Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi, lakini awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha mimi na sisi sote tuliomo humu ndani kuamka salama tukiwa na afya njema. Vilevile nielekeze shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyolitendea haki Taifa letu na kwa namna anavyopambana katika kutekeleza Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri iliyosheheni kila mahali na ufafanuzi wenye viwango.

Mheshimiwa Spika, mimi nitajielekeza kwenye mambo mawili makuu. Wakati naingia kwenye Bunge hili nilisema kwamba Wilaya ya Liwale ilikuwa kisiwani. Wakati ule wilaya ya Liwale ilikuwa kisiwani kwa sababu ilikuwa haifikiki kwa barabara wala kwa mawasiliano ya simu; lakini kwa namna Chama cha Mapinduzi kinavyotekeleza Ilani yake nashukuru kusema leo hii Wilaya ya Liwale inafikika kwa mawasiliano ya simu kwa zaidi ya asilimia 80.

Mheshimiwa Spika, lakini bado Wilaya ya Liwale ipo kisiwani kwa upande wa barabara. Kwa uelewa wangu mimi barabara ni kama mshipa wa damu kwenye mwili wa mwanadamu. Wilaya ya Liwale kipato chetu kipo chini sana na hali ya maisha ni ngumu sana, ni ghali sana kwa sababu ya barabara. Ili mazao ya mkulima yafike kwenye masoko yanahitaji barabara.

Mheshimiwa Spika, na kwa mwaka huu na miaka ya hivi karibuni tumepata miradi mingi sana kwenye halmashauri zetu. Hata hivyo Wilaya ya Liwale utekelezaji wake unakuwa mgumu kwa sababu gharama ya usafirishaji wa malighafi kupeleka site ni kubwa sana kutokana na ubovu wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimezungumza mara nyingi kuhusiana na barabara ya Nachingwea – Liwale mpaka Masasi, barabara hii upembuzi yakinifu umeisha mwaka 2014. Leo tukiambiwa kwamba Serikali inatafuta fedha za ujenzi wa barabara hii akili yangu ya kawaida inakataa, kwa sababu ziko barabara zilizofanyiwa upembuzi yakinifu 2015, 2016, 2017, 2018 zimeshajengwa. Hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba utashi wa kujenga hii barabara bado haupo Serikalini, Serikali bado haijaona umuhimu wa kujenga barabara hii. Naomba sana Barabara hii ya Masasi – Nachingwea – Liwale ijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi nataka niseme ukweli kwamba shida yangu si kwenye bajeti; nimedumu kwenye Kamati ya Miundombinu miaka saba; maika yote saba barabara hii imekuwa ikitengewa fedha lakini haijengwi. Naomba sana Serikali, maendeleo haya yote ambayo tunayosema tumeletewa sisi Wilaya ya Liwale; upande wa elimu, afya na wa kilimo, kama hatutaweza kupata barabara ya uhakika haya yote kwetu yatakuwa ni kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini barabara ya pili ninayoweza kuizungumza ni Barabara ya Nangurukuru – Liwale, barabara hii inazaidi ya Kilometa 230, upembuzi yakinifu umeisha kwenye baketi iliyopita ya mwala 2021/2022. Ninaiomba sana Serikali waone umuhimu wa kujenga hii barabara ili na sisi tuweze kutoka kuwepo kule kisiwani.

Mheshimiwa Spika, na nikienda mbali zaidi, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye bajeti ya mwaka jana alisema mwenyewe kwamba hii barabara kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 itajengwa; lakini mpaka leo hakuna chochote kinachoeleweka kwetu watu wa Liwale. Tuliambiwa hii barabara inajengwa kwenye huu mradi wa EPC+F sijaelewa mpaka leo hii EPC+ F imeishia wapi na sisi tuna shida ya hii barabara ya Nachingwea – Masasi – Liwale.

Mheshimiwa Spika, lakini barabara nyingine ambayo naweza kuizingumzia, ambayo inaweza ikatutoa sisi kisiwani ni barabara ya Morogoro. Naomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi tuitoe Liwale kisiwani.

