Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Afya. Namshukuru Mungu kwa kunijalia zawadi ya uhai na afya njema. Pia nampongeza sana Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Naibu Waziri wake Mheshimiwa Dkt. Mollel na Katibu Mkuu Dkt. Abel Makubi na watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wanapata huduma bora za afya, nawapongeza sana, Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Spika, nieleze kwa masikitiko makubwa juu ya kusuasua kwa ujenzi wa hospitali yangu ya rufaa ya mkoa ambao ujenzi wake umekuwa ni wa muda mrefu kwa zaidi ya miaka13 hadi sasa hospitali hii haijakamilika.

Mheshimiwa Spika, majengo haya ambayo yalijengwa miaka iliyopita yameshaanza kuchakaa na yatahitaji bajeti nyingine kwa ajili ya ukarabati hivyo kutokuwa na thamani ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa kuendelea kututengea fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali yetu ya rufaa lakini fedha hizi zimekuwa hazitoshi. Ninaiomba Serikali itutengee fedha za kutosha ili hospitali hii ya rufaa iweze kukamilika, endapo hospitali hii itakamilika itakuwa ni msaada mkubwa sana kwa wananchi ambao wengi hawamudu gharama za matibabu kwenye hospitali za rufaa za mikoa ya jirani hususani wanawake waishio pembezoni. Ninaomba Mheshimiwa Waziri Ummy atapokuja ku-wind unipe commitment ya Serikali ni lini hospitali hii ya rufaa ya Singida ni lini itakamilika?

Mheshimiwa Spika, pia hospitali hii ya rufaa ya mkoa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa tiba, watumishi wakiwemo madaktari bingwa, tuna madaktari bingwa sita tu na miongoni mwa hao wapo masomoni. Ninaiomba Serikali ituletee madaktari bingwa wa kutosha akiwemo daktari bingwa wa watoto ili wananchi wetu waweze kupata huduma za kibingwa ndani ya mkoa wao.

Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali kwa kutujengea hospitali za Wilaya ya Mkalama, Singida DC na Ikungi, lakini hospitali hizi hazina vifaa tiba, watumishi na dawa za kutosha.

Mheshimiwa Spika, uwepo wa majengo haya mazuri bila ya vifaa tiba na wataalam ni kazi bure, mfano hospitali ya Wilaya ya Mkalama, kwa mwaka wa fedha ulioisha 2021/2022 tulitengewa fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ununuzi wa vifaa tiba, lakini ni vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 77 tu ndivyo vilivyoletwa katika hospitali hii, jambo hili linasikitisha sana, fedha ipo lakini ni kwa nini MSD hawaleti vifaa tiba? Wilaya hii pia ina uhaba mkubwa wa watumishi 607. Naomba tuletewee vifaa tiba, watumishi na dawa za kutosha katika hospitali zetu za Wilaya, vituo vya afya na zahanati za Mkoa wa Singida ili malengo mazuri ya Serikali yaweze kutimia.

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja.