Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu za kusimama hapa kuongea, nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa kwa masuala aliyoyafanya hapa nchini. Afya, elimu, miundombinu, diplomasia, uchumi lakini mimi nitajilenga kwa aliyofanya kwa watumishi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu ameamua kutoa kwa miaka miwili bilioni 26.3 kwa ajili ya ajira za watumishi nchini, pia akatoa bilioni 23.1 kwa ajili ya kupandisha vyeo Watumishi, zaidi ya hapo akaonesha uungwana wa kutoa msamaha kwa wenzetu waliopata janga la vyeti fake, kuachia bilioni 35.2 ziende kuwalipa hawa watumishi siyo jambo dogo ni jambo kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye hotuba Wizara ya Kazi mmetuambia wamekwishalipa wahanga 11,896. Ni kweli hata mimi nimeenda kwenye Mifuko ya Jamii na Mheshimiwa Waziri nilikupa taarifa. Hata hivyo kuna 541 ambao bado hawajalipwa. Mifuko iliniambia hawajalipwa kwa sababu gani? Taasisi, Wizara na Idara za Serikali hazijapeleka viambatisho vyao na vielelezo vyao ili walipwe, kupitia kiti chako, hizi taasisi ambazo zinajua hazijapeleka vielelezo hivyo zipeleke ili hawa wahanga walipwe basi lengo la Mama Samia litimie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza mmekuja na electronic ya kuweza kutoa vibali vya ajira na mmefanya, maana mnasema mmetoa vibali vya ajira 8,000 lakini nina imani hivi ni vibali vy ajira vya wageni. Hivi kweli vyuo vyetu vinatoa wahitimu kila mwaka, kelele zetu hapa imekuwa kwamba hatuna ajira nchini, tunatoa ajira 8,000 kwa wageni! Hili tunaandaa bomu na bomu kubwa. Yawezekana Sheria inasema hivyo lakini ilikuwa ni wakati ule hatujapata wasomi wa kutosha. Kama ni Sheria ndiyo inatupeleka kule, basi tukaibadilishe hiyo Sheria ili vijana wetu wanaomaliza vyuo vikuu waweze kupata hizo ajira.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameongelea kaguzi za kiafya za usalama kazini niwapomgeze, lakini mmefanya kwa asilimia 99 na mkapata ambao walikosea 173 na mkawachukulia hatua. Mngefanya kwa asilimia 100 mngepata wengi zaidi. Mimi kuna viwanda ambavyo nimevizungukia kwa Wilaya ya Temeke, kiwanda kile hauwezi kuweka watumishi. Sitovitaja majina lakini ninyi muende mkavizungukie muone. Watumishi wamefungiwa mule, hakuna hewa, hakuna nini, unauliza kisa ni nini? Wataibiwa. Pale kuna maisha ya watu na usalama wa watu, ninawaomba Wizara ya Kazi mkazunguke mfike asilimia 100 mtagundua mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna suala la kisheria la uanzishwaji wa vyama vya wafanyakazi. Kifungu cha (9) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004, inatoa haki ya wafanyakazi kuunda vyama vya wafanyakazi sehemu zao za kazi na hili ni haki ya Kikatiba. Utaratibu wa kutumia haki hiyo kwa wafanyakazi unasomwa kwenye Sheria Na. 6 ya Mwaka 2004 upo kwenye Kifungu cha 45, ambao unasema sisi tukishaanzisha chama chetu kwa miezi Sita tuna haki ya kuomba kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi ili atusajili lakini pale kumekuwa na mgogoro na Mheshimiwa Waziri tumeshaongea mara nyingi na wengine nawazuia wasiende sehemu zingine nawambia tutaongea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Waziri ninakushukuru sana nilipopiga simu ulipokea kwa haraka sana lakini ukija kuuliza wanasema vyama vitakuwa vingi, si Sheria mmeitunga nyie kwamba vyama kila mmoja ana hiari wakiwa watu Kumi wanaweza wakaanzisha chama chao sehemu ya Kazi? Majibu yanakuwa vyama vitakuwa vingi sehemu za kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye Halmashauri unakuta kuna TALGWU, CWT na TUGHE sehemu moja ya Kazi. Tunachofanya vyama vikiwa zaidi ya kimoja, viwili, vitatu tunaangalia chenye majority ndicho kinaingia kufunga mkataba kuanzisha Baraza la Wafanyakazi. Kwa hiyo, hii haijakatazwa. Ninashauri tu wale walioomba kawapeni. Hivi mtu