Mheshimiwa Spika, pointi nyingine, naomba niende sasa kwenye upande wa maliasili. Kwa upande wa maliasili huku nako kuna uelewa mdogo sana wa jiografia ya nchi yetu. Kwenye bajeti ya mwaka 2021 tuliletewa fedha kutoka World Bank kwa ajili ya kuendeleza utalii kusini lakini sisi Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Liwale hela zile hatukupata. Nilipokuja kuuliza humu nikaambiwa kwamba eti fedha zile zimekwenda Songea, Morogoro na Mbeya, Nyanda za Juu Kusini, kwa hiyo sisi Liwale hatupo. Kwa bahati mbaya Mwenyezi Mungu naYe ana karama zake, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano akalipandisha hadhi Pori la Selous kuwa Hifadhi ya Mwalimu Nyerere, asilimia 60 ya hifadhi iko Liwale. Sasa wale waliosema kuendeleza utalii wa kusini wakimaanisha ni Mbeya, Songea na Morogoro kwa sababu wao ndio Nyanda za Juu Kusini wameumbuka kwa sababu tayari TANAPA ipo Liwale na Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Spika, lakini hapo hapo utakuta kuna Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Mimi nisikitike sana, kama Bwawa la Mwalimu Nyerere mkaiweka Lindi tofauti na hiyo mnaikosea sana. Kwa sababu asilimia 60 ya Pori ya Selous iko Liwale. Sasa unapokwenda kutengeneza mradi ukasema Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere iko Pwani na Morogoro, mimi siwaelewi. Mimi nawaomba sana Watendaji hebu nendeni mpitie jiografia ya Nchi yetu, mnaposanifu hii miradi pitieni jiografia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji ya Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa asilimia 60 yapo Liwale, nendeni mkapitie jiografia. Mito yote tunayoitegemea kupeleka maji, Mto Rwebu, Mto Mbarang’andu, Mto Mbwemkuru yote hii imetoka Liwale. Hebu nendeni mkaangalie ramani hiyo, kututenga sisi na Bwawa la Mwalimu Nyerere mnatukosea sana.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kwa upande wa Maliasili…

SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka ngoja, na mimi nataka nielewe maana mimi sitoki Liwale; lile Bwawa la Mwalimu Nyerere pale lilipo ni Liwale? Wewe ni Mbunge wa pale?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, lipo, ukitaka kulifahamu lile Bwawa lilipo, ukichukua zile heka zote ambazo zimetajwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, nendeni mkaangalie ramani tunapopakana sisi na Songea…

SPIKA: Usitutume, usitutume kwenda kuangalia mimi ninazungumza na wewe, pale mahali bwawa…

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, jibu ni ndiyo.

SPIKA: Umeeleza kwenye maelezo yako, kwa nini nakuuliza, kwa sababu umeeanza kwa kusema mito inayopeleka maji kwenye lile bwawa inatoka Liwale. Kwa hiyo mito inayopeleka iko Liwale na Bwawa pia lipo Liwale.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, jibu ni ndiyo kwa sababu sehemu ya bwawa lile ipo Liwale.

SPIKA: Sehemu ipi ya bwawa? Maana tulishaenda pale, tulimsindikiza Mheshimiwa Rais kubonyeza kile kitufe ili maji yaanze kujaa. Sehemu ipi ya lile bwawa?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, upande wa kusini na upande wa magharibi wa lile bwawa iko Liwale. Mahali ambapo tunapakana na Mahenge na tunapakana na Kilwa.

SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka unajua inabidi ukatafute hiyo ramani uniletee hapa mbele. Kwa sababu wewe upo Mkoa gani?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Lindi, ndiyo

SPIKA: Kwa hiyo, Mkoa wa Lindi sasa hivi lile bwawa lipo Mkoa wa Lindi?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, lipo sehemu ya Mkoa wa Lindi.

SPIKA: Usiseme sehemu…

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, mimi nasema lipo Mikoa Mitatu, Pwani, Morogoro na Lindi.

