Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nichukue nafasi hii nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameweza kutupa afya kuweza kuingia hapa Bungeni tuweze kujadili mambo ya Kitaifa, mambo ya maendeleo ya wananchi wa nchi yetu ya Tanzania na kwenye Majimbo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi kwanza niseme kwamba naunga mkono hoja Wizara hii. Vilevile nimpongeze Rais wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya katika nchi yetu na katika majimbo yetu. Pia nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na Katibu Mkuu na wote wanaoendelea kumsaidia kwenye Wizara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nijikite katika maeneo ambayo fedha zimekuja na zimeweza kutatua matatizo katika Jimbo langu. Zimekuja milioni 645 katika Vijiji vya Mwakizega na Kabeba; huu Mradi ulikuwa umekwama kwa muda mrefu. Imekuja milioni 43 kwa Kijiji cha Sunuka kwa ajili ya ujenzi wa tenki la maji lita 150,000. Pia imekuja milioni 992 kwa ajili ya Vijiji vya Sigunga na Kangwena Mkandarasi amepelekwa pale tarehe 07 mwezi huu wa Tano. Lakini pia 1,600,000,000.00 kwa ajili ya Vijiji vya Herembe pamja na Kaparamsenga. Mradi huu bado unafanyiwa vetting.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia milioni 281 kwenda Kijiji cha Mdabazi kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati huu Mradi ni wa muda mrefu lakini ulikuwa kidogo hautoi maji lakini mpaka leo nilikuwa naongea na Diwani bado kuna shida kidogo. Lakini kuna milioni 281 ambayo imetengwa kwa ajili ya kufanya ukarabari. Milioni 450 ni kwa ajili ya Kijiji cha Kashaguru. Pia milioni 495 Vijiji vya Mlela na Kandaga. Mkandarasi yupo site; ingawa fedha ilichelewa kufika lakini juzi niliambiwa wamelipwa na wanaendelea na Mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, milioni 650 kwa ajili ya Kijiji cha Malagarasi Mkandarasi yupo anaendelea. Milioni 87 kwa ajili Vijiji vya Basanza na Msebeyi hivi sasa gari za kuchimba visima viwili ziko pale kwa ajili ya Basanza na Msebeyi. Milioni 132 Kijiji cha Rukoma ukarabati, huu Mradi ni wa mwaka 2012, ni mradi wa muda mrefu sana. Ulikwama kwa sababu ya ubadhirifu wa wale wanaopewa kazi ya kutengeneza mradi huu, lakini nashukuru kwamba hii milioni 132 tayari hata nilikuwa naongea na Mwenyekiti leo wa Kijiji kuna baadhi ya sehemu maji yameanza kutoka. Hata hivyo kwenye tenki lenyewe yalikuwa hata hayafiki lakini Mwenyekiti amethibitishia Kijiji kwamba maji yanaingia kwenye tenki na limejaa; kwa bado sasa namna ya kuepeleka maji kwenye magati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili kwa kweli inasikitisha sana kwa sababu tangu mwaka 2012 ni muda mrefu sana ni miaka 10 wananchi wanasubiri maji na fedha imepelekwa pale. Yaani unaweza kuona jinsi ambavyo watendaji wanavyoichonganisha Serikali na wananchi, kabisa, haipendezi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba tukimaliza Bunge hili twenda ukaone kabisa wananchi watafurahi sana na mimi nitafurahi sana, mimi naomba niende na wewe mwenyewe Waziri kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia 2,400,000,000.00 Kijiji cha Kaziromimba Mradi uko pale lakini bahati mbaya sana Kijiji kile, Mheshimiwa Waziri jambo la kusikitisha sana, naomba unisikilize. Kuna tenki ambalo liliagizwa kwa ajili ya Mradi ule liko Bandarini sasa hivi ni mwezi wa tatu. Wananchi wanajiuliza hivi lile tenki ambalo tuliahidiwa kwamba linakuja, limetoka nje ya nchi limekuja mpaka Bandarini mbona bado liko pale Bandarini? Na mimi Mheshimiwa Waziri nataka nikwambie kabisa pamoja na kwamba nimekushukuru na kukupongeza lakini kwenye eneo hili nakusudia kushika shilingi yako kama hukutoa maelezo mazuri ni lini tenki hili litatoka Dar es Salaam Bandarini kwenda pale Kazuramimba ili wananchi wakazi wanaokaribia kufika 48,000 waweze kufaidi maji. Lakini pia katika eneo la Kijiji cha Uvinza ambacho ndiyo chenye jina ambalo kimebeba Makao Makuu ya Wilaya. Kijiji kile Mheshimiwa Makamu wa Rais juzi juzi alisimamishwa pale wakalalamika kwamba Kijiji kile hakina maji, lakini mimi nilivyofuatilia ni kweli kijiji kina maji, lakini Vitongoji vyake ndiyo bado havijapelekewa maji. Na hili Mheshimiwa Makamu wa Rais alinipigia simu kunipa taarifa kwamba Mbunge angalia kwa nini wananchi wa Uvinza wanalalamika maji. Maji yapo lakini kwenye maeneo ya Vitongoji ndiyo maji hayajafika. Lakini pia pale Makao Makuu ya Halmashauri bado kuna shida ya mtandao wa maji mradi wa maji pale bado kuna shida, ni kizungurumkuti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Nguruka, Mradi ule ulikamilika vizuri lakini bahati mbaya sana haufanyi kazi vizuri na wananchi wameshindwa kuupokea kwa maana ya matumizi kwa sababu ule mradi chanzo chake kwa maana ya pump inatumia mafuta ya petrol.
Kwa hiyo sasa unaweza ukaona kwamba gharama ni kubwa mimi nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Waziri kwenye chanzo kile cha maji basi kwa kuwa umeme haujafika basi tuweke miundombinu ya solar ili wananchi waweze kufaidi maji ambayo kidogo yatakuwa na nafuu pale Nguruka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Nguruka imebeba Kata mbili, kwa maana ya Kata ya Nguruka yenyewe na Kata ya Itebula, kwa hiyo unaweza ukaona kwamba Mradi huu ni mradi mzuri sana na umeshakamilika lakini wananchi wameshindwa ku-afford bei kwa sababu ya mafuta ile pump inayosukuma yale mafuta. Lakini pia ninajua utatuletea fedha mwaka huu wa fedha lakini bado kuna Vijiji vingi sana havijapata maji kwa mfano Vijiji vya Kata ya Mgabo vyote vitano havijapata maji, Kata ya Mtego wa Noti vyote havijapata maji Nachakulu haijapata maji ni Vijiji vingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi nilikuwa nadhani katika eneo hili wengi wamesema na mimi naomba niseme lakini nashukuru kwamba kwenye Hotuba yako umeongea vizuri kwamba unakusudia kutumia vyanzo vya maji yanayotokana na Ziwa ili yaweze kusaidia kwenye maeneo hayo. Kwa mfano Ziwa Tanganyika ni chanzo kizuri cha maji kwa nini kisitumike hiki? Wabunge wengi wamelalamika ametoka kuzungumza Mbunge mwenzangu wa Sumbawanga kule, lakini Wabunge….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Bidyanguze, muda wako umekwisha.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: … kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri katika eneo hili chanzo cha Ziwa Tanganyika kiweze kutumika. Ahsante sana, naunga mkono hoja.