Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kunipa nafasi kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Mheshimiwa Aweso kwa kule Mwanza sisi wewe ni bado green guard tu, lakini maskini wa Mungu sasa umezeeka, yani unaota upara kwa ajili ya maji, lakini Mungu atakulipa. Dada yangu, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mungu atawalipa; kazi ya maji ni sadaka. Msione Wabunge humu ndani wanalia maji, Mheshimiwa Rais yeye mwenye anajua kabisa kazi anayokuja kufanya ni sadaka kwa wananchi wa Tanzania na Mwenyezi Mungu atamlipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kwetu katika Mkoa wa Mwanza hakuna mahali popote ambapo haufanyiki mradi wa maji. Magu kuna mradi mkubwa wa zaidi ya mabilioni, ambao unakamilika sasa hivi; Misungwi kuna mradi wa bilioni 45; sasa hivi hapa tunapiga hesabu mradi wa Majimbo ya Sumve na Kwimba pekee yake tu wana bilioni 41; Sengerema mimi hapa sasa hivi katika miradi iliopo kuna mradi mkubwa wa bilioni 21 na sasa hivi kuna mradi wa bilioni 17, huyu mama tunataka tumpe nini? Na bado anahikikisha tena tunapata mitambo 25 kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi ninachoshauri tu ni kwamba hii mitambo Mheshimiwa Waziri Aweso muhakikishe wataaalam wanaokwenda kuihudumia mitambo hii tusije tukashindwa kufika 2025 hatujamaliza kero ya maji kwa nchi hii; hakuna mtu ambaye atakosa maji. Hawa wanaosema wanakosa maji kutoka Ziwa Victoria kuna mitambo itachimba.

Mheshimiwa Spika, na mimi ninachotaka kukuambia ni kwamba badala ya kuigawa hii mitambo kwa mikoa, iende kwenye kanda ili tufanya kazi kwa pamoja. Wilaya moja inaweza ikashambuliwa na mitambo mitatu au minne ionekane kazi ya Mheshimiwa Rais. Haya ndiyo maono yake, yaonekane kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hakuna mbadala wa maji kama unavyosema. Na hii Wizara yako mara nyingi nakusikia unasema siyo Wizara ya ukame, na mama ameshatuhakikishia kwamba suala la maji katika nchi hii litakuwa historia. Waheshimiwa Wabunge, kubalini mipango Mheshimiwa Rais anayoifanya sasa hivi kupitia Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Aweso, ushauri wangu ni kwamba kwa kutumia magari haya ambayo uyatumia sasa hivi kuendelea na safari, kutembea nchi nzima unaweza ukachoka kuifikia miradi yote kuikagua. Sasa hivi duniani watu wanakwenda katika mabadiliko. Gharama za kutumia helikopta Watanzania wanatakiwa waambiwe; kutumia helikopta ni gharama ndogo sana, mafuta lita 400 ukitoka na jet kutoka Dar es salaam unaweza ukakagua miradi 10 mpaka kufika Sengerema.

Mheshimiwa Spika, mnashindwaje idara kama hii, Wizara ya Maji mna miradi mikubwa ya mabilioni, kutoa pesa bilioni moja na nusu mkanunue helikopta. Na unakagua miradi yote kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nimekuona juzi unaangalia bwawa unadaganywa bwawa lilikuwa hapa; bwawa linaweza likapotea? Hawa watu wengi wanakuwa sio waadilifu. Sasa unakuja kuambiwa kwamba mara paipu zilipaa. Paipu zinaweza kupaa namna gani zimechimbiwa chini? Sasa hii yote ni kwa sababu unachelewa kufika katika yale maeneo. Jitahidi Mheshimiwa Aweso, wewe ni mdogo wangu, na Mwenyezi Mungu atakulinda na sisi tunakuombea dua.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wenzangu, ninachotaka kuwaambia ni kwamba kazi ya kusimamia miradi hii ya Serikali siyo mchezo. Hii miradi ya maji ni mingi sana katika nchi hii. Tuwe waadilifu, sisi wenyewe Wabunge twende tuka-visit hii miradi, tusisubiri kuja kulaumu ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, tuchukuwe majukumu yetu. Wabunge tuchukukuwe majukumu yetu jamani, tuhakikishe tunamsaidia Waziri kutoa taarifa. Na bahati nzuri ile Wizara yake nimekwenda kule mara nne, unafika unapewa chai unapewa na korosho. Juzi nilipewa korosho nikashangaa mimi, nimekwenda na shida ya maji nikapewa korosho na kukaribishwa chai, nikapewa na maji ya kunywa.

Mheshimiwa Spika, miradi ya ma-tank Sengerema, nakushukuru sana. Umeweka tank Sengerema lita milioni 5; siyo mchezo. Tunaweka kwenye chanzo cha Nyamazugo, Nyamkurukano kuna lita kama milioni mbili; haya maji yaliyoko Sengerema yanaweza yakatosha kuilisha Geita, Boshosa na kila mahali tukamaliza miradi ya maji.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Aweso, karibu Sengerema, dada yangu karibu Sengerema, mmekuja mmeona ile hali iliyopo, endeleeni kuwa waadilifu na Mwenyezi Mungu atawalinda.

Mheshimiwa Spika, Katibu Mkuu Sanga, najua unafanya kazi kwa niaba ya nchi. Unatoka hapo DUWASA, mimi nakukuta pale mpaka saa sita za usiku, mimi nipo jirani pale Sanga, Mwenyezi Mungu atakulipa. Hii kazi ni ya sadaka, wananchi wanakuona wala usiwe na wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wakati mwingine hawa watu wawe wanapewa hata zawadi hapa Bungeni kwa kazi wanayoifanya ya maji. Lakini Mheshimiwa Rais tumuombee kwa Mwenyezi Mungu; Wabunge hapa tumuombee, kazi ya maji siyo mchezo katika nchi hii. Tusiwe tunalaumu tu muda wote.

Mheshimiwa Spika, nchi hii ni kubwa, hii nchi siyo ndogo kama Burundi au Rwanda hapana. Kuna wananchi zaidi ya milioni 60 wote wanataka maji; siyo mchezo. Mheshimiwa Aweso, endelea tu kutusikiliza hivyo hivyo, lakini tunalia kwako na miradi yetu iweze kwenda. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)