Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi niweze kuchangia Hotuba hii ya Waziri Mkuu iliopo mbele yetu, lakini niombe Mawaziri wanapokuwa wanatoa taarifa wakati wana muda wa kujibu wanatuchukulia muda wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza kwa kutoa pole kwa wananchi wangu wa Kata ya Kilando na Itete ambao wamepata mafuriko nikiwa hapa, zaidi ya kaya 500 na hatujui leo wanachi wangu watalala wapi. Niwape pole sana wananchi wangu lakini nianzie kwenye hilo hilo. Kumekuwa na uzito sana kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kunapotokea majanga kuchukua hatua. Hilo jambo limekaa kinadharia sana kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu na ni vizuri kama Bunge tukajua utaratibu mwingine ambao unatumika inapotokea majanga na namna ya kuwasaidia Watanzania, kuliko ambavyo ipo sasa kwenye maandishi lakini kwenye utekelezaji haipo ni sifuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na kwenye sekta za uzalishaji. Sekta za uzalishaji nitajikita kwanza kwenye suala la uvuvi. Mkoa wetu wa Rukwa uvuvi kwetu ndio uchumi na kilimo ni uchumi. Kwenye sekta pekee yake ya uvuvi ukitilitazama Ziwa Tanganyika tuna-share zaidi ya nchi tatu lakini taarifa tulizonazo mpaka sasa ni kwamba wanategema kufunga Ziwa Tanganyika na hili jambo limeleta tension kubwa sana kwa Watanzania ambao wako kwenye mikoa ambayo ipo kwenye Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufunga ziwa kwa sababu ambazo Wizara wamefanya tafiti sio jambo baya. Mara zote tumekuwa tunapishana na mitazamo ya wasimamizi au Mawaziri waliopo kwenye sekta hizi kwa mambo yafuatayo; kwa sababu kuna watu ambao wamekopa mikopo leo kwa sababu ya shughuli ya uvuvi ukifunga Ziwa Tanganyika wakati hao wavuvi wamekata leseni ya mwaka mzima, hao wavuvi mikopo hiyo wanategemea wavue ili waweze kulipa hiyo mikopo, ukafunga ziwa bila kutengeneza njia mbadala ya wao kupata fedha na kuendesha Maisha yao, unakwenda kutengeneza vibaka kwa makusudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la kufunga ziwa kwa taarifa ambazo zinasikika kwa sababu hata Mbunge sijaambiwa wala sijashirikishwa. Wanasema eti samaki wamepungua, ukifunga ziwa kwa miezi mitatu, Samaki wanaenda kuongezeka? Kwa nini Serikali isije na mkakati wa makusudi wa kuzuia uvuvi haramu uliosababisha samaki kupungua? Mnakuja na sababu nyepesi ya kufunga ziwa kwa miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kama nia ni njema ya Serikali ya kusaidia haya maziwa yawe endelevu kwa vizazi na vizazi. Cha kwanza wangeanza kuwapa elimu na kuwasaidia nyenzo wavuvi wetu kuanza kufuga samaki ili hata kwa kipindi hiki angalau cha hiyo miezi mitatu cha mpito wawe na njia mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kama ndivyo tunataka tutekeleze hili jambo vizuri Serikali kwamba ikatoe elimu kwa wavuvi hawa, hii kazi sio haramu na ndio maana wamelipa leseni. Lazima muende kule muwaambie wavuvi kwa nini mnafunga ziwa? Na kwa sababu mnafunga ziwa mmewaandaliaje mazingira ya wao kuishi na kulipa mikopo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na hapo ni jambo la ajabu sana ambalo linakwenda kufanyika hivi sasa. Leo watu wa Mwambao wa Ziwa Tanganyika, wale uchumi wao, maisha yao ndio uvuvi kwa hiyo ukifunga hilo ziwa hawana eneo lingine la kuweza kujisaidia na kusaidia watoto wao. Naomba sana kama hilo jambo ndivyo lilivyo basi Serikali itafakari kwanza athari ya hili jambo ambalo wanaenda kuchukua. Kwa sababu hata ukifunga miezi mitatu kama umeshindwa kudhibiti uvuvi haramu baada ya miezi mitatu watakuja tena wavuvi haramu utakuwa umefanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe wataalamu wetu wasiwe wanatoa sababu nyepesi kwenye mambo magumu. Waje na mikakati ambayo itawasaidia Watanzania wote, ni kweli tunatambua faida watapokuwepo Samaki wengi hata wale wavuvi watanufaika. Lakini hii miezi mitatu hii fedha ambayo mnaenda kuitumia kufanya patrol, kwa nini msiitumie kufanya patrol ku - control huo uvuvi haramu badala ya kusubiri hicho kipindi ambacho hamtaki wavuvi waende. Lakini mtuambie kama mtafunga kwa hiyo miezi mitatu ile leseni ambayo wamelipia mwaka mzima itakuaje? Mtawalipa fidia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kwa kuwa wavuvi wanapoambiwa wanaelewa, waende kwanza wakazungumze na wavuvi, wakishazungumza na wavuvi wavuvi nao watawaambia kwa nini miaka yote huko nyuma hawajawahi kufunga ziwa. Ziwa Tanganyika linajifunga automatically muda wa Samaki wanakwenda wanavuliwa…

