Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kwa dhati nikushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, ningependa nichangie maeneo matatu. Kwanza ni suala zima la kilimo katika Mkoa wa Dodoma, lakini suala zima la ukuaji wa viwanda hapa nchini na suala la utoaji wa huduma za elimu na afya hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana nilirudia katika mchango wangu kwa Wizara ya Kilimo kwamba Mkoa wa Dodoma ni lazima uchukuliwe kwa hali ya tahadhari kwa upekee ulionao kwamba hatupati mvua ya kutosha. Kwa kweli tumekuwa wahanga kila mwaka sisi hatupati mvua za kutosha na mwaka huu vile vile hatujapata mvua za kutosha na mwakani hatutapata mvua za kutosha na 2025 hatutapata mvua za kutosha kutokana na hali yetu ilivyo hapa.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa na challenge mara nyingi kwamba tunahitaji tuwe na sera ya kilimo katika maeneo kame ikiwepo Mkoa wa Dodoma. Mkoa wetu nataka niseme Serikali bado inahitaji nguvu kuwekeza. Tunapata mvua kidogo kama nilivyosema, lakini ukija kwenye suala la pembejeo sisi tumekuwa siyo watumiaji wa mbolea kwa utamaduni wetu na ni kwa nadharia mbalimbali. Tunapata mvua kidogo, ukiweka mbolea ile itabaki pale pale juu na mimea itakauka. Kwa hiyo sisi hatutumii hii mbolea ya kemikali na tunatumia mbolea ya chumvi chumvi. Sasa kikubwa tunachofanya tunalima mazao yanayostahimili ukame; mtama mfupi umefanyiwa research unastahimili sana Dodoma unaweza ukachukua miezi miwili tayari ukawa umeiva, lakini mbegu hatupati. Mwaka jana nimefanya kampeni kubwa kwenye jimbo langu kuhamasisha wakulima walime mtama mfupi na tukawaorodhesha wakulima ili kila mmoja apate kiasi cha mbegu anachotaka kulima.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hiyo, hatukupata mbegu. Tumefuatilia kwa wakala wa mbegu na jibu tulilopata kwamba mbegu hamna. Kwa hiyo maeneo mengine wanavyokuwa na utaratibu wa mbolea za bei nafuu za ruzuku kwetu sisi hakuna. Nataka niseme Serikali ilichukue kwa dhati kuona namna gani ya kuinua suala la kilimo katika mkoa wetu. Nachelea kusema tumetelekezwa, kama tumeachwa vile, tunajilimia tu. Kwa Mkoa wa Dodoma, naomba Serikali na hata bajeti inayokuja ya kilimo ioneshe nia thabiti kabisa ya kwenda kuinua kiwango cha kilimo katika mkoa wetu. Fedha inayokuja kwenye bajeti ni fedha ya uendeshaji na uratibu, lakini katika pembejeo bado hatupati kabisa katika kuinua kilimo chetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine Dodoma sisi tunastawisha zabibu na zabibu imekuwa ni mkombozi. Bahati mbaya zao hili limekosa usimamizi na nataka kujenga hoja hapa kwamba kuwe na Bodi ya Zao la Zabibu. Zao la zabibu liko sasa chini ya Wizara ya Kilimo, lakini Wizara ya Kilimo ina mambo mengi, zao hili limekuwa halihudumiwi vizuri. Tuunde Bodi ya Kilimo na hili Bunge wengi wamepita wanaomba Bodi ya Kilimo. Tuna Bodi nyingi za Kahawa, za Chai, kwa nini Bodi ya Zabibu imekuwa ni mtihani mkubwa? Ikishaundwa Bodi itafanya mambo yake, itafuatilia yenyewe kilimo lakini vile vile hata kufuatilia masoko.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la mchuzi wa zabibu, Serikali imekuwa ikitoa fedha kwamba iwezeshe wanunuzi, lakini kuna curtail kwenye suala hili. Wako wanunuzi wanapewa fedha wanazunguka zunguka kununuanunua lakini hawanunui ile zabibu kwa wakulima na hata ule mchuzi kwa wakulima hawauchukui, bali ipo namna wanayoifanya. Wanachofanya wanaagiza concentrate ya unga hapa nchini lakini wanasema tumenunua. Ukiwauliza wanasema Vumi tumenunua kwa wakulima kiasi hiki, Chibelela kiasi, Mpunguzi kiasi hiki. Nenda kaulize mkulima aliowauzia, hakuna. Serikali bado inaagiza, inaruhusu concentrate iingie hapa kwetu nchini. Sasa zabibu itakua? Kwa hiyo suala hili ninachotaka kusema curtail ipo kwenye suala la zabibu na tunaomba Bodi iundwe tuwe na Bodi ya Zao la Zabibu. Nataka niwahakikishie kwamba kilimo cha zabibu kitainuka na biashara ya zabibu itasonga mbele.

