Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kadha wa kadha anazofanya kwa mustakabali wa Taifa letu. Napenda kumpongeza kwa jitihada za hivi karibuni za kuendelea kujali utumishi wa umma ambapo amegusa sekta zote ikiwemo sekta hii ya afya.
Mheshimiwa Spika, mwaka jana wakati wa maadhimisho ya sherehe za kitaifa za Mei Mosi, Mheshimiwa Rais alisema, mafanikio ya Taifa lolote hutokana na juhudi za wafanyakazi wake, yaani every nation owes its success to its labourers. Mheshimiwa Rais amedhihirisha maneno yake kwa matendo kwa kuwa mwaka jana alipunguza kodi ya mshahara kwa watumishi wa kima cha chini kutoka asilimia tisa hadi asilimia nane na kama haitoshi mwaka huu amewaongeza mshahara wa asilimia 23.3 pamoja na kada zingine za mshahara. Mheshimiwa Rais kwa mtindo huu anaendelea kuupiga mwingi kweli kweli na kwa kweli Watanzania watarajie makubwa zaidi kutoka kwa Rais wetu anayewapenda sana.
Mheshimiwa Spika, naomba kumpongeza Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu. Moyo wake wa dhati wa kuboresha sekta ya afya haujaanza leo. Tumeona jitihada zake nyingi za kuboresha sekta ya afya tangu alipoaminiwa kwa mara ya kwanza katika sekta hii. Mara zote amesimama kidete kupambania afya za Watanzania. Namuombea Mheshimiwa Waziri afya njema ili maono aliyonayo kwa sekta ya afya yatimie kwa mstakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, uviaji wa mimba ama utoaji wa mimba usio salama umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vifo vya kinamama wajawazito. Uviaji wa mimba ni utokaji wa mimba kabla ya wiki ya 28 ya ujauzito. Utokaji wa mimba unaweza kusababishwa na sababu ambazo sio za kukusudia ila kwa kiasi kikubwa ni kwa sababu zinazotokana na mimba zisizotarajiwa na hivyo kupelekea wengi kutoa mimba kwa watu wasio na ujuzi wa kitabibu na katika maeneo yasiyo salama kabisa.
Mheshimiwa Spika, duniani kote, utoaji wa mimba upo kwa kiasi cha milioni 56 kila mwaka ambapo katika utoaji huo, takribani wanawake milioni 25 wanafanya utoaji wa mimba usio salama. Kila mwaka kati ya wanawake hao wanaotoa mimba kwa njia zisizo salama asilimia 98 hutokea katika nchi zinazoendelea ambapo takribani milioni tatu ni watoto wa kike kati ya umri wa miaka 15 hadi 19 na takribani wanawake 47,000 wanafariki kila mwaka kutokana na utoaji huo wa mimba usio salama.
Mheshimiwa Spika, hapa kwetu Tanzania, takribani wanawake 405,000 wanatoa mimba kwa njia zisizo salama na asilimia 40 ya wanawake hupata madhara mbalimbali yanayotokana na utoaji wa mimba usio salama. Asilimia 18 ya wanawake hawa wanatoa mimba kwa madaktari walio na ujuzi stahiki, asilimia 31 wanatolewa na wauguzi ambao hawana ujuzi stahiki na asilimia 51 wanatoa kwa njia za kienyeji ikiwemo kunywa dawa kiholela kwa kushauriwa na wafamasia au kwa njia nyingine ambazo sio za kitabibu.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuwa tatizo hili limepelekea matatizo mbalimbali ya uzazi kwa wanawake ikiwemo ugumba na matatizo mengine sugu ya uzazi ningependa kushauri, elimu zaidi inahitajika juu ya utoaji wa mimba usio salama. Pamoja na elimu, uboreshwaji wa vitendea kazi na dawa stahiki zinahitajika katika vituo vya afya ili kusaidia madhara yanayotokana na utoaji wa mimba usio salama kwa sababu hatuwezi kusema tuache waathirike na matatizo hayo kisa tu ni jambo lisilo la kimaadili. Tuendelee kuwahimiza kuachana na utoaji mimba usio salama na uzazi salama lakini madhara yanapotokea tuwasaidie kwa kuweka dawa stahiki na vitendea kazi kwa sababu pamoja na yote wapo pia ambao wanapata matatizo ya kutoka kwa mimba bila kukusudi na wanahitaji kusafishwa ila sasa ili huduma zipatikane kwa urahisi ni vyema kuweka dawa na vitendea kazi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo naomba suala la Muswada wa Bima ya Afya kwa kadri Mheshimiwa Waziri alivyoeleza lifanyiwe kazi mapema ili Watanzania wengi wanufaike na huduma bora za afya.