Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Lucy Thomas Mayenga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama hapa. Lingine kwa kweli leo ni siku ambayo nina amani sana na furaha kubwa, kwa sababu naichangia Wizara ambayo inaonesha kwamba watu wapo serious. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi ambao ni Wabunge Mawaziri wote hawa tunawaona, tunajua kila mtu utendaji wake ulivyo. Vipo vitu ambavyo kuna Waziri anaongea, hata maswali wananchi wanatutuma, tunakuja hapa tunauliza, Waziri akidanganya tunajua, Waziri akifanya siasa tunajua na Mawaziri ambao wapo serious pia tunajua. Wizara hii ya Kilimo ni Wizara ambayo ipo na watu serious kupita mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Wizara zangu chache; Wizara ya Kilimo, Wizara ya Madini, nyingine siwezi kuzisema leo lakini hizo naamini kwamba zipo na watu serious na lazima niwapongeze watu hawa kwa sababu kazi kubwa na hali halisi ya maisha ya wananchi wetu inajulikana. Wananchi wetu wana shida sana kule, vipo vitu vingine tukikaa kupongezana na kusifiana sana mambo kule yatakuwa hayaendi. Mwaka 2025 itafika wakati sasa tunakaa tunaanza kutafutana, tunabembeleza, tunapiga magoti tunaonekana kwenye magazeti haipendezi. Kwa hiyo, kwa Mawaziri ambao wanafanya kazi vya kutosha na kwa kiwango cha juu, ni lazima tuwapongeze. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nakubaliana na dada yangu Lucy Mayenga kwamba ni kweli mawaziri hawa vijana wanafanya kazi, lakini jukumu letu kama Bunge ni kuhakikisha Wizara ya Fedha tunaibana ili wawapelekee hawa Mawaziri fedha wakabadilishe maisha ya watanzania ambao asilimia 80 ni wakulima. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mayenga unapokea taarifa?

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Taarifa hiyo si mbaya, naipongeza kwa sababu pesa ndiyo kila kitu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais wetu, kwa kweli huyu mama anafanya kazi kubwa sana, nasema hivi kwa sababu hata kwenye Wizara hii tumeona kiwango cha pesa bajeti ya Wizara hii kwa mara ya kwanza imefika shilingi bilioni 751 haijapata kutokea. Kwanza ameonesha kuwathamini sana wakulima, lakini amewaheshimisha… (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mayenga imefika bilioni 700, bilioni weka takwimu vizuri.

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema bilioni 751.