SPIKA: Mimi nataka nikuelewe, Mheshimiwa Kuchauka kama ukisema kuhusu maji basi maji yanatoka kila mahali. Nataka nielewe hoja yako, mahali bwawa lilipo, pale ni Lindi?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Pale ni Lindi?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Sawa, kaa, ngoja tufuate hiyo ramani kwanza halafu utakuja kupewa nafasi. Maana naona tusije tukapata upotoshaji hapa wa ziada, sijui kama Serikali mtu wa nishati yupo hapa? Hebu tuelezee kidogo hiyo ramani maana tunaweza kujikuta tumeenda Lindi, Mheshimiwa Waziri Mkuu anatoka Lindi, sasa kumbe bwawa liko Lindi bwana, sisi kila siku tunasema Morogoro tunasema Pwani, hebu tuelezee.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kutoa taarifa kwamba Mheshimiwa Kuchauka alinifuata na kunipa hiyo taarifa yake lakini nikamwambia sisi kama Serikali kwa uelewa wetu na mipaka na ramani tulizokuwa nazo, bwawa lipo katika Mkoa wa Pwani na Morogoro. Ndio uelewa tuliokuwa nao, na nikamsisitiza kama anauelewa tofauti basi atusaidie ili na sisi tujifunze. Alikuwa anazungumzia CSR na nikamwambia sisi kwa uelewa wetu na ufahamu wetu Bwawa lipo katika Mkoa wa Pwani na Morogoro. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa umemaliza? Nilichokuuliza, Mheshimiwa Naibu Waziri umemaliza eeh?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nimemaliza.

SPIKA: Haya kuna maelezo nyuma yako hapo, Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. DKT. ENG. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Spika, nilikua naomba kumpa taarifa muongeaji kwamba ni kweli bwawa liko Mkoa wa Pwani lakini catchment area litakapojaa ndio asilimia hiyo nyingi ipo Liwale.

SPIKA: Sawa sasa, naomba tusaidie kwa sababu wewe unatatupeleka vizuri. Kwa hiyo Bwawa la Mwalimu Nyerere liko wapi? lipo Mkoa gani? Maana umesema litakapojaa, sasa litakapojaa sasa maana yake litaendelea kutawanyika huko linakoelekea. Sasa hivi tukisema hivi, Bwawa la Mwalimu Nyerere litakalo zalisha umeme kilowati 2,115, liko wapi?

MHE. DKT. ENG. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Spika, nadhani hapo mchanganyiko unakuja kwenye bwawa ni nini? Kwa sababu ile infrastructure iliyojengwa ile miundombinu iliyojengwa ipo Mkoa wa Pwani lakini litakapo…

SPIKA: Haya, ngoja, lile jengo. Wewe mwenyewe umesema pale palipojengwa na maji yatakayojaa tumeyatenganisha? yaani yametangana?

MHE. ENG. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kwa hiyo pale palipojengwa ni mkoa mwingine, patakapojaa ni mkoa mwingine?

MHE. ENG. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Spika, patakapojaa si mkoa mmoja tu ni huu Mkoa wa Pwani, Liwale…

SPIKA: Swali langu lililonifanya nimuulize Mheshimiwa Kuchauka si bwawa litaenda umbali gani? Hoja yangu Bwala la Mwalimu Nyerere liko Mkoa wa Lindi au liko Pwani na Morogoro ndiyo hoja iliyoko hapo.

MHE. ENG. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Spika, lile liliojengwa lipo liko Mkoa wa Pwani lakini maji yakijaa ni mikoa minne.

SPIKA: Sasa ukianza maji yatakayojaa maana yake hata maji yanapotoka nako basi ni bwawa, maana hayo maji yanayojaa pale yanatoka mahali. Sasa jamani, ngoja ngoja tusijichanganye wenyewe tusiwachanganye wananchi. Bwawa la Mwalimu Nyerere ukianza kusema litakapojaa litaenda mbali mpaka wapi, mimi ninafikiri tusiende huko na maji yatakapojaa mengine yataelekea wapi mimi nadhani tusiende huko la sivyo tutachanganya mambo na tutawachanganya wananchi. Kama zipo huduma ambazo zinahitajika kupelekwa Liwale kwa yale maji yanayojaa pale hilo ni suala lingine, lakini hatuwezi kusema bwawa sasa kijiografia liko wapi? Liwale. Sasa maana yake Morogoro limetoka na Pwani limetoka likahamia huko Liwale. Je, maji kama hayakujaa kiasi hicho cha kufika huko Liwale? Tunalihamishaje hilo bwawa? (Kicheko)

Mimi ninafikiri tutumie jiografia tena ile ya shule ya msingi kabisa, Bwawa la Mwalimu Nyerere Mheshimiwa Kuchauka kwa ufafanuzi huu uliotolewa kama umeelewa, liko mkoa gani? Ili nikuruhusu uongee, la si hivyo itabidi uniletee ramani inayoonyesha pale Liwale ipo wapi kwenye lile bwawa.

