Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi japo sijafahamu ni dakika ngapi natakiwa kuchangia lakini itoshe tu kusema kwamba nami napongeza Ofisi ya Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri na kwa utendaji mzuri, pia kwa kwake Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi alivyokuwa mtu rahimu na mtu ambae anafikika hata ukiwa na jambo kwa ajili ya wananchi wako anakusikiliza na linapata ufumbuzi pale ambapo kuna changamoto. Kwa hiyo nawapongeza sana yeye na Mawaziri wanaofanya kazi katika Ofisi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa siyo mwingi wa fadhila kama sitampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo inafanyika katika sekta zote muhimu za afya, elimu maji na barabara, kama alivyosema Mheshimiwa Seif kweli kabisa Mheshimiwa Rais anaupiga mwingi. Anaupiga mwingi kama Mayele lakini pia anaupiga mwingi kama Clatous Chota Chama. Sasa ukichanganya hapo unaweza kuona ni jinsi gani mambo, yaani unajaribu ku-imagine Chama na Mayele mambo yanavyoweza kuwa mazuri. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa sababu mimi ni mwanamichezo naomba pia nitumie nafasi hii kuwapongeza Simba na Yanga kwa kufika hatua ya robo fainali, kwa sababu tumesema kwamba mpira na michezo kwa ujumla ni ajira ni biashara ni uchumi. Ninapenda pia nitumie nafasi hii kuwakumbusha tu Watanzania kwamba Simba hii ambayo imepangiwa na mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika ilishawahi kupangiwa na mabingwa watetezi Zamalek mwaka 2003 na ikawatoa pale pale Cairo – Misri kwa mikwaju ya penati tatu kwa mbili baada ya kuwa wametoka moja bila Simba wameshinda kwa goli lililofungwa na Ndugu Emmanuel Gabriel dakika ya 56 lakini walipoenda kule Simba wakafungwa moja ikabidi waende kwenye changamoto ya mikwaju ya penati na Simba wakawang’oa Zamalek. Kwa hiyo, kama ambavyo tumepangiwa Mabingwa Watetezi vilevile watu waweze kujua kwamba tumejipanga vizuri tunaweza tukalitangaza Taifa na tukatangaza utalii wa nchi yetu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nampa taarifa mchangiaji anatueleza historia sana lakini ninataka kumwambia ukizungumzia kikosi bora ni cha Young Africa na nimhakikishie kwenye mechi tunayokutana na Simba tutawafunga nasi kama tunaongoza group Nigeria tunaenda kushinda. Tunaenda kuwaonesha, tunaenda kushinda ugenini. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Chumi taarifa unaikubali?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa muktadha ufuatao, kwamba maisha ni historia, leo yetu imetengenezwa na jana na kesho yetu itatengenezwa na leo kwa hiyo nakubaliana nae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo napenda kutumia nafasi hii kuipongeza sana Serikali katika suala zima la mbolea na ruzuku ya mbolea, kwa kweli Serikali imetusaidia sana. Serikali ilikuwa sikivu tulijenga hoja na kwa kweli wakatuwekea ruzuku. Hata hivyo, kumekuwepo na changamoto ya hapa na pale katika upatikanaji wa mbolea ile ya ruzuku. Kwa mfano, mbolea kutofika vijijini kwa wakati, pia changamoto za stika watu wanaenda stika zinakuwa bado, wakati mwingine wanaenda wanaambiwa kwamba stock haijasoma na kadhalika, lakini ni changamoto ambazo ni manageable tunaamini kwamba msimu ujao tutafanya vizuri zaidi. Kwa hiyo, ili tuboreshe suala zima la upatikanaji wa mbolea nina mambo machache ya kushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nashauri ule usambazaji walau uende mpaka ngazi ya Kata. Pili, ninashauri ujazo wa mbolea iwe na ujazo tofauti tofauti. Wapo wakulima wengine wanahitaji ujazo wa kilo tano, wengine kilo 10, wengine kilo 20. Isiwe tu mbolea ya ruzuku mifuko iwe ni ya kilo 50 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba upatikanaji wa mbolea uwe ni kwa mwaka mzima. Nikisoma hapa katika taarifa ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 31, kiasi cha takribani shilingi bilioni 284 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa scheme za umwagiliaji. Maana yake ni kwamba, sasa tunaenda kujidhatiti