanya mkutano mimi ukigeuka likipiga wimbi kubwa maji yanakuja kunigusa mpaka mimi lakini wananchi hawana maji ya kutumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji nini? Mungu ametupa maji kilichokosekana ni uthubutu wa viongozi mliopo kama maji yapo yanaonekana kuyapandisha kufikisha kwa wananchi kuna shida gani? Na hili jambo, kwa sababu ya muda unavyokwenda haraka zaidi, naomba nizungumze fedha ambazo zinatumika kwenye upotevu wa maji. Tunapima maji ambayo yanazalishwa na maji ambayo yanawafikia wananchi, maji kwa utaratibu wa kawaida yakipotea asilimia 20 tunajua yanapotea kwenye vyonzo mbalimbali aidha miundombinu na vitu vingine lakini kwa Tanzania ni asilimia 35 ya upotevu wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa ya EWURA ya Machi, 2022, walizalisha maji milioni 322, lakini maji yaliyopotea ni mita za ujazo milioni 113.5 sawa na asilimia 36.8. Ukipeleka kwenye fedha inamaana fedha ambazo walikusanya ni bilioni 484.2 zilizopotea ni bilioni 178.9. Kwa hiyo kama ni mradi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika na kuzambaza Mkoa wa Rukwa mngesambaza na fedha ikabaki, lakini inapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri nilazima fedha itengwe kwa ajili ya kuboresha miundombinu yam aji kuepusha upotevu wa maji ili fedha hiyo ambayo inapotea iende kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tujue vigezo vinavyotumika kupeleka miradi ya kimkakati kwenye haya maeneo. Mkoa wa Rukwa tuko kwenye miji 28, lakini Ziwa Tanganyika tunalo na nyie mnasema gharama ni kubwa, bilioni 70 mnasema gharama ni kubwa, lakini kuna maeneo yanapata zaidi ya hiyo fedha, lakini maji yanapotea kwa gharama nyingi zaidi ya fedha. Tunaomba kwa kuwa ulifika na ukaona na unasema mara nyingi hatuitaji kauli tunahitaji maji. Ahsante.