Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buchosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mungu kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge hili nikiwa mtu wa kwanza kutoa mchango wangu kwa Taifa langu kuhusu idara hii ya afya.
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninampongeza sana kwa niaba ya Watanzania kwa uamuzi wa kuongeza mishahara kwa asilimia 23.3. Nchi nzima imejaa shangwe kwa sababu ya jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi naomba nianze kwanza kwa kusema maneno yafuatayo: -
Mheshimiwa Spika, mwaka 2001 nchi za Afrika zilikutana kule Abuja-Nigeria na wakafikia uamuzi wa kwamba bajeti ya Taifa lolote la Afrika Marehemu Mzee Mkapa alikuwa pale ni lazima asilimia 15 ya bajeti ilielekezwe kwenye huduma za afya. Jambo hili halijaweza kutimia 2019 tulikuwa na asilimia Saba, Mwaka 2020 tulikuwa na asilimia 6.7 na ninavyotazama naona kama tunaendelea kushuka. Sasa mimi nilikuwa ninaushauri mmoja kabla sijaanza ni kwamba naomba Serikali yangu ifikirie kuongeza bajeti kwenye afya kwa sababu afya ya Mtanzania ni kitu cha muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la preventive medicine, suala la kuzuia magonjwa yasitokee, tumefanya kazi kubwa sana kama Taifa kutibu watu, tumefanya kazi kubwa sana kuwatibu watu wetu wanapougua lakini hatujawekeza kiasi kikubwa sana kwenye suala la kuzuia magonjwa yasitokee. Katika suala la kuzuia magonjwa yasitokee nitajikita moja kwa moja kwenye chanjo ya homa ya ini na homa ya ini yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 mimi na wenzangu katika Kampuni ya Global Publisher tuliamua kufanya kampeni nchi nzima kuwaelimisha watu kuhusiana na ugonjwa wa Homa ya Ini. Kilichotufanya tufanye kampeni ile ilikuwa ni data zilizokuwepo za Homa ya Ini zilitushtua, zilitutisha na tukaona kwamba ilikuwa sababu ya mimi na wenzangu kutoa mchango kwa nchi yetu ili kuweza kusaidia watu waweze kupata ufahamu.
Mheshimiwa Spika, wakati huo 2014 katika akina mama waliofanyiwa uchunguzi wa afya wajawazito asilimia tano ya akina mama wote walikuwa wanakutwa na Homa ya Ini. Damu iliyotolewa kwenye benki ya damu hapo Dar es Salaam na sehemu mbalimbali chupa 100 zilizochukuliwa chupa nne zilikutwa na homa ya ini na uwepo wa homa ya ini katika nchi ulikuwa ni asilimia tano data zile zilitutisha tukaanza kampeni ile, tumefanya kampeni kwa muda tu, wakati ule Waziri wa Afya alikuwa Rais wa Zanzibar sasa hivi Mheshimiwa Hussein Ally Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Mheshimiwa Said Meck Sadiki, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Dada yangu Grace Magembe na Meya wa Ilala alikuwa Mdogo wangu Mheshimiwa Jerry Silaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumefanya kampeni ile kwa muda mfupi nikaitwa nikaambiwa Eric kampeni yako ni nzuri lakini tunaomba uiache kwanza inasababisha hofu inaleta taharuki watu wanaogopa, tukakubali kuacha kampeni ile kwa shingo upande. Miaka nane baadaye nikiwa naongea leo naomba nikusomee data za homa ya ini nchini Tanzania. Kwa wajawazito 100 wanaopimwa leo kwenye antenatal clinic zetu asilimia Saba mpaka Nane wanakutwa na homa ya ini, imeongezeka. Benki ya damu wanapotoa damu watu 100 chupa sita zinakutwa na homa ya ini.
Mheshimiwa Spika, rate ya homa ya ini, uwepo wa homa ya ini kwenye Taifa letu sasa hivi ni asilimia mpaka 7.2 katika baadhi ya maeneo. Hii inatisha, hili siyo jambo la kukalia kimya, wala siyo jambo la kuacha kuliongelea.
Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa leo kuongea nikiamini ya kwamba tuna uwezo wa kuzuia ugonjwa huu, tuna uwezo wa kuokoa maisha ya watu wetu kwa sababu chanjo ipo na mimi nafahamu Waheshimiwa Wabunge humu ndani mnaonisikiliza wengi mmechanjwa kwa sababu chanjo ililetwa hapa hapa Bungeni, lakini huko nje watu wetu wanashindwa kuimudu hii chanjo, kwa bei ya Serikali ni Shilingi 10,000 kwa chanjo moja mtu anahitaji chanjo tatu na kabla hajachanjwa lazima afanyiwe rapid test kuona kama ameambukizwa au hapana Shilingi Elfu Arobaini, Elfu Arobaini ni nyingi kwa mwananchi wa kawaida. Wananchi wanauliza kama chanjo ya COVID tumechanjwa bure kwa nini chanjo ya homa ya ini tunaombwa pesa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wanakufa, maisha ya watu yanapotea, watu wengi wameambukizwa. Hapa ndani mnaonisikiliza kama haujafiwa, kama humjui mtu aliyekufa basi wewe mwenyewe jipeleleze. Ugonjwa huu unazidi kuenea, kasi ya kuenea ni mara 100 zaidi ya UKIMWI. Tuna sababu ya kuchukua hatua kuokoa maisha ya watu wetu. Tuna kila sababu ya kuchukua hatua kuokoa maisha ya watu wetu, watu wanakufa. Hatuwezi kunyamaza, hatuwezi kujifanya hatuoni, lazima tuchukue hatua tuokoe maisha ya watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuko hapa Bungeni Waheshimiwa Wabunge kwa ajili ya watu waliotuchagua. Tuko hapa Bungeni kama hatuwezi kutetea maisha ya watu wetu waishi hatuna sababu ya kuwa Wabunge. Najiuliza kila siku kwanini hatuchanji? Kuna mtu akaniambia nchi yetu ni maskini na hatuna uwezo. Nikakataa, nikamwambia ukiniambia nchi ni maskini niletee report ya CAG nitakuonesha fedha zinapotelea wapi. Mabilioni ya fedha yanapotea mikononi mwa watu wasiokuwa waaminifu. Tungeokoa fedha zetu kwenye report ya CAG katika nchi hii tungeweza kuwachanja watu wetu wote na chenji ikabaki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiachana na hilo, naomba niongee jambo moja la msingi sana na bahati nzuri wataalam wako hapa wananisikiliza. Umuhimu wa kumchanja mtu badala ya kumtibu ni jambo la maana mno. Kansa ya Ini, the Hepatocellular Carcinoma gharama ya kumtibu hapa Tanzania ni Shilingi Milioni 16 mtu mmoja. (Makofi)
SPIKA: Sekunde 30 malizia.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, sasa kama gharama ya kumtibu mtu mmoja hapa Tanzania ni Shilingi Milioni 15 mwenye Kansa ya Ini inayosababishwa na Homa ya Ini. Ni kwanini tusiwachanje watu kuokoa maisha yao? Fedha zipo, tuwachanjeni watu wetu tuweze kuokoa maisha yao. (Makofi)
SPIKA: Haya ahsante sana. Ahsante sana.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)