katika kilimo ikiwemo kule Mtula kwamba tutalima mwaka mzima. Kwa hiyo, kama tutalima mwaka mzima maana yake ni kwamba nashauri mbolea ya ruzuku pia ipatikane mwaka mzima, tusisubiri tu wakati ule ambao msimu unaanza, kwa sababu tume- encourage wananchi wetu walime mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, watu wa Iringa, Njombe tunalima kile kilimo cha mabondeni, kilimo cha vinyungu ni mwaka mzima. Tukimaliza sasa hivi kulima hichi kilimo cha kawaida tutarudi kilimo cha mabondeni pamoja na kuwa tunazingatia kutunza vyanzo vya maji. Kwa hiyo, ushauri wangu mbolea ipatikane mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama ambavyo tumetoa ruzuku kwenye mbolea, Wananchi wa Mafinga nilipofanya ziara wameshauri kwamba pia mbegu nazo zipatikane mbegu za ruzuku ili kusudi vyote hivi viweze kusisimua kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine tumeelezwa hapa kuhusu usalama wa chakula, lakini usalama wa chakula unaendana pia na usalama wa upatikanaji wa mbegu. Mimi nilikuwa nashauri hebu pamoja na taasisi yetu ya utafiti wa mbegu tuvishirikishe vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hususan Jeshi la Kujenga Taifa katika kufanya tafiti za mbegu. Kwa sababu baadhi ya mbegu ambazo tunaletewa ni zile mbegu ambazo mwaka huu ukipanda mwakani haiwi kama zamani ambavyo tulikuwa tunatumia lilelile zao umepanda mwaka huu mwakani ukivuna baadhi ya sehemu ya mazao unatumia kama mbegu. Kwa hiyo, nilikuwa napenda kushauri hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa sababu ya muda ni suala la TARURA. Kweli tunawapongeza kabisa kunatengwa bajeti, kama mimi hapa Mafinga mwaka 2021 tulikuwa tunapata shilingi milioni kama 900 lakini 2022/2023 tunapata mpaka shilingi bilioni 2.3 na tunatarajia itaenda kuongezeka. Kama alivyosema Mheshimiwa Iddi kumekuwa na shida kubwa sana na changamoto ya Wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mafinga kwa mfano, kuna barabara ambayo Mkandarasi ilikuwa atukabidhi Tarehe 04 mwezi Machi lakini mpaka hapa ninapozungumza ameshakamatwa na TAKUKURU, ameshahojiwa na Mkuu wa Wilaya, ameshaitwa kwa Mkuu wa Mkoa, ameshaitwa mpaka kwa viongozi wa chama, nothing is going on. Kwa hiyo, nashauri wakati Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla inatenga fedha kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo, wako watu au baadhi ya Wakandarasi ambao siyo waaminifu wanapewa kazi lakini hawazifanyi kwa wakati, ambapo kimsingi wanakwamisha au kuchelewesha maendeleo ya wananchi. Kwa hiyo, ninashauri Serikali tutafute namna ikiwezekana tuwe na Wakandarasi wachache au kama hawana nguvu ya kifedha basi tuwatafutie mechanism ya kuwapa mikopo kwa namna ambayo itawezesha wao kufanya kazi kwa wakati na kwa ufanisi ili kusudi zile fedha na zile shughuli ambazo zimepangwa ziweze kufanyika, kwa sababu it is very embarrassing kwamba mtu kapewa kazi anatakiwa akabidhi Tarehe 04, Machi, mpaka leo ninavyozungumza tarehe 06 Aprili, amefanya kazi asilimia 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo vyote vya Kiserikali including Chama cha Mapinduzi kimechukua kila hatua, nothing is going on. Sijui tunafanyaje maana sasa tunasema tusije tukawa tu Taifa la kulalamika ndiyo maana nashauri tutafute namna ambayo Wakandarasi wa namna hii pamoja na kuwachukulia hatua, tuone Je, kuna namna gani kama Taifa tunaweza kuwajengea uwezo Wakandarasi wetu wanaopewa kazi za ndani ili fedha ile tunayopitisha hapa Bungeni ikafanye kazi ambayo imekusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo naomba kuunga mkono hoja, nikisisitiza na kurudia kwamba kuhusu suala la mafuta ya kula bado nasisitiza na kushauri tufanyeni kama trial tuwape JKT miaka miwili tuwawezeshe, tuone kama hatujajitosheleza kwa mafuta ya kula tukaokoa fedha za kigeni hizi ambazo kila mwaka tunatuma kununua mafuta ya kula hapa nchini, huo ndiyo ushauri wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu atubariki wote, aibariki Simba na Yanga na awabariki Watanzania kwa ujumla. (Makofi)