Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. BONIVENTURE D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu kwa namna ya pekee ambavyo wamelichukulia suala la Wizara ya Kilimo kwa mtazamo si msimamo. Nchi zote duniani viongozi ili tupate mabadiliko lazima tuwe na mitazamo kuliko kuwa na misimamo. Kwa hiyo, hili Mheshimiwa Waziri ameliweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mazao matano ya kimkakati ambayo Waziri Mkuu aliyasimamia ili kuondokana na adha mbalimbali ambazo wananchi wetu wanazipata. Leo ukienda kule mitaani mfumuko wa bei wanalalamikia mafuta ya kula, mfumuko wa bei wanalalamikia sabuni. Sasa sisi tunayo mazao ambayo yanaweza kumaliza tatizo hili. Zao la kwanza; zao la michikikichi hili linatoa mafuta pamoja na sabuni. Kama tutalisimamia na kuliimarisha tutaondokana na tatizo hili kubwa ambalo wananchi wetu wanaendelea kuwa nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la pamba pamoja na zao la alizeti, hizi zote ni mbegu ambazo zinatoa mafuta ambayo wakulima wetu na wananchi wanaweza kupata mahitaji muhimu zaidi. Zao hili la pamba na alizeti ni mazao ambayo yanalimwa kila mwaka, ni mazao ambayo yanahitaji mvua ya kutosha. Nipo kule Magu nimeona mazao ya pamba pamoja na alizeti ambavyo yanakabiliwa na ukame wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kutoa hapa mchango kwamba tunayo mabonde, tunayo maziwa, tunayo mito, tutumie kwa ajili ya umwagiliaji, hapa ndipo ambapo wawekezaji ambao wanatafutwa na Wizara mbalimbali kuja kuwekeza hapa Tanzania, waje wawekeze miundombinu ya umwagaliaji ili wananchi wetu waweze kulima, waweze hata kuchangia kulipa hiyo miundombinu. Tukifanya hivyo, tutaondokana na adha na tutazalisha mazao ya kutosha kuhakikisha kwamba tunapata mafuta na sabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba hivi sayansi imegota kutengeneza mbegu ya zao la pamba ambayo inaweza kuwa ni mti? Ukilimwa leo unapaliliwa miaka mitano ili wananchi wasiwe wanalima kila mwaka ili tuwe na uhakika wa kuvuna miaka yote. Kwa sababu wananchi wetu wanahangaika sana kila mwaka kulima zao hili. Hivi sayansi imegota ndugu zangu? Tuone utafiti ambao unaoweza kusaidia ili tuweze kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninampongeza sana Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba na Wataalam wake kwa kusimamia zao hili muhimu. Ninaomba, wananachi wamenituma mbegu za pamba ziwe zinakwenda mwezi wa Septemba. Maana wanapolima mwezi wa Oktoba na wa Novemba haya ni mazao ambayo sasa yanaonekana hata wadudu hawapati shida kwenye kupulizia. Kwa hiyo, ninaomba sana mbegu za pamba ziweze kwenda mwezi wa Septemba. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Tabasam.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba suala la kugawa mbegu za pamba liendane na dawa za pamba na mbolea wakati huo huo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga unapokea taarifa?

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea naunga mkono. Kwa sababu ardhi yetu kule Kanda ya Ziwa imechoka. Nampongeza Waziri hapa amesema hatafanya kazi nyingine bora mbolea iende kwa wakulima. Tatizo kubwa tulilonalo sisi kule, mvua yetu ni ya wastani na wananchi wetu wanapata taabu kutumia mbolea hii. Wanataka mbolea ya samadi au mbolea ambayo inaweza kuendana na hali ya hewa kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa ndipo utafiti sasa unatakiwa utumike kwa hali ya juu sana. Hili nakwenda na kwenye mbegu, nimesikia hapa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba mbegu za asili, mbegu za mahindi, mbegu za alizeti, mbegu za pamba za asili zitaanza kutumika. Nchi ikikosa mbegu za asili ni hatari. Kwa hiyo, nakupongeza sana kwa sababu vituo vyetu vya utafiti vimeanza kuizalisha mbegu hii na kuwa nyingi. Mbegu hii ndiyo ambayo inavumilia magonjwa mbalimbali ambayo yanakuja kutuathiri Watanzania na kutuondolea kabisa tija ya mazao. Kwa sababu tatizo tunalohangaika nalo hapa ni tija. Mazao tunazalisha kidogo kwa sababu ya wadudu kuwa wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho tusijifungie, dunia imekwisha kubadilika. Kule duniani nchi za wenzetu zilizoendelea wana kilimo cha aina mbalimbali ambacho kinasaidia. Kwa mfano, kuna mbegu za mahindi ambazo zinaweza kutoa mafuta ya kula na mafuta mengine. Hebu tutafiti, tuone namna ambavyo tunaweza kulifanya Taifa likawa na mazao mbadala mchanganyiko ambayo yanaweza kusaidia. Hata maua pia, kuna maua yanatoa mafuta halafu hayo hayo majani yanakwenda kulisha mifugo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri umeleta mfumo mpya, watu wako leo wanavaa sare za kilimo, tuone sasa kwamba wanamfikia mkulima na kwa sababu umeamua jambo hili na sisi tunakuunga mkono. Wewe bado ni kijana, wewe bado una nia njema, wewe bado una mtazamo, tunauhakika kilimo chetu kinakwenda kubadilika. Tuombe wataalam wako wakusaidie, kama hawatakusaidia walete mbele ya Bunge tuweze kukusaidia hao ambao hawawezi kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)