Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. IDD K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniweesha kunipa afya njema leo kusimama katika Bunge hili Tukufu na mimi leo kuchangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kwa nchi yetu hii ya Tanzania. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitampongeza Mheshimiwa Mama Daktari Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi ambazo ametutunuku wana Msalala. Mama Daktari Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha nyingi katika miradi mbalimbali ikiwemo Huduma za Afya, barabara, umeme, maji, na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianza na afya. Mama Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha ambazo zimetupelekea kujenga kituo cha afya katika kata ya isaka kiasi cha shilingi milioni 500 hajaishia hapo akatuongeza fedha nyingine kujenga Kituo cha Afya Kata ya Morogoro milioni 500, hajaishia hapo ametupatia fedha nyingine kujenga Kituo cha Afya Kata ya Burige milioni 500, hajaishia hapo akatupatia fedha nyingine milioni 400 kujenga Kituo cha Afya Kata ya Segese. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na uhaba wa zahanati katika maeneo mbalimbali ya maboma lakini Mama Daktari Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma zaidi ya 18 ya zahanati ambayo yote yamekamilika mpaka sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambambamba na hilo, ili kuhakikisha ya kwamba tunaondoa upungufu wa watumishi katika maeneo hayo Mama Daktari Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha ambayzo fedha hizo tumeenda kujenga chuo cha nursing na sasa kipo katika hatua ya mwisho ili kianze kutoa hudumahajaishia hapo ametupatia fedha kwenye sekta ya barabara. Mambo mengi sana kwa niaba ya wana Msalala nichukue fursa hii kumpongeza Mama Daktari Samia Suluhu Hassan kwa wema aliotutendea sisi wana Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya lakini kwa hotuba hii ya leo ambayo amewasilisha hapa bungeni. Katika hotuba hii ya Waziri Mkuu imeanisha kwamba ataenda kuboresha miundombinu ya barabara na niseme katika suala langu la barabara hasa niliouliza hapa asubuhi kwenye swali la nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna fedha ambazo zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara inayotoka Buliankhulu inaenda mpaka Kahama lakini pia barabara hiyo inaunganisha kutoka Ilogi kwenda mpaka Geita lakini hivyohivyo inatoka hapo inaenda Nyang’wale inaenda mpaka kuunganisha daraja ambalo linajengwa la Kigogo Busisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii na leo niizungumzie kwa uchungu mkubwa sana kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri leo wakati ananipa majibu yake pia alinipa majibu ambayo hayakuridhisha kabisa. Fedha hizi Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan ameidhinisha kiasi cha Shilingi dola milioni 40, takribani bilioni karibia bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii na fedha hii ipo na toka mwaka jana barabara hii ilikuwa ianze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kuwa na milolongo mingi ya manunuzi, vikao vingi ambavyo havikamilishi ajenda zao bado mpaka tunavyozungumza hivi hakuna mpaka leo tunaambiwa bado makabrasha yanaandaliwa ili mkandarasi watangaze tenda hiyo. Sasa niseme fedha hii tumepatiwa na Mgodi wa Bulyankhulu na niwapongeze sana mgodi wa Bulyankhulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahusiano ya sisi tunaoishi karibu na migodi na wananchi yalikuwa ni mabaya mno lakini niwapongeze sana Mgodi wa Barrick na hasa kupitia maafisa wao wa mahusiano akiwemo Agapiti anafanya kazi kubwa sana. Wameona kuna haja ya kutupa fedha ili tujenge barabara hii kwa kiwango cha lami ili tuondoe vumbi ambayo itapitika kila leo na makinikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaathirika