Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi pia nishukuru kwa ajili ya juhudi kubwa za Wizara ya Afya na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anaendelea kuimarisha afya katika Taifa letu. Nawashukuru kwa ajili ya Kituo cha Afya Mkimbizi ambapo mmetupatia Shilingi milioni 250 na baadaye mmeongeza tena Shilingi milioni 250 nawashukuru sana, kwa ajili ya Wodi zinazojengwa katika Hospitali ya Frelimo ya Wilaya pale mawili na ICU pamoja na Mochuari. Nawashukuru pia kwa utanuzi unaoendelea wa Hospitali yetu ya Mkoa wa Iringa ingawa tuna changamoto kubwa ya upungufu wa watumishi, maana tunahitaji kuwa na watumishi karibu 466 na tuna watumishi 266 tu na nyinyi mmeipangia ile kwa ajili ya huduma ichangie zaidi ya Shilingi Bilioni 5.8 kwa hiyo tunaomba tuongezewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba leo niongelee hoja ya afya ya akili. Mheshimiwa Waziri nimesoma katika mambo yako sijaona sana unaongelea suala la afya ya akili, lakini afya ya akili ni kitu cha muhimu sana na ni lazima kama nchi tuhakikishe kwamba tunakichukulia uzito mkubwa na kukiwekea mipango. Kwa sababu, suala la afya ya akili tunaposema mtu awe na afya ya akili maana yake kwanza awe na uwezo wa kujitambua. Mtu anaonesha ana uwezo wa kutatua changamoto zake, mtu anaweza kufanya kazi na kuzalisha lakini mtu huyo anaweza akatoa mchango kwenye jamii yake. Sasa ukitaka kujua mpo kiwango gani cha afya ya akili kama wananchi lazima mjielekeze kuangalia hoja hizo. Kwanza kabisa tukienda namna gani labda kama Watanzania tunachangia ukiona mara nyingi raia wanajiuliza, Serikali inatufanyia nini na sio wao wanataka kusema sisi tunaifanyia nini Serikali ujue kuna tatizo kubwa kwenye afya yao ya akili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wote wenye afya za akili wanajiuliza mimi nitaifanyia nini Tanzania na sio Tanzania itanifanyia nini. Sasa sisi mara nyingi tunatumia Technic ya walevi au ya watu wanaopenda kunywa mara nyingi wako baadhi yao, wakiwa na tatizo anaahirisha tatizo kwa kulewa halafu kesho anajua akiamka mambo yatakuwa safi. Lakini kiuhalisia haiwi hivyo kwa sababu akiamka kesho fedha ile, ambayo anatakiwa aanze kutatulia changamoto ameitumia yote imekwisha. Suala hili lipo kwetu inapotokea changamoto mara nyingi tunakimbilia kutaka Serikali ifanye jambo bila kuangalia sisi wenyewe tunakwendaje kutatua lile jambo. Uwezo wetu wa kutatua changamoto kama wananchi/viongozi inaonekana umeshinda na hiyo ndio ina- comprise afya ya akili mna afya ya aina gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juzi juzi ikishuka bei ya mazao tunataka Serikali iweke ruzuku ikishuka bei ya mbolea tunataka Serikali iweke ruzuku imepanda bei ya mafuta tunataka Serikali iweke ruzuku. Sasa mimi najiuliza ni kwa nini hatufikirii kutatua changamoto na siku nyingine kutumia akili walizotumia wazee wetu, yamkini akili zao zilikuwa zina afya wakasema tunapita kwenye kipindi cha vita ni wakati wa kujifunga mikanda tuhakikishe tunapambana ili tujenge uchumi. Mimi leo najiuliza ile Shilingi Bilioni 100 tunayoiweka huku haijatoka kwenye TARURA kweli hatutaanza kutembea kwenye barabara zina makorongo, hatutaanza kukosa dawa? Sasa Mheshimiwa Waziri wa Afya tuangalie sana kwenye suala la afya ya akili, unatusaidia vipi tuweze kutatua changamoto zetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kujitambua ni ukweli usiopingika Taifa lolote linalotegemea kuendelea kuwa na nguvu, linafanya