Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbarali
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii. Awali ya yote ninaipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wote waandamizi ngazi ya taifa kwa kuendelea kutoa fedha nyingi katika miradi mbalimbali ya afya kwa Watanzania.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Godwin Oloyce Mollel, Katibu wa Wizara pamoja na Watendaji wote kwa usimamizi wao mahiri na Wizara inakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu leo nitajikita zaidi kuelezea uhaba wa rasilimaliwatu namna unavyoathiri uadilifu na ufanisi katika kazi. Kabla sijaingia kwenye mchango wangu niongelee kidogo kuhusu ajira. Nashukuru na kuipongeza Serikali kwa ajira hizi 10,285 lakini kwenye Kamati yetu tulishauri kwamba ajira hizi zizingatie usawa, haki na kijiografia pia kwa kuona kwamba mchakato mzima wa ajira zenyewe kwa kuwa ni mfumo basi angalau kila sehemu, kanda, iwe na waliochaguliwa. Sisi kama wawakilishi kwa kweli tumekuwa tukipigiwa simu nyingi na waliomba nasi kama sauti zao naomba kusisitiza hili kwamba, kwa kuwa wanaomba kwa mfumo labda Waziri aangalie namna ya kuunda Posts Selection Committee ambayo atachagua wataalam baadhi kutoka Wizarani na wengine kutoka hospitali mbalimbali ili kuhakiki kuona kwamba malengo yaliyowekwa yamefikiwa.
Mheshimiwa Spika, nina wasiwasi mifumo wakati mwingine inaweza kuwa tampered, badala ya kuchagua kama ilivyoainishwa kwenye mpango, idadi na aina za wale wanaochaguliwa ikawa tempered badala yake wakachaguliwa wa sehemu moja au ukanda moja na pengine wengi kupitia kanda moja kuliko nyingine kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili niendelee na mchango wangu kuhusu uhaba wa Rasilimaliwatu. Kwenye Kamati tumeshauri kwamba hawa watumishi wasimamiwe vizuri katika kuziba mapengo yaliyopo katika Idara mbalimbali. Lakini kukiwa na uhaba wa Rasilimaliwatu mara nyingi sana kama tulivyoona michango ya Waheshimiwa waliotangulia kwamba wengi wao kufuatana na maadili yao na viapo vyao siyo walalamishi wanavumilia, anazidiwa kufanyakazi lakini anajituma anaendelea kujitahidi kwa kadri ya uwezo alionao. Tofauti na sekta zingine kama walimu utaona athari zake moja kwa moja, amezidiwa wanafunzi wengi wanapiga kelele, hata akichoka anaweza akawapa assignment akaenda kunywa chai, akaenda kupumzika kidogo, lakini huyu wa Idara ya Afya hana nafasi hiyo, atajitahidi mpaka pale atakapotimiza kumaliza wagonjwa wote walio mbele yake.
Mheshimiwa Spika, kazi nyingi hazihitaji presha, hata kama ni kazi ndogo kiasi gani iwe ya kutafuta mshipa wa damu, kama ana presha ana haraka hiyo kazi badala ya kutumia dakika mbili atatumia nusu saa. Halikadhalika upasuaji mdogo na kadhalika, hivyo tunahitaji rasilimali watu ya kutosha ili wafanye kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, athari nyingine ni wale wagonjwa wanaosubiri watahisi kwamba huyu mtu labda hahudumiwi ili apewe rushwa, kumbe yule mtumishi amezidiwa. Sasa wanashawishika kutoa rushwa wakidhani kwamba wanacheleweshwa maksudi lakini kumbe ni uhaba wa rasilimaliwatu.
Mheshimiwa Spika, pia wapo wanaotumia nafasi hiyo kuchukua rushwa, kwamba atajifanya amezidiwa na kazi mpaka ndugu wa mgonjwa aende amuone atoe chochote ndipo amhudumie. Imetokea hospitali fulani ipo barabara sintaitaja hapa, na ni Hospitali ya Mkoa ya Rufaa. Kijana alipelekwa usiku pale anavuja damu, amevunjika mfupa unaonekana, hahudumiwi, ndugu wanaambiwa nendeni barabarani mkatafute Panadol na baadaye wale vijana wanashangaa wanaulizwa je, mna fedha zozote mtupatie? Kama hamtoi mgonjwa wenu atafariki, wanaambiwa waziwazi. Wale ndugu baada ya kushauriana ilibidi wamtoe mgonjwa usiku ule wakaondoka naye kwenda hospitali nyingine ambako walihudumiwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda unakwenda mbio, niongelee athari katika upimaji physical examination. Pale kuna takiwa wafanyakazi wa kutosha wa jinsi tofauti tofauti kwa sababu kuna hatari kama anayepima ni jinsi nyingine na ni peke yake, akamdhalilisha yule mgonjwa akamfanyia visivyo lakini kumbe wakiwa wengi basi atafanya kwa uhakika na bila matatizo yoyote wala wasiwasi kwa mgonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee Hospitali zetu za Rufaa. Sina shaka ngazi ya Taifa zinafanya vizuri, wabobezi wapo wengi, wanafanya kwa umakini, lakini hizi za Mikoa nina wasiwasi nazo huduma kwa kweli labda zichunguzwe ziitwe Rufaa zile zinazotoa huduma nzuri kabisa. Pamoja na ubobezi walionao lakini kama mtu anavuja damu anaambiwa akanunue Panadol halafu inaitwa Hospitali ya Rufaa kwa kweli hii inatia shaka sana. Wale wa Hospitali za Rufaa tulizotembelea kule Muhimbili, Taasisi ya Mifupa MOI na Taasisi ya Magonjwa ya Moyo, kwa kweli waliomba kwamba tunaomba tufikiriwe, tunaomba mtupigie kelele tuongezewe angalau tupate fedha zaidi kwa sababu tunajituma na kazi ni kubwa. Nami leo hapa natumia nafasi hii kuomba Wizara i- top up kwa kuwa Mkurugenzi kule alituambia kwamba yeye anatoa motisha kulingana na mapato ya ndani. Lakini Serikali, Wizara naomba i-top up kwa kweli kuwapongeza wale wanafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia zipo kazi ambazo zinatumia umakini zaidi. Kwa mfano, tulifika MSD tukakuta kijana amekaa pale muda wote ana-check kidonge kwa kidonge kwenye mizani, kina uzito gani, kina ugumu gani, kiko bora kiasi gani? Lakini tulivyotoka pale wanalalamika kwamba sisi hapa hatuna mgahawa. Sasa motisha ya aina hii kukosekana kwa watu wanaofanya very tedious work kwa kweli inakatisha tamaa na hawa wakati mwingine ndiyo wakuibua maovu yanayofanyika pale. Sasa wasipoangaliwa vizuri, wanahudumiwa vizuri hawatatoa taarifa yoyote na ni rahidi kurubuniwa wakapewa kitu kidogo mambo yakaenda hovyo. Mara nyingi wale wanaotoa siri, waadilifu wanapigwa vita.
Mheshimiwa Spika, tumefika Butimba tukakuta Muuguzi mmoja anasota pale Butimba kwa kosa dogo tu la kukosea kuingiza data kwenye mfumo, hasara ya Shilingi 8,000 imemuweka muuguzi yule Butimba, kwa kweli, inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa…
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja.(Makofi)