na vumbi, wameamua kutenga fedha kwa ajili ya kujenga barabara hii, lakini leo kumegeuka sasa Wizara ya Ujenzi kumegeuka kuwa ni sehemu ya kutafuta sijui ni nini lakini kila siku ni vikao wameanza vikao vya kwanza tumekaa kila kata tukamaliza wakaja wakafanya tathmini wamemaliza, wamerudi tena wanasema wanataka warudie wafanye review ya upembuzi yakinifu wamemaliza na wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii hawataki kutangaza Barabara hii na fedha ipo, mgodi huo madini yakipotea tutapata wapi fedha? Tumepewa fedha za wahisani tujenge barabara Mheshimiwa Naibu Waziri unakuja kusimama hapa majibu rahisi kabisa mpaka leo hamjatangaza nini ambacho kimewafanya ninyi msitangaze barabara hii? Fedha zipo siyo kwamba hazipo hata leo mkileta certificate wanalipa wale watu. Fedha zipo cash kwa nini hamjengi Barabara hii wananchi wanaendelea kuumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara hii ni nguzo ya uchumi katika kuunganisha Geita toka Mkoa wa Geita mpaka shinyanga lakini leo nimezungumza hapa nikasema kahama ndio kitovu cha uchumi kanda ya ziwa. Unapozungumzia kanda ya ziwa huwezi kuiacha Kahama. Kuna wafanyabiashara wakubwa wanahitaji kusafirisha watu wanahitaji kuleta mali kutoka geita wanahitajikuleta mali kutoka Kagera na maeneo mengine. Barabara hii fedha zipo leo mtatuambia nini nani kachelewesha? Leo mnaniambia dakika ya mwisho naulizia wanabadilishana kukaa vikao naambiwa leo wameitana tena wanataka kwenda kukaa Dar es salaam kikao cha nini? kila siku mnakaa vikao kama vikao vya harusi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inauma, vikao vimekuwa ni vingi sana. Vikao vile vinatumia posho fedha ile itajenga Barabara lini? Fedha ipo wananchi wanaumia niombe Mheshimiwa Waziri Mkuu atakaposimama hapa kufanya windup ya hili atueleze ni lini hasa barabara hii itaanza kujengwa kwa sababu fedha zipo hakuna kinachoshindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inauma sana leo nimezungumza kwa uchungu sana kwa sababu ninaona kuna uzembe mkubwa unafanyika kwenye maeneo haya hasa Wizara ya Ujenzi. Barabara nyingi ukiangalia, kuna barabara zinachelewa kujengwa na ukiuliza tatizo ni nini wanakuambia tatizo ni eidha ni hatua za manunuzi kwa nini tusizipitie upya hizi hatua za manunuzi? Ukiuliza unaambiwa bado kuna changamoto ya kupata tax exemption kwa nini hawa watu wa TRA wasikae pamoja na watu wa ujenzi wakaorodhesha barabara zote kama kikwazo kama ndio kupewa msamaha wa kodi wangalie ni namna gani wanaweza wakafanya ili kutoa msamaha wa kodi haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inauma sana kuona watendaji wanakuwa wazembe kiasi hiki. Mheshimiwa Rais anapambana kutafuta fedha, anaenda nje kutafuta fedha anatuletea fedha, anajitoa kuzungumza na wahisani mbalimbali leo watu wanakuja wanataka kutusaidia lakini watendaji wanamwangusha Mheshimiwa Rais. Ni katika shilingi nitakapokuja kuchangia Wizara nitashika mshahara wa Mheshimiwa Waziri mpaka atuambie ni lini barabara hii itaanza ujenzi kwa sababu fedha hizo tunazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia kwenye suala zima la TARURA amezungumza Mbunge mwenzangu hapa. Wilaya ya Kahama ndio wilaya kubwa inawezekana kuliko wilaya zote hapa Tanzania. Ukiangalia Mkoa wa Shinyanga ndio unaweza kuwa ni mkoa mkubwa lakini una wilaya chache kuliko zote hapa Tanzania. Mkoa wa Shinyanga una wilaya tatu tu lakini una halmashauri sita, sasa niombe TRA wamefungua Mkoa wa Kikodi Kahama, watu wa amdini wamefungua Mkoa wa Kimadini Kahama, niombe kwa nini hawa watu wa TARURA nao wasifungue Mkoa wa Ki-TARURA Kahama? Lakini pia tulikuwa na hawa Mameneja kwenye halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kahama ina vijiji zaidi ya mia tatu na ishirini na kitu, leo kama Mkuu wa Wilaya akianza kutembelea kila Kijiji maana yake ni kwamba mwaka mzima