Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii na nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mungu lakini kukupongeza pia kwa kupata nafasi ya kuaminiwa na Bunge kwa ajili ya kutuongoza sisi wenzako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo napenda kuzungumzia mambo machache yasiyozidi matatu. Ningependa nianze na suala la kwanza ambalo kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu liko jambo ambalo amelizungumza katika ukurasa wa 37 linalohusu masuala ya Maliasili na Utalii pamoja na ukurasa wa 46 linalohusu viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu namna bora ya kusaidia utalii katika nchi hii ni pamoja na kuunga jitihada kubwa zilizofanywa na Mheshimiwa Rais katika Filamu yake ya Royal Tour ambayo imetusaidia sana kuleta watalii wengi nchini. Tumekuwa tukisema kila mara juu ya Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Natamani sana kuona bajeti hii tutakapokuwa tunakwenda kuihitimisha Uwanja wa Ndege wa Mwanza uwe umetengewa fedha zitakazokwenda kuujenga na kuukamilisha kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo sababu nyingi za kwa nini tunahitaji uwanja wa ndege wa Mwanza ukamilike. Hivi tunavyozungumza jana kule Arusha ndege ya KLM imeshindwa kutua kwa sababu za hitilafu ya uwanja na kulazimika watalii kwenda kushushwa Entebbe. Mpaka hivi ninavyozungumza inawezekana watalii wote waliokuwa wanakuja Tanzania kwa Ndege ya Shirika la KLM wako Entebbe na hawana namna tena ya kurudi hapa mpaka pale Wizara ya Maliasili na Utalii itakapojipanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yangu ni nini? Laiti uwanja uliopo Mwanza ungekuwa umekamilika na kuwa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege ingekuwa ni rahisi sana kwa ndege ya KLM kutua Mwanza na abiria wote wakaendelea na shughuli za utalii hapa hapa nchini. Kwa hiyo nitoe wito kwa Serikali kwamba jambo hili ni la muhimu na tulitazame upya kuhakikisha kwamba Mwanza ambayo tunaitazama kama hub ya utalii kwa kanda ya ziwa, basi iweze kufanikiwa na kutoa matunda ambayo tunayategemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nilitamani sana nizungumzie habari ya wafanyabiashara ndogo ndogo, Machinga. Niiombe sana Serikali, nafahamu imekuwa na utaratibu mzuri toka Mheshimiwa Rais alipotoa maelekezo wafanyabiashara ndogo ndogo nchini wote walitii na kwenda kwenye maeneo yaliyopangwa. Bahati mbaya sana ni maeneo machache sana yaliyojengwa kwa nguvu ya Serikali, maeneo mengi yamejengwa kwa nguvu za wananchi, wale wafanyabiashara wenyewe, lakini wajibu wa Serikali ilikuwa ni kuimarisha maeneo haya ya kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niiombe sana Serikali, wafanyabiashara na Serikali itazame, yako mambo hakuna sababu ya kuyaunganisha nchi nzima. Ukizungumza habari ya wafanyabiashara ndogondogo nchi hii iko miji ukiitazama tu unaweza ukaichukua hiyo na ukatengeneza mazingira bora yatakayowasaidia wafanyabiashara, Mkoa wa Mwanza, Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla wake, Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Mbeya lakini na hii sio Mkoa kwa ujumla nikisema Mwanza namaanisha Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza per se.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamejenga masoko, lakini mpaka leo masoko hayana namna bora ya kuwasaidia hao wafanyabiashara. Tafsiri yake tunaanza kuwaacha holela na wanaanza kufikiria kurudi kule walikokuwa kwa sababu na wao kule waliko wanatafuta riziki na huwezi kuipata riziki kwenye mazingira magumu. Kwa hiyo nitumie nafasi hii kuiomba Serikali, pale Mwanza walitengewa maeneo ya Igoma kule kwa Ukwaju, wakatengewa Dampo kule maeneo ya Buhongwa, lakini wakatengewa eneo moja pale Mjini Igogo ambalo linaitwa eneo la Mchafukoga. Maeneo haya toka wamejenga wenyewe Serikali ikawekeza nguvu kidogo na sasa tulipopata milioni 500 na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kuipeleka pale Mchafukoga, fedha hii ni kidogo.

