Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karatu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Bajeti ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Spika, awali nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu na wenzake wote Wizarani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme katika Jimbo la Karatu tuna changamoto; na bahati nzuri sana Naibu Waziri alifika katika Jimbo la Karatu. Lakini vilevile Waziri alifika takribani miezi mitatu. Mwezi wa pili alifika katika Jimbo la Karatu. Lakini pale Karatu maji yanapatikana kwa asilimia 33 katika taasisi ya Serikali. Lakini kuna taasisi binafsi ambazo upatikanaji wa maji unapatikana kwa asilimia 25.
Mheshimiwa Spika, shida kubwa katika Jimbo ka Karatu ni bei kubwa ya maji. Bei ya maji Karatu kwa unit moja inapatikana kwa Shilingi 3,500. Katika taasisi ya Serikali inapatikana kwa Shilingi 1,750. Lakini Mheshimiwa Waziri alifika katika Jimbo lile na akasema ndani ya siku 30 bei hii inaweza na ikawa uwiano. Hili haihitaji hela ya Serikali, inahitaji kauli ya Waziri kusema bei iuzwe kwa bei fulani katika Jimbo la Karatu. Na mimi siombi niongezewe fedha, mimi ninachohitaji ni kauli ya Waziri kusema bei ya maji ambayo inatokana na maelekezo ya EWURA katika Jimbo la Karatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, alisema jambo hili lingechukua ndani ya siku 30 lakini takribani leo ni miezi mitatu na siku tano. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, hii pia ni sehemu unapofuatilia, unapozunguka nchi hii maamuzi magumu unapofanya maeneo mengine. Sijajua kwa nini Karatu inashindikana bei ile kuwa ya aina moja; kwa sababu kuna wengine wanauza kwa Shilingi 3,500, wengine wanauza kwa Shilingi 1,750. Na ulifika katika Jimbo la Karatu ukasema hata hao wa chini wanaouza Shilingi 1,750 bado wanawaibia wananchi wa Jimbo la Karatu.
Mheshimiwa Spika, napenda sana uweze kutoa kauli katika Jimbo la Karatu, wananchi wale waweze kupata fursa ya kuweza kupata kulingana na bei katika maeneo mengine katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naamini ukiwa katika Jimbo la Karatu ulisema kwamba uliweza kushusha bei ya hapa Dodoma, kama sikosei ilikuwa Shilingi 1,200 au Shilingi 1,300 kwa unit na Arusha na maeneo mengine yaliyoko ndani ya nchi hii mpaka Dar es Salaam. Naamini hilo kwako wewe si kitu kigumu, unaweza kulifanyia kazi kwa muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo lile kuna mradi ambao unaendelea, naamini Serikali ilitoa fedha za kutosha Shilingi zaidi ya Milioni 800. Lakini kuna eneo la Ayalabee limetoa Shilingi Milioni 800 na kuna eneo la Bwawani limetoa zaidi ya Shilingi Milioni 400, lakini mradi ule unahitaji kama zaidi ya Shilingi Milioni 700. Lakini na katika eneo hili la Ayalabee imefika mradi asilimia kama zaidi ya 80 lakini mradi wa Bwawani asilimi ni 34. Asilimia hizi zote 80 zikikamilika asilimia 100 na ile asilimia 34 ikikamilika asilimia 100 tunaweza kupata zaidi ya asilimia 70 katika Mji wa Karatu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri najua alitembelea maeneo mengi katika Jimbo la Karatu wakati umetembelea mwezi wa pili. Tulifika Bonde la Easi ambako upatikanaji wa maji ni wa asilimia zaidi ya 60. Lakini vilevile tulifika katika katika maeneo mengine katika Jimbo la Karatu, upatikanaji wa maji haujazidi asilimia zaidi ya 60 katika maeneo mengi.
