Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi tena ya kuweza kuchangia hoja hii. Nichukue fursa hii pia kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jinsi ambavyo ameendelea kutekeleza majukumu yake kwenye miradi mbalimbali na wananchi wa Kilolo wamenituma nishukuru sana kwa mambo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, orodha ni ndefu sitaweza kuimaliza, lakini tushukuru kwamba baada ya miaka 30 ya kusubiri ameweza kutoa fedha kwa ajili ya ufufuaji wa mashamba ya chai ambayo yalikuwa yametelekezwa kwa miaka mingi. Pia zimetolewa fedha za ruzuku ya mbolea na wananchi wa Kilolo wamenufaika sana tunashukuru sana. Pia imetolewa fedha kwa ajili ya ukuzaji wa miche ya parachichi ambayo mkulima alikuwa ananunua kwa shilingi 5,000 na watu wa TARI wametuahidi kuuza kwa shilingi 1,000, ni punguzo kubwa na naamini kwamba wananchi watanufaika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Iko miundombinu ya afya, lakini pia iko miundombinu ya elimu, kwa uchache wa muda kwa ujumla wake tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi anayoifanya na nimkaribishe sana Kilolo kwa ahadi yake kwa ajili ya kuja kuhamasisha kilimo cha parachichi, tunamkaribisha sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wananchi wa Kilolo wanamsubiri.

Mheshimiwa Spika, napenda nijielekeze sana kwenye suala la vijana hasa utaratibu wa ajira na kwenye changamoto mbalimbali wanazozipata kwenye masomo. Jambo la kwanza ambalo ningependa kuzungumza ni utaratibu wa ajira kwa vijana wanaojitolea kwenye taasisi mbalimbali hasa kwenye sekta ya elimu na sekta ya afya.

Mheshimiwa Spika, tulishatoa ushauri mara kadhaa tukiwa kwenye Kamati kwamba utengenezwe mfumo maalum wa vijana kujitolea na huo mfumo uanzie jinsi vijana wanavyopatikana. Tukianza kuangalia jinsi vijana wanavyopatikana utengenezwe mfumo ambao hautoi upendeleo. Tukiacha hivi hivi maana yake ni kwamba mtoto wa Mwalimu ndiye atakayejitolea, mtoto wa mkulima hatajitolea na watoto wa watu wengine watajitolea na wengine hawatapata nafasi ya kujitolea. Tuanze na jinsi gani vijana watatakiwa kujitolea.

Mheshimiwa Spika, kitu cha pili, wale vijana wakishajitolea kuwe na mfumo mzuri wa ufuatiliaji ili ule mserereko inapofika wakati wa kuajiriwa waweze kuajiriwa. Sasa hivi hata namna wanavyopatikana wanavyoingia kujitolea bado haiko sawa na Serikali inajua wako vijana wanajitolea, waliingiaje? Ni rahisi kupanga namna wanavyoingia ili kuwafuatilia kwa sababu tukiacha hivi, kwa sababu watu ni wengi hata kuingia kujitolea nayo ni fursa. Kwa hiyo tuangalie namna vijana wanavyoingia kujitolea na jinsi wanavyolelewa mpaka wakati wa kuajiriwa ili uwe mserereko na huo unaweza ukatengenezwa mwongozo ambao Serikali inaweza ikautumia kuhakikisha kwamba kuna utaratibu mzuri hata wa kuingia kwenye kujitolea.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili bado linahusu ajira na jinsi ya upatikanaji. Siku za karibuni kumekuwa na vijana wanaokwenda JKT. Wanapofika JKT unafika wakati wa kwenda kujiunga na jeshi, hizo nafasi zinatolewa pale lakini hakuna uwazi wa jinsi vijana wanavyotolewa JKT na kuingia kwenye ajira. Matokeo yake ni vi-memo vingi vya vijana walioko JKT kwa Wabunge na viongozi tuwasaidie wajiunge na jeshi. Serikali iandae utaratibu mzuri na iweke uwazi kwa vijana wanaokuwa JKT ili wanapoingia jeshini nafasi zinapotolewa kuwe na uwazi ili vijana wale wasiwe wanasema leo wamechukuliwa watatu, ni ndugu pengine wa mtu fulani, kuwe na uwazi wa kueleweka ili Serikali inapowachukua kila mtu aridhike. Wale vijana wanaotoka JKT zile nafasi hazitoshi wale vijana wanaotoka JKT ambao hawakuajiriwa watoke wakiwa wameridhika, lakini kwa utaratibu wa sasa siyo wa wazi, una malalamiko na manung’uniko makubwa na siyo fair kwa vijana kutokujua uwazi huo umefanyika kwa kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado niko kwenye vijana na kwenye sehemu ambazo kidogo zina changamoto. Sijajua kigugumizi cha kuwakopesha vijana wanaosoma vyuo vya kati kinatoka wapi? Vijana hao ni watoto wa maskini, vijana hao wakimaliza vyuo tunawaajiri sasa hivi tuna zahanati, pharmaceutical technician, tuna lab technician wametoka kule. Kwa nini vijana ambao ni wa vyuo vya kati hawapewi mikopo na wakati wa kuajiriwa wanaajiriwa? Wakati wao pia ni watoto wa maskini wakati ada zao nyingine ni ndogo? Tumeongea muda mrefu hapa lakini Serikali haitoi majibu ya kueleweka kuhusu vijana wa vyuo vya kati kupata mikopo?

Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali na nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunao vijana wengi sana ambao wako vyuo vya kati na wao pia wana haki ya kupata mikopo kama wanavyopata vijana wa vyuo vikuu.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho kuhusiana na vijana, ni uunganishaji wa miradi hii inapotengenezwa. Nataka nitoe mfano, hivi karibuni kulitokea tangazo la miradi ya BBT. Naishukuru sana Serikali kwa ubunifu mzuri, lakini kwenye maeneo yetu kuna vikundi vya vijana vya 10% ambavyo vinajihusisha na kilimo. Sasa ilikuwa ni rahisi ku- search vijana ambao tayari wako kwenye kilimo kupitia kwenye mikopo ya 10% na kuwaingiza kwenye BBT badala ya kuchukua vijana wapya ambao watatakiwa kuanza upya na hawa vijana wenye 10% ambao wana mikopo tayari wana mashamba ndiyo maana walikopa na interest yao ni kulima na ndiyo maana wamekopa mikopo ya kilimo. Kwa hiyo kama tungechukua vijana wale maana yake ni kwamba ni rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba BBT itakayofuata tuchukue vijana waliokopa mikopo ya 10%, wafundishwe kwa sababu tayari ni wakulima, wako kwenye kilimo na ndiyo interest yao badala ya kuchukua vijana wapya na hao vijana wa 10% wako waliomaliza vyuo vikuu na wanataka kulima. Kwa hiyo itakuwa rahisi zaidi wao kwenda na kilimo kuliko mpya ambaye ametafuta tu fursa. Napendekeza kwamba hilo liangaliwe ili vijana waendelee kupata mikopo.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa sitendi haki kwa kuwa pia watu wengi wamezoea kuniita mchungaji hapa kama sitazungumzia suala hili la mambo ya mahusiano ya jinsia moja ya ushoga na haya mambo mengine yanayoendelea ya unyanyasaji wa watoto. Pia nitakuwa sijakitendea haki kizazi hiki na kizazi kijacho.

Mheshimiwa Spika, Tanzania hii sisi kama viongozi inabidi tukemee kwa nguvu zote aina yoyote ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wetu walioko majumbani na kwenye taasisi. Niipongeze Serikali imepiga marufuku watoto wadogo kwenda shule za bweni, lakini nafikiri kuna hatua zaidi ya kuchukua tena nilikuwa najiuliza ni kigezo gani kilisema la tano ndiyo wanakuwa wameshafikia kwenda boarding? Kwa sababu kwa kawaida kulitakiwa kuwe na kigezo kwamba darasa la tano wana umri gani badala ya kuangalia darasa, tungeangalia umri kwa sababu wengine darasa la tano na bado ni watoto wadogo, lakini kwa ujumla wake ni vizuri tukatengeneza mifumo maalum ya kuwalinda watoto.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine hatuwezi kufundishwa na Taifa lolote jinsi sisi tunavyoweza kukuza mila na tamaduni zetu. Sisi wenyewe tunao uwezo wa kuelewa tunachotaka kukifanya, tunao uwezo wa kuamua namna mahusiano tunaweza kuwa nayo ambayo ndiyo yalijengwa na ndiyo yaliyosababisha sisi tuzaliwe. Kwa kweli tutajenga Taifa zuri kama tutaendelea kuheshimu mila, taratibu na desturi zetu katika mazingira yoyote yale na hapo tutakuwa pia tumelinda imani zetu ambazo sisi sote tunaabudu kwazo na tena kipindi hiki ni miezi mitakatifu kwa kila mmoja. Naomba sana sana kila Mtanzania aone haja ya kuwajibika katika kulinda Taifa letu kwa kutunza mila na desturi zetu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)