yeye asifanye shughuli nyingine wala kwenda likizo anatembelea tu vijiji. Kwa nini hawa Mameneja wasirudishwe ili waweze kutoa huduma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mvua zinaendelea kunyesha tunapokea malalamiko kwenye maeneo yale utaona barabara zinakatika, watu wanataka kurekebisha barabara lakini ukiuliza hatua za manunuzi hivi haya manunuzi hamuwezi mkayaleta hapa tukayapitia tukaona njia rahisi ya kurekebisha? Leo utaanza kuona tunapitisha bajeti mwezi wa saba mwezi saba akaunti zimefungwa mfumo bado tunaenda tunatangaza tenda, tunatangaza tenda hatua za manunuzi, manunuzi, manunuzi, mpaka mkandarasi anaenda site mwezi wa pili mvua zinanyesha barabara haitengenezwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan anatafuta fedha nyingi anatuletea, changamoto siyo fedha kwenye maeneo yetu kwa sasa fedha zipo lakini changamoto utaambiwa tulitangaza barabara hii mkandarasi hakupatikana, hakupatikana alienda wapi? Wanasema tumetangaza barabara hii hatua za manunuzi bado, bado kivipi? Wakati meza zipo? Niombe sana Wizara ya TAMISEMI hebu oneni namna ya kuweza kuona namna ya kurudisha mfumo ambao uliokuwepo wa Mameneja Wilaya ya Kahama ni wilaya kubwa mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyohivyo niendelee kuomba ikiwezekana basi tuone namna ya kugawa utawala mtuongezee hizi halmashauri, Halmashauri yangu ya Msalala, Halmashauri ya Usheto na Halamashauri ya Manispaa ya Kahama hizi zote zinajitegemea kiuchumi na uchumi wao ni mzuri, kwa nini tusipatiwe wilaya kila sehemu tukajitegemea? Kwa sababu halmashauri yangu ni halmashauri lakini ukilinganisha na wilaya zingine inawezekana kiuchumi Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ikawa iko vizuri kuliko wilaya zingine ambazo zinaendelea hasa niazoziona za Jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza sana kwenye suala zima la barabara naumia sana, kwenye umeme nitakuja nizungumze kwenye Wizara ya umeme lakini niombe hii barabara ni changamoto kubwa sana na narudia tena kwa sababu ni barabara ambayo kuna uzembe na ikiwezekama watu wawajibike kwenye hili, nani amekwamisha? Nani kashikilia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaniumiza sana kuona fedha tunazo kwenye maeneo mengine wanalia kila siku Mheshimiwa Naibu Waziri anatuambia ikipatikana fedha Serikali itajenga sasa fedha imepatikana kwa nini hamjengi? Kama fedha ikipatikana leo ipo Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii na Katibu Mkuu niwaombe sana punguzeni vikao. Ikiwezekana CAG nimuombe kwenye ripoti inayokuja achunguze hivyo vikao vinavyo kaa kaa hivyo vikao vinatumia fedha kutoka mfuko gani? Kwa sababu vikao vimekuwa vingi haviishi kutangaza barabara mbona barabara zingine hazina vikao vingi kama hii barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaozalisha dhahabu ukiangalia mgodi wa Buliankhulu na jimbo langu la Msalala ndio jimbo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa sana kwenye mfuko wa taifa. Leo hii utaona kwenye wizara ya madini tunalipa reality asilimia saba na niendelee kuomba Mheshimiwa Waziri yupo hapa ananisikia Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe sana watu tunaotoka kwenye maeneo ya madini maisha yetu ni duni, hayafanani na vile ambavyo tunazalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe ikiwezekana kwenye asilimia saba ambayo tunalipa mrabaha asilimia saba ambayo makampuni yanalipa mrabaha niombe asilimia mbili iweze kubaki kwenye maeneo hayo ili tuweze kujenga miundombinu yetu wenyewe kwenye maeneo yale bila kutegemea fedha kutoka Serikali kuu, uwezo huo tunao kwa sababu fedha zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea kwa uchungu sana nafikiri nisiharibu niishie hapo lakini niombe na niombe nitashika shilingi kama barabara hii haitaanza kujengwa kwa sababu fedha zipo, ahsante. (Makofi)