Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon Ally Juma Makoa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Afya. Nianze kwa kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayofanyika, lakini niwapongeze Wizara ya Afya kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mambo machache; jambo la kwanza, nimpongeze Dkt. Chandika ambaye ni Mkurugenzi wa Benjamini Mkapa, Hospitali yetu ambayo ipo hapa Mkoani, kwa kazi kubwa anazozifanya. Ombi langu kwa Wizara ni kwamba Hospitali yetu ya Benjamini Mkapa watu wote sisi Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali tunakwenda kupata huduma ya afya pale, kwa hiyo wajitahidi kama Wizara kuhakikisha hospitali ya Benjamini Mkapa inatoa huduma kwa kiwango kama vile Muhimbili ama zaidi ya hapo. Wapatiwe vifaa vya kutosha na vyenye sifa na hadhi kwa sababu Benjamini Mkapa sasa Serikali ndio ipo hapa na mikoa mingi ya jirani tunategemea kwenda huko kwa sababu ni karibu kuliko Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunaomba Serikali basi iiangalie hii hospitali kwa sababu sasa inatuhudumia wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naishukuru Serikali unakumbuka Bunge la Bajeti lililopita tuliongelea kesi za akinamama ambao walikuwa wanakufa kwa kukosa huduma za hospitali hasa kwenye Kata ya Suruke. Nilikwenda kwa Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye alikuwa Waziri wa TAMISEMI kumweleza ile hali mbaya ya akinamama ambao walikuwa wanakosa huduma kwa sababu wako kisiwani.

Mheshimiwa Spika, leo hii ninapoongea Serikali imekwishajenga kituo cha afya kikubwa cha kisasa na tayari kinakwenda kukamilika. Ombi langu sasa kwa Serikali, katika nia ile ile njema ya kuwasaidia akinamama wale, sasa tunaomba katika mgao huu wa ajira basi tupatiwe madaktari japo watano ili waweze kwenda kukihudumia kituo hicho cha afya, wale akinamama ambao walikosa huduma nzuri ya uzazi wakawa wanapoteza maisha na watoto wao, basi waweze kupata huduma. Kwa sababu Serikali imekwishawekeza fedha nyingi na kituo kilikwishakamilika, ni vema sasa basi Waziri, Mheshimiwa Ummy atupelekee Madaktari ili msimu huu wa mvua unapoanza wale akinamama ambao wanajifungua kipindi hicho wasipate tena shida ya kuzuiwa na mto, ukizingatia daraja la mto bubu linapelekwa litajengwa mwakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tuna kituo cha afya kilijengwa Awamu ya Tano. Kituo kile cha afya kinaitwa kituo cha afya lakini hakijakamilika majengo, tunahitaji kupata jengo la OPD, chumba cha x-ray, pamoja na wodi ya akinamama na akinababa. Kwa hiyo ili kikamilike kile kituo cha afya na kiwe na sifa ya kituo cha afya, basi tunaomba yale majengo yakamilike.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri au bahati mbaya katika bajeti hii sikuona kama nimepata kituo cha afya, lakini sasa kama watatusaidia tukakikamilisha kile kituo cha afya ambacho kilijengwa Awamu ya Tano nab ado hakijakamilika, watakuwa wamefanya jambo jema sana.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, tuna vituo vya afya, tuna hospitali zetu, tunamwomba Mheshimiwa Ummy hospitali hizi ziweze kupatiwa vifaa pamoja na watumishi ili wananchi waweze kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, nashukuru sana kwa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)