Kwa hiyo, niombe Serikali itazame upya, kama tumeamua kuwapanga wafanyabiashara na wamekubali kwenda kwenye maeneo tuliyowapanga, basi ni lazima tuchukue makusudi ya lazima kuhakikisha tunapeleka fedha kwenda kuboresha maeneo waliyopo ili waweze kufanya biashara zao kwa uhuru na wale wanaokwenda kununua wawe na amani ya kwenda kununua kwenye yale masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba masoko yote yako kiholela. Masoko yote hayana ubora wa kumfanya mtu atamani kwenda kununua kwenye yale masoko. Kwa hiyo kwa namna yoyote ile bado tunaendelea kuweka ukinzani kati ya wafanyabiashara na Serikali na tunafahamu halmashauri zetu. Ukichukulia mapato wanayokusanya, ukachukulia fedha inayokwenda kwenye miradi ya maendeleo, hata iweje ukiwaambia wawekeze fedha zingine kwenye kuboresha yale masoko bado haitawezekana na itaendelea kulaumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko hatua ambazo Mheshimiwa Rais alizielekeza na hatua hizi ni mahsusi. Niombe sana tunaposema Mheshimiwa Rais alielekeza maeneo yote waliyopangwa wafanyabiashara, usafiri wa daladala na mwingine utengenezewe mazingira ya kufika pale. Sasa inafika wakati Mbunge unashauri, Mkuu wa Wilaya anashauri, viongozi wengine wanashauri, lakini hakuna utekelezaji, maana yake ni nini? Hawa wafanyabiashara itafika wakati watachoka kwa sababu yale tuliyokubaliana nao hayatekelezeki na kufanya ugumu wa wanunuzi kushuka kwenye yale maeneo na kwenda kununua bidhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana, kwanza zichukuliwe hatua za dharula kuhakikisha maeneo yote tuliyotenga vinajengwa vituo vya daladala kwa lazima na kwa muda mfupi ili kuwarahisishia wanunuzi wafike kwenye maeneo hayo.

Pili, Serikali iwe na uwiano wa kupeleka fedha. Jiji la Mwanza ndio Jiji linaloongoza kwa wafanyabiashara wengi hapa nchini. Tuna wafanyabiashara, machinga, mama lishe na watu wa aina hiyo zaidi ya 12,000. Sasa ukichukua soko na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, tunajenga soko kubwa lakini uwezo wa soko hili utachukua watu takribani 1,400. Kati ya 1,400 ni machinga 200 peke yake ndio wanaweza kukaa humu ndani, lakini Ukwaju kuna Machinga zaidi ya 2,800, ukienda Buhongwa pale kuna Machinga zaidi ya 3,600, ukienda Mchafukoga kuna Machinga zaidi 2,000, lakini mazingira sio wezeshi kuwafanya watu wafike kwenye haya maeneo. Kwa hiyo, niombe sana kama tuna dhamira njema ile ambayo Mheshimiwa Rais ameikusudia na sisi wasaidizi wake tuwekeze nguvu kuhakikisha mazingira haya yanakuwa bora na yanafanyiwa kazi kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba sana kama tunayo dhamira njema, ile dhamira ambayo Mheshimiwa Rais ameikusudia, nasi wasaidizi wake tuwekeze nguvu kuhakikisha mazingira haya yanakuwa bora na yanafanyiwa kazi kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kuhusu TASAF; katika jambo amblao nataka kuishukuru Serikali na kuishauri iendelee kuwekeza nguvu nyingi zaidi ni kwenye mpango mpya wa TASAF ambao unawekeza katika miundombinu ya kudumu kwenye sekta ya afya, sekta ya elimu na sekta ya barabara. Kwa kufanya hivi utakubaliana nami, fedha nyingi ambazo tumeshazitoa kwa watu zaidi ya 14,000 tukitafuta uhalisia na thamani yake leo hatutaupata kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Jenista Mhagama na hata ambapo amemuachia Mheshimiwa Simbachawene leo naamini kazi hii itaendelea. Ukienda pale Nyamagana peke yake tumepata ujenzi wa shule mpya pia tumepata ujenzi wa kituo kipya cha afya. Tumejenga barabara zaidi ya kilometa 416. Huu ni mpango ambao kupitia mradi wake wa OPEC, kama utaendelea hivi utawakwamua sana wananchi kwa ujumla wao wengi kuliko ilivyo hivi sasa inavyokwenda kwa mtu mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nyongeza ninaomba sana awamu ya pili ya OPEC ilitakiwa ianze mwezi huu wa Nne. Mradi huu unataka kusisitiza na nirudie kusema tena

Mheshimiwa Waziri Jenista ulipopita ziara yako wananchi wa Nyamagana wanakushukuru sana, hata leo umemuachia Kaka yako Simbachawene naamini na yeye atakuja kuhakikisha hii awamu ya pili ya mradi wa OPEC ambao tunategemea tupate Shule ya Sekondari kule Kata ya Igoma, tunategemea tujenge barabara nyingine kule ya Mabatini - Kleruu na tunategemea tupate mradi mwingine kwenye eneo lingineā€¦

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mabula.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa hiyo nachotaka kusema naunga mkono mapendekezo ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini tusisitize kupeleka fedha kwenye miradi unganishi ili iweze kuwasaidia wananchi. Nakushukuru sana. (Makofi)