Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya. Pia nimpongeze Waziri wa Afya pamoja na timu yake yote.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimshukuru Rais wetu kwa kutupa fedha kwa ajili ya kujenga jengo la mama na mtoto katika hospitali ya Wilaya ya Lushoto na pia tumepata shilingi 1,200,000,000 kwa ajili ya kujenga vituo vya afya kama ifuatavyo; Kituo cha Afya Mlola shilingi 700,000,000; Kituo cha Afya Ngwelo shilingi 250,000,000 na Kituo cha Afya Kwekanga shilingi 250,000,000.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuishukuru Serikali, bado kuna changamoto ya kujenga vituo vya afya katika maeneo yafuatayo; Kituo cha Afya gare; Kituo cha Afya Kwai Kwemakame na Kituo cha Afya Mdando Kata ya Makanya. Vituo vyote hivi nilivyotaja hapo juu wananchi wameshaanza kujenga na majengo yapo kwenye hatua mbalimbali. Kwa hiyo niiombe Serikali itenge fedha katika awamu hii ili kuunga juhudi za wananchi walizokwisha kuzianza.

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto ya upatikanaji wa dawa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Changamoto hii imekuwa ikiathiri sana wananchi wetu hasa kinamama wajawazito pamoja na Watoto. Kwa hiyo, naomba Serikali ichukue hatua za haraka ili kunusuru wananchi wetu wasiendelee kupoteza Maisha.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa ushauri kwa Serikali, kwa kuwa nchi yetu imejaaliwa na rasilimali ya miti ya dawa pamoja na mimea dawa, na katika nchi hii kuna Watanzania waliojaaliwa vipaji vya kujua miti dawa na mimea dawa, na kupitia miti hiyo wakajaaliwa kutibu magonjwa mengi ni yale yasioambukiza, na utafiti umeshafanyika na kubaini ya kuwa matabibu hao wana uwezo wa kutibu magonjwa yafuatayo; ugonjwa wa kisukari, pressure, vidonda vya tumbo, bawasili, figo stage zote, kansa stage zote, tezi dume stage zote na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, magonjwa yote niliyoorodhesha hapa tumeyathibitisha kwa kuwatibu wagonjwa na mpaka sasa hivi wagonjwa wote wanaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali kwa nini Serikali isitume wataalam wake kuwafuata matabibu hawa ili nao wajiridhishe ili Serikali ikijiridhisha iwasaidie matabibu hawa, kuwapa vitendea kazi vyote vinavyohitajika ili waweze kuzalisha dawa nyingi na ili Serikali ipunguze kuagiza dawa nyingi nje. Pia Serikali itaokoa fedha nyingi kuagiza dawa nje. Lakini pia kwa kuwa dawa zetu ni za miti yetu ya asili, kwa hiyo dawa zetu zitakuwa ni organic ambazo hazitakuwa na madhara yoyote kwenye mwili wa mwanadamu, na hii wazungu wakija kugundua ya kuwa dawa zetu ni organic, ni imani yetu kuwa Serikali yetu itaingiza fedha za kigeni, na pia dawa zetu zitakuwa zinachangia pato la Taifa. Sambamba na hayo wataalam wetu waziruhusu au wazisambaze katika hosptali zetu pamoja na kuzitangaza.

Mheshimiwa Spika, hili sio la kupuuzwa, ikiwezekana wataalam wetu wafanye ufuatiliaji wa haraka ili tiba asili iweze kuwa miongoni mwa sekta inayochangia pato la nchi yetu na sisi matabibu tumejipanga kutoa ushirikiano wa hali ya juu popote pale tutakapo hitajika hatutasita kutoa ushauri wetu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.