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sawa. Imetoka bilioni 200 mpaka bilioni 751, lakini Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara hii wameweza kupandisha, yapo maeneo ambayo tunajua kabisa kwamba ukiyagusa, kama tunavyojua kwamba kilimo kinamgusa mwananchi kwa asilimia 100. Maeneo ya utafiti, maeneo ya hawa ndugu zetu Maafisa Ugani, maeneo ya maendeleo yote katika Sekta ya Elimu yamepandishwa kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano kwenye utafiti; kutoka bilioni 7.0 mpaka bilioni 11.6; kwenye huduma za ugani bajeti imepanda kutoka milioni 603 mpaka bilioni 11.5; kwenye umwagiliaji kutoka bilioni 17 mpaka bilioni 51; ni mabadiliko makubwa sana na kwa kweli kwenye hili tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii Naibu na Watendaji wote. Kama ingekuwa kuna uwezo Waziri mmoja na watendaji wake na hii timu ya Wizara ya Kilimo kuhudumia Wizara mbili, kuna Wizara ningependekeza kama iende huko pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze mama yangu Mwenyekiti wa Kamati hii. Ni mama ambaye amekuwa anafanya ziara kwa vitendo na kwa kweli Kamati hii imekuwa ikifanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo matamko mengi sana ya historia ya kilimo katika nchi yetu, imeanza kwa mambo mengi sana. Awamu ya Kwanza naya Nne wao walijikita kwenye masuala mazima ya uzalishaji; Awamu ya Pili na Tatu wao walijikita kwenye Muundo wa Taasisi pamoja na mifumo mizima ya kilimo; Awamu ya Tano iliyopita ilijikita kwenye kuboresha masuala mazima ya kuongeza thamani ya mazao, uzalishaji lakini na pia vilevile kuweka miundombinu bora kwa ajili ya kusaidia kilimo chetu katika mazao ambayo yanapatikana yaweze kusafirishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ambayo nataka niyazungumzie, tunazungumza kwamba kwenye sekta hii, zipo pesa nyingi sana. Wizara hii Mheshimiwa Waziri kaka yangu Bashe amepewa fedha nyingi sana na fedha hizi naomba awe mkali sana. Nasema hivi kwa sababu moja kati ya tatizo kubwa sana ambalo limekuwa likitokea hapa nchini kwetu, ni kwamba bado baadhi ya watu ni kama wanataka ku-test test mitambo hivi, bado hawaamini kwamba kula fedha ya Serikali ni kosa na unaweza kuchukuliwa hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali au Wizara hii ijitahidi sana kusimamia pesa hizi kwa sababu kule kwa wananchi kilimo ni kinachukua asilimia 70 ya Watanzania. Kwa hiyo, bila fedha hizi kusimamiwa ipasavyo maendeleo na yale matokeo ambayo tunahitaji hatutayapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuzungumzia, kuna Miradi ya Umwagiliaji katika Wilaya yangu ya Kishapu, ipo Miradi ya Umwagiliaji katika Kata za Mwadui, Lohumbo Itilima na Talaga, kuna skimu za umwagiliaji. Naomba Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu mkubwa, ikiwezekana tuweze kupata fedha pale. Katika skimu ya Umwagiliaji ya NIDA ambayo ilikuja mwaka 2020, namshukuru sana Wazii alikuja pale Shinyanga Vijijini baada ya kelele nyingi sana za kaka yangu Mheshimiwa Ahmed, Mbunge wa Jimbo, alikuja akasikiliza shida zetu na akatuelewa na nimpongeze na nimshukuru kwamba ametupatia fedha kwa ajili ya skimu hiyo ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia atusaidie skimu ya umwagiliaji ya kwenye Kata Uhendele ambayo ipo kwenye Manispaa ya Kahama Mjini. Kuna Mheshimiwa Diwani wetu pale anaitwa Justin Sita amekuwa akipiga kelele kila mara kwenye kila kikao kwamba mradi huu uweze kupata fedha, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie. Miradi hii endapo kama itafanikiwa, itasaidia akinamama. Watu wanategemea miradi hii ikifanikiwa maji yale yaweze kulisha mifugo pamoja na akinamama waweze kupata maji kwa ajili ya matumizi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho; naomba kusema hivi, naomba tumpe Mheshimiwa Rais wetu muda. Mheshimiwa Rais wetu ameingia katika kipindi ambacho kina changamoto nyingi sana, endapo sisi wanasiasa tutakuwa tunakaa katika kila kitu kwa kuangalia dosari, kuangalia hapa amefanya hivi, kwa kuangalia kukosoa, hatuwezi kumpa moyo Mheshimiwa Rais wetu. Tumpe muda tukae, kama ambavyo tulikuwa tumeanza mwezi Januari, Februari, Machi mpaka Aprili maneno yalikuwa mengi mengi, lakini juzi amekuja amefanya jambo la maana, maneno yamekuwa mengi ndivyo Watanzania walivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kumpa moyo Mheshimiwa Rais, afanye kazi, ameingia kipindi kigumu, kipindi ambacho kina matatizo mengi, matatizo ya vita ya Urusi, UVIKO na mengine mengi, lakini naomba nimpe moyo, tupo pamoja naye hata kama kuna wanasiasa ambao tunawasikia wanaongeaongea vitu ambavyo havieleweki, sisi tupo pamoja naye na naomba wanasiasa hao washindwe na walegee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)