uwekezaji mkubwa kwa vijana wake na tunaposema vijana hapa ni miaka 15 mpaka 35. Sasa tuangalie kama Taifa tunawekezaje kwa vijana wetu unapofika mahali unaona vijana wa miaka 35 hawapewi priority wakati nchi nyingine sasa hivi zinahama zinaelekea hata kumpa kijana mwenye miaka 27 kuwa Rais wa nchi. Lakini sisi kwenye nafasi tu za Umeneja kwenye nafasi tu za Uenyekiti wa Bodi, tunajaa wazee na tunakaa sisi tu wakina bibi hili Taifa ni Taifa ambalo litafika mwisho. Kwa sababu, kama unaendelea kuwekeza kwa wazee unaendelea kila siku kuhuisha mikataba watu wamestaafu unakazi ya kuhuisha mikataba wazee waendelee wazee waendelee, maana yake ni kwamba vijana wako utawatumia lini? Utawapa practice lini maana huo ndio udumavu wa akili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu udumavu wa akili ni kama unashindwa kuwa na adequate simulation ile Sy social simulation ukishindwa kuwa nayo ile ina maana unashindwa kuwandaa vijana wako wajipange. Kwa nini kwenye hizi nafasi kama Profesa ni bibi basi msaidizi wa Profesa awe kijana mdogo ili kumuandaa. Kwenye nafasi kubwa tunashika sawa wewe umeshika nafasi kubwa ni mtu aged kwa nini hufanyi succession plan ya kumuandaa kijana. Sasa Taifa letu litakuwa halina nguvu kama siku zote tutaendelea kufikiri kwamba wanaoweza kushika nafasi kubwa, ni watu wenye umri mkubwa na kusahau vijana na hilo ni tatizo la afya ya akili. Kutotambua kwamba wewe ni mzee utaondoka nchi unatakiwa umuachie kijana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri afya ya akili tunaiangalia sehemu nyingine sisi tunaweza tukaleta hoja kutoka huku chini lakini wenzetu mkikaa huko Wizarani mnatuona sisi kama... sisi tuko juu ndio wenyewe. Unaona sisi tuliwaambia ile Hospitali ya Mkoa wa Iringa mmeng’ang’ania kuitanua pale kwenye car seater pamejaa hata hapatanuliki mmebanwa na Magereza mmebanwa na Mahakama, pelekeni kwenye heka 35 kule mkaitanue vizuri nyinyi wenzetu mmekataa mmetuona sisi hatuna afya ya akili lakini kimsingi nyinyi ndio hamna afya ya akili. Kwa sababu, wewe unaweza kubadilisha Magereza iwe ICU kwa kuwaondoa Magereza pale? Nyinyi ndio hamna afya kwa hiyo sisi tunaomba muangalie. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Ummy hilo lisikupe taabu unafanya kazi vizuri mimi ninachoomba niletee Hospitali ya Wilaya ya Iringa, hujaiingiza hapa na uliniahidi kwamba basi tutakujengea Hospitali ya Wilaya lakini kwenye bajeti haipo mama yangu. Naomba kwa sababu sisi ile hospitali hatutibu watu wa Iringa tu na Majimbo yote yanayotuzunguka wanakuja pale, Isimani wanakuja, Kilolo wanakuja, kule kwa Kiswaga wanakuja, Kalenga na Mafinga wanakuja pale katikati tunaomba mtujengee hiyo hospitali yetu ya wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapoongelea afya ya akili angalia hali halisi ya performance ya Watanzania wetu. Leo hii unaweza kumuona mama amebeba begi zuri ukafikiri labda ndani ya begi mule sijui kuna nini lakini ukiangalia kuna maji ambayo amepewa sijui kwa Nabii gani yamletee magari, yamletee nyumba, yamletee utajiri, ana tango ameombewa sijui la kuimarisha ndoa, ana chumvi sijui ya kumwaga avute wateja, ana vitu kibao yaani vitu vinavyoonesha watu hawana afya ya akili. Wanadanganywa kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Afya hiki ni kitu cha msingi, tunaomba ukiweke kwenye bajeti yako utatusaidiaje Watanzania hawa wawe na afya wasidanganyike? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hakuna namna hata Mungu mwenyewe anasema nitabariki kazi ya mikono yako sio kwa kutembea na maji yaliyochotwa Jordan au maji yamechotwa Mto Meru sasa hili ni tatizo la afya ya akili. Hebu tuangalie afya za akili zetu wanasema afya ya akili ni kujitambua. Leo hii tuna vijana wengi wanaogopa kuoa wanaogopa kuolewa ukimuuliza wewe kwa nini huolewi anasema nipo nipo kwanza umri unakwenda, wewe kwa nini huoi nipo nipo kwanza. (Makofi)