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi ambacho sio cha msimu wa kuvua samaki wanaondoka…

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

T A A R I F A

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru lakini nilikuwa nataka, moja nimpe comfort Mheshimiwa Aida Khenani, kwamba alishalizungumza hili jambo na Ofisi yangu na baada ya kulizungumza tumekubaliana ya kwamba ziko hatua tunazokwenda kuzichukuwa. Miongoni mwa hatua ambazo tunakwenda kuzichukua ni pamoja na kukaa na Waheshimiwa Wabunge wa mwa mwambao wote wa Kanda ya Ziwa Tanganyika, Mikoa mitatu yote Kigoma, Rukwa na Katavi, lakini pia vile vile tutakaa na wawakilishi wengine wa wananchi ili tuelewane na dhumuni la Serikali kwenye jambo hili si baya lakini kama anavyosema nia ni kupata uelewa wa pamoja na tukienda twende kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo namuomba katika mchango wake pamoja na kwamba anatoa mchango mzuri wa kutukumbusha juu ya umuhimu wa wananchi kuendelea na shughuli yao lakini pia ajue kwamba ziko hatua Serikali inaendelea nazo ili kutokuleta taharuki kwa wananchi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Khenani unapokea taarifa?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea ni taarifa njema kwa sababu amesema na nasubiri utekelezaji wa hayo maneno yake na ni kweli tumeshazungumza na ofisi yake lakini mpaka sasa hatujaona chochote kinachoendela na presha ni kubwa sana kwa wananchi wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ndivyo basi nishauri ushirikishwaji uwe wa kutosha, yaani ushirikishwaji kikamilifu sio wa juu wa juu najua wananchi wakielewa hata utekelezaji wake utakuwa ni mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee, Serikali imejenga bandari, imejenga Bandari Kalema, Kabwe, Kasanga, Kigoma ukitazama hizo bandari Serikali ilikuwa inategemea kupata matokeo chanya kupitia hizo bandari na kama ndivyo hatuwezi kuwa na bandari wakati mazao ambayo yanatakiwa yasafirishwe kwenda Congo hatuna meli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu ambavyo ndio uwekezaji ambao tunauzungumza leo ni uwekezaji gani huu? Unawekeza bandari huna meli unategemea meli ya nani sasa iwezekuja kubeba hiyo mizigo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Waziri alichukuwa muda wangu nimalizie kwa dakika mbili.

MWENYEKITI: Sekunde 30 Mheshimiwa malizia.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri suala la MV Liemba imeshabaki ni historia, tupewe majibu ya meli ya mizigo na abiria si hizi stori ambazo zimekuwepo muda wote na hili jambo litawasaidia wananchi wa Mkoa wa Rukwa na itainua uchumi Mkoa wa Rukwa na mikoa yote ambayo inazunguka Ziwa Tanganyika, ahsante. (Makofi)