Mheshimiwa Spika, ombi langu kwake, na kipindi kile wakati umetembelea Jimbo la Karatu ulituahidi sisi wananchi wa Jimbo la Karatu. Ulisema upatikanaji wa maji Karatu ili shida hii iishee kabisa ilionekana kwamba tunahitaji zaidi ya Shilingi Bilioni 4.5. Na mimi naamini katika Serikali na Wabunge wengi wamesimama katika ukumbi huu kwamba kuna maeneo mengine wapeleke Shilingi Bilioni 10, kuna maeneo mengine wapeleke Shilingi Bilioni 15; na mimi naomba katika eneo hili la Karatu tuweze kupata Shilingi Bilioni 4.5 na Mheshimiwa Waziri uliahidi katika Jimbo la Karatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na uliahidi wananchi wa Jimbo la Karatu kwamba Shilingi Bilioni 4.5 kwa Serikali si kitu kikubwa sana na ulisema Serikali haifanyi biashara. Kazi kubwa ya Serikali ni kutoa huduma na wananchi wa Karatu walikunukuu vizuri. Na mimi nikuombe umekuja Karatu na wananchi wa Karatu wamekusikiliza vizuri na wamekuelewa vizuri. Nakuomba sana usinitengenezee ajari katika Jimbo lile tuweze kupata huduma ili wananchi wale waendelee kuniamini Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kwamba tumepata katika maeneo kata mbalimbali katika Jimbo la Karatu. Kwa mfano; katika eneo hili la Mang’ola Juu tumepata Shilingi Milioni 191, Kata ya Daa lakini pale Kata ya Kansay tumeweza kupata Shilingi Milioni 225. Vilevile mradi mwingine katika eneo la Mang’ola Balasani tumepata Shilingi Milioni 360. Kuna eneo lingine Kata ya Rotya tumeweza kupata Shilingi milioni zaidi ya 360. Maeneo mengine ya Barai tumeweza kupata Shilingi Milioni 360.
Mheshimiwa Spika, kazi imefanyika na sisi tunashukuru sana Wizara. Nami pia kama Mbunge wa Jimbo wakati naingia kama Mbunge wa Jimbo lile fedha ilikuwa ya Wizara ya Maji kidogo ni changamoto lakini tangu mwaka jana, mwaka huu fedha katika Jimbo lile imepatikana kwa asilimia kubwa. Hata katika hizo hela za UVIKO - 19 tumeweza kupata shilingi milioni 500 na mradi unaendelea na unasambaa katika Mji wa Karatu kwa zaidi ya kilometa 45. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, kwamba sasa tumesambaza ule mradi kwa eneo la mabomba tu kwa kilometa 45 ili maji yale yasambae vizuri nahitaji mradi ule ukamilike ambao unahitaji zaidi ya shilingi milioni 800. Na sasa imeshatolewa kama shilingi milioni 600. Kinachohitajika pale ni shilingi milioni 250 na eneo hili la Bwawani hela zimeshaenda zaidi ya shilingi milioni 300. Kinachohitajika pale zaidi ya shilingi milioni 300 ili iweze kufikia shilingi milioni 700. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nakuomba hili kwako siyo kubwa na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Chama cha Mapinduzi naamini siyo kitu kikubwa. Naomba, eneo hili likikamilika katika Jimbo la Karatu tutakuwa tumesogea sana katika eneo hili la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba kazi imefanyika, tunashukuru kwa hili ambalo limefanyika na japo naamini katika mwaka huu wa fedha miradi mingi ile ya mwaka jana wanaimalizia. Naamini hii miradi mkimalizia tutapata maji, kwa sababu katika Jimbo la Karatu kuna changamoto kubwa. Kuna miradi mingine ilikuwa ya miaka zaidi ya nane, saba ilikuwa imemelala lakini baada ya Waziri kuingia na Serikali ya Awamu ya Sita kuingia miradi mingi imefufuliwa na wananchi wetu wanaendelea kupata maji katika eneo la Jimbo la Karatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi na pia naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)