Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Wizara hii nyeti, Wizara ya Afya. Kwanza kabisa nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia afya njema lakini pia kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nipende kumpongeza Mheshimwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha wananchi wetu wa Tanzania wanakuwa na afya njema ili waweze kutimiza majukumu yao.
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Waziri, Ndugu yetu na rafiki yetu, anafanyakazi kubwa sana kuhakikisha wizara hii inafanyakazi nzuri sana kwa wananchi wa Tanzania waweze kuwa na afya njema lakini niishukuru wizara nzima Naibu Waziri, Katibu Mkuu lakini na watendaji wote wa Wizara.
Mheshimiwa Spika, Kanda ya Ziwa tumekuwa na tatizo kubwa sana na changamoto kubwa ya kansa ya kizazi kwa sisi wanawake. Nimesimama kwenye Bunge lako kuongea tatizo hili kwasababu tumekuwa na changamoto hii wanawake wengi tumekumbwa sana na tatizo hili la kansa ya kizazi hasa Kanda ya Ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2021 wanawake 36,224 waliofanyiwa uchunguzi wa kansa ya kizazi waliokutwa na dalili za kansa ya kizazi walikuwa ni wanawake 1,597 na wanawake 252 walidhaniwa kuwa na vimelea vya kansa ya kizazi, wanawake 66 walikutwa tayari na ugonjwa wa kansa. Hii inaumiza sana ukizingatia sisi ni wanawake na ukizingatia ndio tunaotegemewa katika nchi yetu na katika majukumu makubwa ya familia zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu kubwa kwa Wizara ya Afya ni kutoa elimu kuanzia kwa mabinti zetu mpaka kwetu sisi akina mama ili kuweza kuelewa ni kwasababu gani tatizo hili limekuwa kubwa sana katika Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, leo hii ukienda Bugando kuna wagonjwa wengi sana wa kansa ya kizazi. Ukienda Ocean Road imejaa wagonjwa wengi sana wanaotoka Kanda ya Ziwa. Hii inaumiza sana, ukizingatia na sisi ni wanawake na Mheshimiwa wetu Waziri wa Afya ni mwanamke mwezetu. Ombi langu ni kuomba sana elimu itolewe kuanzia mashuleni kwa mabinti zetu na hata kwa akina mama ambao watakuwa wanakwenda kliniki hata wanaokwenda hospitali waweze kujua tatizo hili linapatikana vipi lakini pia linatibika vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekuwa ni nchi ya nne kwa tatizo kubwa la kansa ya kizazi. Tanzania inaongoza kuwa ni nchi ya nne. Kati ya wanawake 100, wanawake 59 wanakufa na kansa ya kizazi nchini kote; na Tanzania ikiwa ni nchi ya nne, hii inaumiza sana na inaumiza kwasababu ni wanawake wengi wanaopoteza maisha kutokana na tatizo hili kubwa. Niombe sana wizara hii iweze kuangalia kwa jicho la tatu tatizo hili kwa wanawake limekuwa ni sugu na linatuangamiza sana sisi wanawake, elimu itolewe sana kwa mabinti zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo hili nchi yetu ya Tanzania inaongoza kwa vifo vya kansa ambavyo tuna aina tano za kansa katika nchi yetu ya Tanzania. Ukiacha kansa ya kizazi ya wanawake tuna kansa za ngozi, mkojo (kansa ya tezi dume), kichwa, shingo, koo na kinywa, pamoja kansa ya matiti. Magonjwa yote haya hayajatolewa elimu ya kutosha, hayafahamiki ni jinsi gani tunaweza kuyaepuka ili tuepukane na hili tatizo. Kwa hiyo, ombi langu kubwa kwa Serikali niombe sana iweze kutoa elimu kuanzia kwa mabinti zetu lakini pia iweze kuwafahamisha ni kwanini tatizo hili limekuwa sugu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, vifo hivi vinavyoangamiza wanawake wenzetu na mabinti zetu ni vingi sana. Inavyoonesha tatizo hili ni sugu katika nchi yetu wanawake wanaokufa kwa kansa ya kizazi ni wengi. Kama takwimu zinavyoonyesha, kati ya wanawake 100,000 wanawake 59 wanakufa kwa kansa ya kizazi… (Makofi)
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Furaha Matondo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Agnes Marwa.
T A A R I F A
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, natoa taarifa kwa muongeaji kwamba kutokana tatizo hili kubwa ndiyo maana Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali Maalum ya Taifa kwaajili ya wanawake na watoto ikiwemo suala la hili la kansa kwa wanawake.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Furaha Matondo.
FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ninaipokea, lakini ninaomba sana elimu itolewe, na hasa chanjo kwa mabinti zetu zipatikane. Kwasababu tatizo hili ni kubwa nasilakufumbia macho. Vifo vya kansa ya kizazi vimekuwa ni tishio katika nchi yetu hasa kwa upande wa Kanda ya Ziwa. Ni vifo ambavyo vinaangamiza sana wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niombe sana Wizara iangalie tena kwa jicho la tatu.Tunaliongelea suala hili hapa lakini wengi hawana elimu na hawajui kwasababu gani wanapata matatizo kama haya. Wengi wanapata tatizo hili wanatoka wanakwenda kutibiwa kienyeji, na wengi wanakufa kwa kukosa elimu.
Mheshimiwa Spika, tulipata tatizo la HIV katika nchi yetu elimu ilitolewa mpaka mashuleni wakajua nini chanjo cha tatizo la HIV; iweje leo wanawake waangamie kwa kukosa elimu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu kubwa ni elimu kwa akina mama na vijana wetu. Chanjo hii kwa vijana inapatikana, kwanini vijana wetu hawapati chanjo? Niombe vijana wetu waweze kupatiwa chanjo hii ya kansa ya kizazi ili tuweze kuepukana na hii changamoto. Sisi akina mama tukimalizika kwa tatizo kama hili nchi yetu itaendeshwa na watu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa haya machache lakini naomba sana, Mheshimiwa Ummy amenielewa Waziri wetu naimani atakwenda kulifanyia kazi kubwa ni mwanamke mwenzetu anawatoto wa kike na anajua changamoto ni kubwa. Hoja yangu ninayomalizia ni elimu itolewe sana kwa vijana wetu…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)