Mhesimiwa Kuchauka.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, labda sikueleweka. Tunapozungumzia Bwawa la Mwalimu Nyerere sio pale tu mahali ambapo bwawa limejengwa. Tunapozungumza ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kuna yard ambayo yenyewe imejengwa na eneo lote lililochukuliwa ndiyo maana Mheshimiwa pale akasema kuna catchment area, kwa hiyo ile area imekusanya mikoa mitatu, ambayo ni Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Pwani, maana yangu ilikuwa ni hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia bwawa kama …

SPIKA: Nimeshakuelewa. Bwawa la Mwalimu Nyerere sasa hivi liko wapi? Wewe nijibu kijiografia tu, liko wapi? Sasa hivi tunapozungumza, liko Mkoa gani?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, liko Mkoa wa Pwani.

SPIKA: Ahsante sana, malizia mchango wako.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, bado niko upande wa maliasili. Kwa upande wa maliasili, kwanza niishukuru Serikali kwa namna inavyopambana na wanyamapori jamii ya tembo. Sisi Wilaya ya Liwale mwaka huu tuliletewa mahindi, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuletea mahindi ya msaada ambayo yameuzwa kwa shilingi 700, ili kufidia yale madhara ambayo wananchi wetu walipata madhara baada ya mazao kuliwa na wanyama hawa tembo.

Mheshimiwa Spika, lakini ninaiomba Serikali kwenye hatua hii, tuongeze bidii ya namna gani ya kupata nafasi ya kwenda kudhibiti wale wanyamapori. Kwa sababu mwaka huu tayari tumeletewa mahindi; na sisi Liwale hatuletewi mahindi kwa sababu ya hali ya hewa, hatuna ukame wa kushindwa kulima kupata mazao ya chakula, tulipatwa na njaa kwa sababu ya wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi ombi langu, kama Serikali itashindwa kabisa kabisa kudhibiti hawa wanyamapori basi hayo mahindi mwakani tusiletewe kwa kununua, tupewe bure, kwa sababu hali yetu bado ni mbaya; wakulima wanakaa mashambani wanahama mashambani kwa sababu ya athari za wanyamapori jamii ya tembo. Tuliahidiwa kujenga vituo kwenye kata ya Lilombe, bado kituo kile hakijajengwa, tuliahidiwa kujenga kituo Kata ya Mkutano, Kijiji cha Nakipulyungu, bado hakijajengwa, tuliahidiwa kujengwa kituo Kata ya Mlembwe katika Kijiji cha Ndapata bado kituo kile hakijajengwa. Vituo hivi vikijengwa na askari wakiwepo hapo tutaweza kupata nafuu kidogo wakulima wakaweza kuvuna mazao yao.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine naomba nizungumze kuhusiana na Wizara ya Mambo ya Ndani. Wilaya ya Liwale kwa jiografia yake kituo chetu kile kidogo cha polisi pale hakina kituo cha karibu cha kweza kupata msaada wa kipolisi. Wizara walikuja wakatuahidi kujenga vituo viwili vya msaada ili kuisaidia Liwale kiusalama. Tuliambiwa tutajengewa Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Lilombe, tukaambiwa kitajengwa Kituo kingine cha Polisi kwenye Kata ya Kimambi, lakini bado miradi hii haijakamilika. Hata hivyo, mimi niende mbali zaidi, hata Kituo chenyewe cha Polisi pale Liwale Mjini, nitasema hapa, kwamba ilikuwa ni nyumba ya mtu binafsi polisi wakapanga mpaka leo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kile kituo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka kengele ya pili imegonga, Sekunde 30 malizia.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ombi langu, pamoja na kwamba mimi nilitoa milioni 10 kwa ajili ya Mfuko wa Jimbo kujenga kituo kile lakini bado Serikali haikutupatia fedha kujenga kituo cha polisi katika Mji wetu wa Wilaya ya Liwale.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)