Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuunga mkono hoja ya kuumunga mkono Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli sina la kusema zaidi ya kusema Mwenyezi Mungu ni mkubwa. Mheshimiwa Rais ameonesha upendo mkubwa kwa watu wenye ulemavu. Hata hivyo, kitendo cha kuonesha upendo kwa watu wenye ulemavu, leo dunia inaitambua Tanzania iko katika ramani ya upendo kwa watu wenye ulemavu na walemavu sasa hivi wanasikika na wanaeleweka.
Mheshimiwa Spika, nitazungumzia maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ameonesha. Alikula chakula na watu wenye ulemavu Ikulu na aliwapongeza kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kupigania Mchezo wa Mpira. Akiwakilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza alituletea Shilingi Milioni 150 kwa watu wenye ulemavu, wakasema hatutakuangusha, tuliweza kushinda mpira wa East Africa, tukashinda Mpira wa Afrika, tukaingia katika World Cup. Haya ni mafanikio ambayo hajaweza kufanikiwa Yanga wala Simba. Tunaomba nao wajitahidi kama walivyofanya walemavu. Natamani siku moja nisikie Simba au Yanga wameingia katika mipira mikubwa kama hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kupitia huo mchezo, sasa hivi vijana 12 wameajiriwa nje ya nchi kama ma-professional Soccer, wanapata mahitaji yao na wengine wameniambia Mama cha kushukuru hatuna, tunatamani tukirudi kule turudi tena kwa Mheshimiwa Rais kumwambia tumefanikiwa kwa hili na sasa hivi familia zetu zinanufaika kwa ajira zetu nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi sina budi kwa hilo niseme tu Mwenyezi Mungu azidi kumbariki, azidi kuwapenda watu wenye ulemavu na vijana kwa ujumla na watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kupitia Wizara ya Madini, nimpongeze Mheshimiwa Rais mwamko huu na spirit aliyokuja nao baadhi ya Mawaziri wanaiga kuonesha spirit ya kuwapenda watu wenye ulemavu. Kwa kupitia Shirika la STAMICO tumepewa vitalu vya kuchimba dhahabu Mbogwe. Mimi mwenyewe nimekwenda pale kugawa vifaa kwa watu wenye ulemavu wenye usikivu hafifu, leo walemavu wanachimba dhahabu. Je, haya sio mafanikio? Tutanyamaza vipi bila kumpongeza kwa kuona leo walemavu wanataka kuuza dhahabu kwa kujifanya na wao wataondoa umaskini? Naomba na Wizara nyingine na taasisi nyingine ziige kama zilivyofanya Wizara ya Madini na STAMICO.
Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara ya Kilimo kwa kupitia mfumo huu waliokwenda na wenzao, wao wametoa hekari 50 kwa baadhi ya wilaya kuhakikisha walemavu wenye ulemavu wa ngozi wanaanza kulima. Kwa mfano, Chamwino wametoa hekari 50 kwa watu wenye ulemavu na taasisi ya ASA ikishirikisha na mwenyewe Bashe aliwaambia wapeni mbegu, wakapewa mbegu za alizeti na mbegu za mahindi. Huu ni mfano wa kuanza nao kuhakikisha na maeneo mengine wanatoa ardhi kwa watu wenye ulemavu walime. Kwa vile walemavu sio wote ambao hawawezi kulima, walemavu wenye usikivu mdogo wanaweza kulima, walemavu wenye matatizo ya ngozi wanaweza kulima.
Mheshimiwa Spika, sasa hii speed ya Mheshimiwa Rais twende nayo vizuri ili angalau tunachosema sasa hivi kuwa haki ya walemavu katika maendeleo inclusion yanakwenda sambamba na speed ya Mheshimiwa Rais. Mwenyezi Mungu amzidishie zaidi Mheshimiwa Rais na walemavu wanasema wana neno lao kuwa wao wako pamoja na yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, CRDB Bank ikishirikiana na waendesha bajaji 500 wa Jiji la Dar es Salaam, wameamua kwa pamoja kushirikiana nao kwa kufungua akaunti ili walemavu wale wasinyanyasike. Wanachukua mikopo huku mitaani ya shilingi milioni 14 kwa wahuni huko mitaani matokeo yake wanashindwa kurudisha pesa, wanakuwa wanatumika visivyo. Hata hivyo CRDB Bank kwa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, kwa kweli ni lazima tuyapongeze haya mashirika ambayo yako karibu na watu wenye ulemavu na tayari tunaona kabisa kama watu wale watawakomboa walemavu ambao wanahitaji mahitaji maalum.
Mheshimiwa Spika, niwapongeze na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge, wakafanye kazi ya kupambana kule chini. Hakuna wa kuachwa nyuma nobody should be left behind there is nothing about us without us. Walemavu wanahitaji inclusion katika kila eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana, kwa speed hii tunayokwenda nayo Mama ameongea neno moja zito kwa Watanzania amesema, tuwe mabalozi twende tukawalinde vijana wetu kule chini, wasiige tabia na utamaduni ambao sio wa kwetu. Kwa vile Tanzania ni Nchi huru ina sheria zake, taratibu zake, Dini zake, lakini vile vile ina mila na desturi. Hivyo wasituletee mila ambazo zitakuja kuwafanya watoto wetu wawe dhaifu kwa ajili ya wanachokitaka wao hapana.
Mheshimiwa Spika, hili neno limewafanya Watanzania wamekosheka, kuwa na faraja kuwa watoto wetu ambao wanataka kuharibiwa kila mmoja akawe balozi katika eneo lake. i Wabunge katika kila…
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
T A A R I F A
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, naomba pia nimkumbushe Mheshimiwa Riziki kwamba Mheshimiwa Rais mwaka 2022 ametoa shilingi milioni 60 kwa ajili ya mafuta ya watu wenye Ualbino na hii iko kwenye mchakato wa Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, ninachotaka kumkumbusha kwamba Mheshimiwa Rais anafanya mengi sana ambayo tutaweza kila siku kuyasemea na kuyatetea na kuyapigania. Kwa namna hiyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Riziki Lulida unaipokea taarifa hiyo?
MHE. RIZIKI S LULIDA: Mheshimiwa Spika, hiyo taarifa ni lazima niipokee, ni taarifa yenye mafanikio na ni kweli wenzetu wenye matatizo yaN wamepewa Mafuta ya Mabilioni. Sasa hivi tunae balozi wetu ambaye ni Mheshimiwa Mwigulu Nchemba amesimama na watu wenye ulemavu kuhakikisha hela zao za mikopo zinapatikana. Vile vile, Mheshimiwa Mwigulu ni balozi wa watu wenye ulemavu napenda awe pamoja na watu wenye ulemavu ili aweze kufanya nao kazi kwa pamoja ili walemavu hao wasihangaike kuombaomba. Hakuna wa kuombaomba kila mmoja atakuwa pamoja na sisi, tufanye kazi kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema tena naunga mkono hoja hii kwa kusisitiza Mheshimiwa Rais kwa kweli anafanya kazi kubwa kwa kupitia vijana na watu wenye ulemavu. Nasema ahsante na Mungu azidi kumbariki, ahsanteni sana. (Makofi)