Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri mkuu kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya na uzima lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli sote tunakubaliana ni mtu wa kazi, ni mtu rahimu sana, ni kiongozi wa mfano wa kuiga Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakushukuru na kukupongeza sana. Pia nakupongeza kwa ziara nzuri unazozifanya kwa Taifa letu ukiwa unashughuluka na wale ambao wanaturudisha nyuma Mheshimiwa Waziri Mkuu hongera sana. Napongeza wasaidizi wako wote kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli wananchi wa Hai wamenituma kwa dhati kubwa sana kwamba nisimame hapa nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wamenipa lugha yao ya kusema, wameniambia niseme “nahavachee lakini ashenalee ologhandumaa, lugha hizi zinamaanisha uzito wa shukurani zikisema asante kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa tanzanaia siyo jambo la kawaida leo tunazungumza Mheshimiwa Rais amekanyaga Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Hai mara saba na pale Hai mimi ni mnufaika maana akishuka Uwanja wa Ndege lazima asalimie watu pale Bomang’ombe. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mambo makubwa aliyoyafanya.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli acha tuseme tulikuwa na hali mbaya miaka 15 hatukuyaona haya ambayo nitasema hapa, tulikuwa na tatizo la maji pale kata zetu za ukanda wa chini Bomang’ombe, Bhundugai, Muungano, KIA leo Mheshimiwa Rais ametuletea fedha bilioni 3.3 na mradi umeshakamilika watu wa Hai wanapata maji.

Mheshimiwa Spika, nikubalie niseme kuhusu Huduma za Afya, tuna Vituo vya Afya vitano vipya havikuwepo vinajengwa ndani ya Wilaya ya Hai Chekimaji, Mkwansila, Kisikii imekarabatiwa, Luongoi niseme haya ni makubwa sana Mheshimiwa rais anatutendea, ukienda upande wa elimu ndio usiseme shule kongwe kwa maana Machame Girls, Nyamungo zimefanyiwa ukarabati fedha kemkem zimeletwa kwa ajili ya shule zetu chakavu.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli wananchi wa Hai wanasema ahsante sana. Barabara ndio usiseme pale Bomang’ombe barabara nne zinajengwa kwa kiwango cha lami na taa juu. Kuna barabara nimehangaika nayo mpaka ilikuwa imepewa majina yasiyofaa leo ni barabara ya lami inajengwa Makoa mferejini tayari kilometa saba mkandarasi yuko site na saba nyingine zinakuja tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa haya anayoyafanya.

Mheshimiwa Spika, Viwanda, nimesema hapa jana kiwanda cha machine tools kinaunguruma tunaomba tu Serikali sasa ilete zile taasisi zikanunue chuma pale na vipuri lakini pia common use facilities mnafahamu kwamba tumeshatengewa fedha nikumbushe wizara ya kilimo wakamalizie kazi hiyo. Skimu za umwagiliaji pale Longo “A” fedha imekuja. Hayo ni mambo makubwa sana Mheshimiwa Rais anayotufanyia nampongeza na namshukuru sana.

Mheshimiwa Spika, niseme pamoja na mazuri hayo Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba nikukabidhi hili linaitwa Soko la Kwasadala, kabisa kabisa nenda nalo Mheshimiwa Waziri Mkuu kafanye nalo kazi soko hili lijengwe ni kichocheo muhimu sana kwa uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro. Niombe pia tunashule ya sekondari pale Lemila nimeshaiomba hapa

Mheshimiwa Waziri Mkuu nakukabidhi haya machache najua wewe utaenda nayo pamoja na chuo kile cha Losoa ni ahadi hizi za Serikali nisaidie Mheshimiwa Waziri Mkuu hili nalo likatekelezwe.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa haraka sana niguse jambo moja hapa. Hizi kuta zisipochukua kumbukumbu zetu tutakuwa hatujajitendea haki. Kila mmoja aliyeko humu ndani alishika kitabu anachoamini nacho akaapa pale na nitatumia kile ambacho nilikitumia kuapa hapa kuzungumza ambayo yanaendelea kwenye jamii yetu.