Kosa la afya ya akili. Akili yake hai-reason sawasawa. Umri umefika, bado hajitambui. Sasa hiki kitu ni cha muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii afya ya akili tusipoishughulikia, ina tabia ya kuleta umasikini kwenye nchi, kwa sababu uwezo wa watu kuzalisha unapungua kwa sababu hawafikirii. Umenielewa? Leo nimekuja nikasema hapa jamani, wanaume hawa wanapendwa wakiwa na kitu (fedha), lakini kuna mwanaume mmoja anaitwa Heche, amelalamika kwa nini nimesema wanaume, sio warembo? Hilo ni tatizo la afya ya akili. Mimi siamini kama kuna mwanaume hapa atataka kuitwa mrembo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, afya za akili za watu haziko sawasawa, mtusaidie. Watu wanalalamika ndoa zinavunjika kwa sababu ya suala la afya ya akili. Tumepeleka mikopo akina mama wakope, leo anakopa FINCA, anaenda PRIDE, anaenda huku anaenda huku. Ndoa nyingi zinavunjika kwa kuwa watu wanakimbia kwa sababu ya mikopo. Hajui namna ya kuzalisha. Unaona! Kwa hiyo, anakosa afya ya akili nini? Ya akili! Kwa hiyo, inatuletea matatizo. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Jesca dakika zako zimeisha, lakini nakuongezea dakika moja, malizia mchango wako. (Makofi/Kicheko)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, naendelea. Kama tunafikiri kwamba umasikini wa nchi hii utaisha kwa sababu ya kutoza kodi, mama aliongea categorically, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatutaki kodi zenye dhuluma. Tunataka kodi kwa haki. Kama kuna kiongozi, bosi amekaa kwenye Ofisi ya TRA, anajua kabisa huyu mfanyabiashara uwezo wa kulipa hii kodi hana, halafu yeye anambambika kodi na kumtoza kodi kubwa, ni afya ya akili hana. Yeye mwenyewe analipwa kwa hiyo biashara, halafu anachagiza kuiua hiyo biashara. Ina maana mtu huyo hana afya ya akili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unapokwenda na nguvu kufunga biashara, badala ya kumwelimisha mtu kwamba hii biashara fanya hivi na hivi, au nipe mpango wako wa kulipa kodi; wewe kazi yako ni kufunga biashara na wakati umetumwa ukalate na kuongeza mapato ya Taifa hili, afya yako ya akili ina mgogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana na viongozi wetu, tupo kwenye idara na kwenye Serikali, bado tunaona kuna vitengo. Mimi niko Kamati ya Nishati, nashukuru sana. Sisi tuna Kitengo cha Geothermal. Geothermal ni umeme wa jotoardhi, wamejipanga vizuri kupitia Waziri wetu anawasimamia, yule mzee tumefika anatusomea taarifa kwamba mimi nastaafu, lakini nimemwandaa kijana huyu hapa, anakuja kuchukua hii nafasi. Zipo Wizara na wapo mabosi wengine wa Wizara hapa, bado wanafikiri kuendelea ku-renew mikataba kwa wazee na wamesha-renew mikataba mara sita, mara saba. Wakati una-renew mkataba mara tatu mara nne, tayari tuna workforce ambayo ni vijana wamesoma hatuwaandai, ni kutokuwa na afya ya akili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami naomba Mheshimiwa Ummy unapokuja hapa, useme hiyo afya ya akili unaiwekaje tupone?
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)