Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha demokrasia nchini na kukuza diplomasia ya uchumi

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa shukrani na pongezi kwa Mheshimiwa Rais.

Kwanza naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Chiwelesa, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais pia tunamshukuru Mungu kwa kutupa Rais msikivu, kutokana na kipindi ambacho kwa kweli Mheshimiwa Rais amepokea madaraka haya hakupokea kwa njia ya kawaida, kwa hiyo hakukuwa na maandalizi. Nimshukuru pia kwa kuwa msikivu, tumepita
kwenye majungu mengi kuna watu wameitwa Sukuma Gang humu, kuna watu wameitwa majina tofauti, kuna watu wamepewa makundi tofauti, lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa usikivu wake, ameendelea kuchapa kazi na kuwaacha wapuuzi wanaounda makundi na kuchafua wenzao waendelee nao, pia kazi zetu za Serikali ziweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana mimi ni mmoja wa watu ambao nilimwangalia sana Mheshimiwa Rais siku anaenda kwenye mkutano wa CHADEMA kule Kilimanjaro, yaani nilikuwa najiuliza hii CCM yetu tunakwenda kuitumbukiza wapi? Lakini baadae nikaja kuona mtu mpaka kufika kwenye cheo cha Rais ujue amepitia mambo mengi sana.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wengi Wana-CCM kule vijijini hawakumwelewa Rais, lakini baadae mimi nilivyokuja kutafakari, leo nataka niwaambie hivyo ndiyo maisha ya wanasiasa tunaishi, kwamba Mheshimiwa Rais alivyoenda kuwasikiliza na kuzungumza nao na kula nao chakula, haya ndiyo maisha yetu wanasiasa. Hata Watanzania mkituona tunazodoana humu na upinzani, tunatoka pale nje tunanunuliana chai.

Kwa hiyo, niwaombe Watanzania sikilizeni hoja za maendeleo kuliko kusikiliza mipasho ya kwenye majukwaa na Mheshimiwa Rais ameonesha mfano, ameenda kuwasikiliza wamepiga cheers lakini sisi huku tunapiga kazi. Kwa hiyo, haya ndiyo Maisha yetu wanasiasa huwa tunaishi hivi. Msije mkasikiliza maneno yetu huku juu wanasiasa halafu mkaenda kuandamana na kuumizwa miguu. Sikilizeni hoja zinazojibu matatizo ya wananchi wetu huko vijijini.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazungumza suala la Mkaguzi (CAG); kwa kweli mimi ni Mbunge huu mwaka tunaenda wa nane, nimemuona Mheshimiwa Rais juzi alivyozungumza kwa ukali mpaka akatumia na kaneno ka kizungu wale wenzangu kule hawakukaelewa akasema stupid! Ni kaneno kagumu sana sidhani kama anavyosikiliza Wabunge mnavyosema wale waone milango hakuna mtu anaweza kutoka kwenye mafuta kwa njia ya hiari nchi hii hayupo.

Mheshimiwa Spika, natoa mfano, Mheshimiwa Mbunge Ng’wasi Kamani kwenye Bunge lililopita yeye ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC, alitoa mfano mzuri hapa akasema, kuna Mkurugenzi ametoka Ilemela ana tuhuma ya wizi wa shilingi bilioni 11 ameletwa kwa Mheshimiwa Musukuma, kwa miaka 22 sijawahi kupata hati chafu, nimo kwenye milioni sita, kwamba mtu anaiba huku halafu ninyi wenyewe mnamhamisha mnampeleka Halmashauri nyingine, huku anaendelea na uchunguzi anachukua pesa zetu kugharamia kesi ya Ilemela. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana ngoma hii ikija humu kama alivyosema mwenzangu Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao hapa, katika vitu ambavyo Spika Mheshimiwa Dkt. Tulia tutakavyokukumbuka, hatutaki tena kupiga swaga, maana hizi swaga tumepiga mno kila taarifa ya CAG tunaongea, Serikali mnatutengenezea uadui bora mmalize wenyewe, tunataja watu watu hawachukuliwi hatua.

Mheshimiwa Spika, mtu anachukua kesi anaenda anapaki TAKUKURU, hivi TAKUKURU unachunguza mtu CAG ya mwaka jana halafu tena unakutwa na CAG ya mwaka huu? Jamani kama huko TAKUKURU na kwenyewe kuna TAKUKURU si na kwenyewe kuundiwe timu ya kuwachunguza? Tunaelekea wapi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani tumejadili mambo haya mwaka jana tukataja watu, Kamati ya LAAC imeletwa taarifa na ikataja Halmashauri zaidi ya tisa, halafu hawahawa
wamepata Hati Chafu! Mheshimiwa Rais amefika hatua ya kusema pumbavu, sasa labda aje asomewe taarifa ya mwakani akiwa na kiboko mkononi, kama Bunge hatutachukua hatua ya kumsaidia! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama sheria zetu tulizitengeneza ni mbovu, hili Bunge ndiyo Bunge la wananchi wote, hatuwezi kuwa tunamuona Rais, ina maana kama Rais mwaka jana alisema atakayechezea pesa zangu za miradi ataitambua sura yangu halisi, maana yake hawa waliochezea hizi pesa wamemvizia Mama wakachungulia dirishani wakaiona sura? Sasa wamerudi kwa utaratibu mwingine haiwezekani! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kauli ya Mheshimiwa Rais mwaka jana mnisikilize vizuri, alisema jamani kama mnakula kuleni kwa urefu wa Kamba, hawa watu hawanunui kamba za katani, wananunua manati likijaa linatanuka! Lazima hili Bunge kwa mara ya kwanza tuoneshe mfano, haiwezekani. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana, naunga mkono hoja tunasubiri ngoma ije hapa tulale nao mbele. (Makofi)