anaomba kuanzisha chama chake cha wafanyakazi ninyi mnasema lazima muulize chama kilichopo, nani atakubali kije chama kingine? Hakuna atakayekubali! Sasa mkisema mnawauliza hamtapata lakini mtakuwa mnataka kuibua migogoro ya vyama vya wafanyakazi na kwa watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea hapa walipomaliza ukagazi wa afya na usalama, mlitakiwa mtuwekee ukaguzi wa Mabaraza ya Wafanyakazi ambayo sasa hivi yanakaguliwa na CAG lakini sina mahali ninapoona. Ninapozunguka kuna mahali bado Mabaraza ya Wafanyakazi hayafanyiki, na tunajua mabaraza ya wafanyakazi ndilo Bunge la wafanyakazi sehemu ya kazi, ndilo daraja la kujenga mahusianao. Sasa hapa hamjatuonesha kabisa. Sasa niwaombe wakati mnahitimisha mtuambie Mabaraza mangapi yamefanyika? Wangapi hawakufanya kihalali? Pia ni wangapi mmewachukulia hatua kama mlivyosema huku kwenye kukagua usalama na afya kazini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye asilimia 10 ya Halmashauri. Asilimia 10 ya Halmashauri tumeamua Maafisa Maendeleo ndio wawe wafanyaji wa kuangalia mikopo ile na kuwapa watu mikopo Baraza la Madiwani wakishapitisha. Halmashauri zote nilizozunguka, kilio cha Maafisa Maendeleo wanasema waondolewe hiyo kazi, inawafanya wasitende kazi zao, kwanza wanaifanya bila utaalam. Pili, inawajengea mahusianao yasiyo sahihi kwa chini wakirudi kwenda kufanya kazi yao ambayo ni ya kuelimisha jamii, malezi, mahusiano sasa hawawezi kwenda kwa sababu wakienda wanaenda kudai ile mikopo waliyowapa wale wakopaji, kwa hiyo inawaweka kwenye wakati mgumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike wakati sasa tuunde vitengo ambavyo vina wataalam, vina Maafisa Mikopo, vinavyo Wahasibu wa kuweza kuwapa hii mikopo. Yawezekana ndiyo maana hizi hela zinapotea, huyu anaetoa hii mikopo hana utaalam wowote wa ktoa hiyo mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri tu kwenye Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Mmefanya mengi sana Mheshimiwa Jenista nakupongeza na najua ambaye amechukua kiatu chako nae ataenda kufanya hivyo lakini kuna tatizo moja la kutokutoa taarifa. Wasaidizi wenu hawatoi taarifa kumbe communication is power! Leo hii Mheshimiwa Rais alikubali kwenye bajeti ijayo hii tunayoijadili sasa iwekwe bajeti ya kufungua barua za promotion za 2016/2017 lakini nilikozunguka kote watumishi hawajui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nawauliza Maafisa Utumishi sasa kama watumishi wenyewe hawajui, rekodi mmezipata wapi za kuwafanyia bajeti hawa ambao walipewa barua zao wakanyang’anywa? Sasa ni jambo zuri Mheshimiwa Rais amefanya lakini hatulitangazi kuonekana ni suala zuri amelifanya likamjengea mahusiano yeye na watumishi. Ninaomba tukafanye hizo nyaraka zisiwe siri, nadhani nyaraka ikishatoka siyo siri. Zamani tulikuwa tunabandikiwa kwenye kuta mnasoma kilichotolewa kwa sababu ikishakuwa wamei – undergrade siyo siri tena lakini unakuta wanakaa nazo kama siri watumishi hawajui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna mikopo ambayo imepelekwa kwenye Manispaa zamani ilikuwa ni kwa Serikali Kuu, mikopo ambayo watumishi hukopeshwa kununua magari (vyombo vya usafiri) lakini hizi Milioni 300 zinazokwenda kwenye Manispaa watumishi hawajui. Unawambia Mheshimiwa Rais na ninyi amewaletea mikopo mkope mnunue vyombo vya usafiri wanaona kama uinawaletea nahau, hawajui! Sasa unamuuliza Mkurugenzi, unawauliza Maafisa Utumishi mnagawaje hizi hela kama Watumishi hawajui? Hizi kawaida yake hufanywa na Kamati inayoingizwa vyama vya wafanyakazi na Wawakilishi kila Idara kuweza kugawiana hizo hela lakini hawajui. Sasa kwa tafsiri iliyopo ina maana zinafika wakubwa wanagawiana wao mikopo, watumishi wa kawaida hawajui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba hili iende ikafunguliwe. Baada ya hapo naunga hoja mkono. (Makofi)