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya Waziri Mkuu amezungumza Habari ya ukatili wa Watoto. Nitaenda mbali si ukatili wa watoto tu lakini na hiki kinachoendelea cha ndoa za jinsia moja. Asubuhi amenipigia Sheikh Omari, Sheikh wa BAKWATA Wilaya ya Hai akaniambia Mheshimiwa Mbunge msiposema mawe yatasema, semeni huko Bungeni na sisi BAKWATA Mkoa wa Kilimanjaro siku Jumamosi tuna maandamano ya kupinga hizi ndoa za jinsia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili mnikubalie ninukuu kitabu cha Biblia ambacho nilishika kuapa hapa. Ukienda Wakorintho wa kwanza 6:9 kasome mambo haya yanakatazwa, ukienda Warumi 1:26-27 yanakatazwa mambo haya ya hovyo yasiyofaa kwenye jamii yetu lakini kwenye sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 inasema, naomba unikibalie nisome ile Ibara ya 154 nanukuu; “Mtu yoyote ambaye; (a) anamuingilia mtu yeyote kinyume na maumbile au anamuingilia mnyama kimwili au anamruhusu mwaume kumuingilia yeye mwanaume au mwanamke kumuingilia kinyume na maumbile atakuwa ametenda kosa atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha Maisha wakati mwingine kifungo kisichopungua miaka 30”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa unyenyekevu mkubwa sana naomba chombo chako hiki kitakatifu kitusaidie kusimamia haya binafsi nakemea jambo hili vibaya mno. Wale wote wanaojihusisha na ndoa za jinsia moja ni jambo lisilokubalika hii ni laana, sisi ambao tumeshika vitabu vyetu vitakatifu hapa tukaapa tukasema Mwenyezi Mungu atusaidie tutailinda Katiba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuanze kuilinda Katiba hii kwa kukemea vikali lakini niombe Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo hili lipo chini ya Ofisi yako, wale wote wanofanya mambo haya ambao wanatajwa kwenye jamii ambao wanaonekana Serikali ichukue hatua kutekeleza hili na wachukuliwe adhabu hadharani ili na wengine wajifunze. Mheshimiwa Waziri Mkuu tukiendelea kunyamaza kizazi kinachokuja watafukua makaburi yetu watuchape viboko maana sijui hata kama watakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo mwanaume amuingilie mwanaume uzao unatoka wapi? Mwanamke amuingilie mwanamke uzao unatoka wapi? Mimi niwaombe watanzania kwenye hili tuungane kwa pamoja kukemea vikali sana na niwaombe viongozi wetu wa dini wala wasione aibu maana wakati mwingine watu wanasema watu hawa wana manguvu, wanamanguvu kuliko mungu? Haiwezekani. mwenyenguvu ni mungu na yeye ndio ametuumba na yeye ndio anatukataza haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo nirudi kwenye hoja kuhusu matumizi ya fedha za Serikali. Kwenye Kamati yetu tumejifunza kitu kigumu sana kinachoitwa bakaa. Utakuta kila Halmashauri inakuambia wamevuka na fedha za mwaka uliopita, lakini fedha hizi zinapokuja sasa kuombewa tena kibali zinatumika nje ya utaratibu na unakuta zipo ambazo zimebaki na ukiwauliza hizo ambazo zimebaki zipo katika akaunti gani, hawakuambii.

Mheshimiwa Spika, ningeomba waende wafanye mapitio ya sheria ile ya bajeti ya mwaka 2015 kifungu cha 21(1)(4) ambacho kinampa pay master general nguvu baada ya fedha kuvuka mwaka anaambiwa anaweza wakileta maombi anaweza kukubali sehemu ya maombi yale au kukubali yote au kutokukubali.

Mheshimiwa Spika, sasa kifungu hiki kinapora madaraka ya Bunge kwa sababu sisi tumeshapitisha bajeti hapa kwamba kituo cha afya kikajengwe. Kwa sababu tu ya uzembe wa watu wachache, wameshindwa kutekeleza miradi, fedha imevuka mwaka sasa tunaambiwa tuombe upya na bado Pay Master General anapewa mandate ya kukubali au kutokukubali ilhali sisi tumeshapitisha hapa.

Mheshimiwa Spika, na jambo hili tusipoangalia fedha nyingi za wananchi wa Tanzania itapotea; na inapotea si kwamba wananchi ndio wamekosea eti kuna mkurugenzi eti kuna afisa mipango ameshindwa kuwasilisha reconciliation za mahesabu yake kwa hiyo anayeadhibiwa sasa ni mwananchi kwa kutokujenga kituo cha afya.

Mheshimiwa Spika, jambo hili halikubaliki, halikubaliki kabisa. Tunawapa wananchi adhabu ya kukosa miradi kwa sababu eti watu watu hawakufunga hesabu. Mimi naomba sana jambo hili liweze kutazamwa vizuri ili tuweze kwenda kwenye uwajibikaji na yale ambayo tumeyapanga yaweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hili ni sambamba pia, nimesoma kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, anasema vyama vinavyopewa ruzuku wamepewa bilioni 17.5 na akataja; kuna chama cha NCCR Mageuzi, CCM, CHADEMA, DP, CUF, ACT Wazalendo; na huko wakaangalie bakaa, kama kuna fedha zilivuka mwaka tuambiwe zitatumiwaje, kama hazikutumika mwaka huu wa fedha, sasa hizi bakaa zinaenda kutumikaje?

Mheshimiwa Spika, nimeona umeshashika mic, ishara ya kwamba nimemaliza muda wangu; nakushukuru sana naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)