Mheshimiwa Spika, suala lingine mwaka jana nilichangia kuhusu kukua kwa kutokutabirika kwa bei ya cement hapa nchini. Wote tunaweza tukachukua historia, sukari imetusumbua sana nchini, lakini kwa sasa uhakika wa bei ya sukari kutokupanda tumeshadhibiti. Kwenye cement bado hivyo hivyo kwamba cement haina uhakika na shida iliyopo ni kwamba ipo kampuni kubwa ina utaratibu wa kufunga kiwanda kwa ajili ya matengenezo na huwa inafunga mwezi wa 11 na bei ndivyo inavyopanda. Suala hili hatuwezi kuruhusu nchi yetu ikaenda namna hiyo. Kwa hiyo tuna uhakika na mwakani tena cement itapanda.

Mheshimiwa Spika, nimepitia kwenye magazeti wiki hii, ipo tatizo kwamba Kampuni ya Twiga Cement inataka kufanya acquisition ya Tanga Cement na bahati mbaya wamepelekana mahakamani, lakini na chombo chetu cha Serikali nacho kiko humo, The Fair Competition. Sasa ninachotaka kukiona katika jambo lile, nimesoma sana makala zile na nimeelewa kwamba anapokuja kuchukua share kubwa, lipo tatizo hili tunaloweza kulipata kama nilivyoelezea la mwezi wa 11. Kwa hiyo hapa tunakuwa na mzalishaji ambaye anaweza kuamua na kupanga bei yeye mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ujenzi wa Taifa letu wananchi kupata nyumba bora, hawawezi wakajenga makazi bora kama bado cement ni bei ya anasa. Kwa hiyo jambo hili naomba liangaliwe na suala hili la sakata kati ya Tanga Cement na Twiga Cement basi tupate maelezo watu waweze kulielewa.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa msemaji taarifa kwamba kwa mujibu wa sheria ya Fair Competition Act sikumbuki ni kipengele gani lakini kimezuia monopoly ya kampuni moja kuwa na market share ya zaidi ya 36. Merger anayoizungumza ya kiwanda hiki kinachotaka kumnunua mwenzake inakwenda kuzidi sheria tuliyoipitisha ya Bunge ya market monopoly. Kwa hiyo kwa namna yoyote lazima Watanzania watakwenda kuumizwa kwenye bei ya cement.

SPIKA: Mheshimiwa Kenneth Nollo unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hii na nimepewa maelezo mazuri ya kisomi zaidi, nilikuwa naongea layman kwa ujumla lakini nashukuru kwa taarifa ya Mheshimiwa Kingu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nataka niipongeze sana Serikali katika ujenzi wa majengo kwa ajili ya kutolea huduma za afya na elimu. Majengo yale tumejenga bahati mbaya kwenye elimu walimu bado hatujapeleka. Zipo shule shikizi tayari tumejenga. Ukienda kule sehemu inaitwa Mangwe Mnarani unaenda Ipole kule Igugule, unaenda Iyumba kule Nondwa majengo yapo lakini hamna Walimu. Hivyo hivyo zahanati nyingi zimejengwa katika vijiji kwenye jimbo langu lakini hakuna wahudumu wa afya. Kwa hiyo, naomba Serikali wananchi wana shauku kubwa ya kupata afya na kama ni majengo wameyaangalia kwa miaka miwili, wameshangaa vya kutosha sasa wanahitaji kupata huduma ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nataka niipongeze kwa dhati Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo. Wamefanya kazi nzuri katika kutuletea mahindi ya bei nafuu. Kwa Wilaya ya Bahi nimekuwa mnufaika mkubwa sana. Kila kata imeweza kupata mahindi yale ya bei nafuu na nataka niseme utaratibu huu kwa kweli sisi ambao nimesema hali ya kilimo bado haijaimarika na mwakani uweze kuendelea, kama nilivyosema mwaka huu hatujapata mvua za kutosha, kwa hiyo Serikali iendelee na utaratibu wa kuweza kutupatia mahindi ya bei nafuu, lakini kikubwa zaidi iweze kuangalia namna gani inaweza kusaidia mkoa wetu katika kuinua kilimo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)